Itabadilisha mwelekeo wa biashara na urahisi wa huduma za fedha kwa wafanyabiashara na wateja nchini.
27 Novemba 2025 – Dar es Salaam, Tanzania: Vodacom Tanzania, kampuni inayoongoza katika huduma za mawasiliano nchini, imezindua rasmi huduma ya malipo ya kimataifa (M-Pesa Global Payments), hatua itakayoleta mageuzi ya kibiashara nje ya mipaka ya Tanzania na kuongeza ujumuiswaji wa kifedha kidigitali.
Kupitia ushirikiano na VISA, Alipay, Network International, Magnati na MTN Uganda, wateja sasa wanaweza kufanya miamala ya malipo kwa kutumia mfumo wa Tap & Pay duniani kote kwa kutumia kadi ya kidigitali ya M-Pesa Visa kwenye machine ya malipo, kulipa wafanyabiashara nchini China kupitia Alipay kwa njia inayowezeshwa na Thunes, kufanya miamala Dubai kupitia wafanyabiashara waliounganishwa kwenye mfumo wa TerraPay, pamoja na kuwalipa wafanyabiashara nchini Uganda moja kwa moja kupitia MTN MoMo. Haya yote yanawezekana kupitia menyu ya M-Pesa (*150*00#) au M-Pesa Super App.
Huduma hizi ni salama, rahisi kutumia na zinaondoa changamoto zinazotokana na mifumo ya kibenki. Kwa pamoja, zimeifanya M-Pesa kuwa moja ya mifumo ya malipo ya kidigitali iliyoendelea zaidi barani Afrika.
Ubunifu huu unajibu mahitaji yanayoongezeka ya wateja na wasafiri wa Kitanzania wanaofanya miamala mara kwa mara katika uwanda wa Afrika Mashariki, Mashariki ya Kati, barani Asia na maeneo mengine duniani, lakini hukabiliana na changamoto za gharama, ucheleweshaji au usalama wa baadhi ya mifumo ya malipo.
Epimack Mbeteni, Mkurugenzi wa M-Pesa Vodacom Tanzania, alisema: “Ushirikiano wetu na VISA, Alipay, Network International na MTN Uganda unaonyesha dhamira yetu ya kujenga mifumo imara na uliounganishwa wa malipo ya kidigitali. Kwa pamoja, tunawawezesha wateja na wafanyabiashara kufanya miamala hata wavukapo mipaka ya Tanzania kwa urahisi ule ule wanaoufanya ndani ya nchi, kwa usalama, haraka na kwa gharama nafuu,” alisema Mbeteni.
Mkurugenzi huyo aliongeza kwamba, “hili ndilo lengo kuu la M-Pesa: kuendeleza ujumuishwaji wa kifedha na kuhakikisha ubunifu wa kidigitali unawanufaisha wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa. Kupitia nguvu hii ya pamoja, tunafungua njia mpya za biashara, kupunguza gharama za uendeshaji na kuwapa wateja uhuru mpana wa kushiriki katika uchumi wa kidigitali wa kimataifa.”
Uzinduzi huu unaleta suluhisho jipya liitwalo M-Pesa Tap & Pay (Gusa Ulipie) kwa ushirikiano na Visa, ikiwa ya kwanza barani Afrika, inayowawezesha wateja kulipa duniani kote kwa kutumia simu zao kupitia kadi ya kidijitali ya M-Pesa Visa.
Victor Makere, Meneja wa Nchi wa Visa Tanzania, alisema: “Kupitia ushirikiano huu, tunawawezesha mamilioni ya wateja wa M-Pesa kufurahia malipo ya kidigitali yaliyo salama na rahisi popote Visa inapokubalika. Teknolojia ya Tap & Pay ni huduma inayomruhusu mteja kulipa kwa kugusisha simu yake karibu na mashine ya malipo yenye mfumo wa Visa, bila kuingiza namba ya kadi au PIN. Malipo yanakatwa moja kwa moja kupitia kadi ya M-Pesa Visa iliyohifadhiwa ndani ya simu. Hii inaongeza usalama na urahisi, ikiruhusu wateja kufanya malipo duniani kote bila kufichua taarifa zao nyeti. Ubunifu huu unaunga mkono safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa malipo ya kidigitali na kuwawezesha wateja na biashara kulipa kwa njia za kisasa zaidi.”
Kupitia Mtandao wa Thunes, wateja wa M-Pesa sasa wanaweza kulipa wafanyabiashara nchini China ndani ya mfumo wa Alipay kwa kasi na usalama.
Andrew Stewart, Afisa Mkuu wa Mapato wa Thunes, alisema: “Urasimishaji wa malipo ya kuvuka mipaka kwa njia ya kidigitali ni hatua muhimu inayoongeza upatikanaji wa huduma na kusaidia dhamira yetu ya kuwawezesha mabilioni ya watumiaji kushiriki kikamilifu katika uchumi wa dunia. Kupitia ushirikiano wetu na Vodacom, sasa tunawezesha biashara za Tanzania kuwalipa wafanyabiashara wa China papo hapo kupitia mtandao wa Alipay. Kiwango hiki kipya cha uunganishaji na ubunifu kinaongeza imani katika mifumo ya kifedha ya simu na kufungua fursa mpya za biashara ya kimataifa”
TerraPay, ambayo inawezesha malipo ya kimataifa kwa wafanyabiashara, ikiwemo kuwawezesha watumiaji wa M-Pesa kufanya miamala na wafanyabiashara waliopo Dubai kupitia mtandao wao mpana wa malipo.
Akizungumzia umuhimu wa mkondo wa malipo wa Dubai, Willie Kanyeki, Makamu wa Rais wa TerraPay Kusini mwa Jangwa la Sahara, alisema: “TerraPay tunaamini katika uunganishaji wa mifumo na kuwezesha malipo bila mipaka. Ushirikiano wetu na Vodacom unapanua fursa za biashara kwa njia salama, kwa Watanzania wanaofanya shughuli za kibiashara Dubai, na kuwaunganisha watumiaji wa Afrika na masoko mapya ya kimataifa.”
Kwa upande wa miamala nchini Uganda kupitia MTN MoMo, MTN ina mchango muhimu katika kurahisisha biashara za kikanda kwa wajasiriamali wadogo na wa kati.
Richard Yego, Mkurugenzi wa Huduma za Fedha kwa Simu MTN Uganda, alisema: “Ushirikiano huu ni hatua muhimu kuelekea biashara huru na endelevu katika ukanda huu. Pamoja na Vodacom, tunafungua upatikanaji mkubwa wa huduma za kifedha kwa maelfu ya wafanyabiashara wanaovuka mipaka ya Uganda na Tanzania, hasa wale wa sekta ya biashara ndogo na za kati ambao ndio uti wa mgongo wa uchumi wa nchi zetu.”
Kwa kuzingatia matumizi makubwa ya huduma za fedha kwa simu na ongezeko la matumizi ya simu nchini Tanzania, masuluhisho haya ni nyenzo muhimu kwa wateja wa kila siku pamoja na biashara ndogo na za kati zinazohitaji huduma za kifedha za uhakika, haraka na rahisi.
M-Pesa ikiendelea kupanuka kama huduma salama na rahisi ya malipo ya kimataifa, Vodacom Tanzania inaendelea kutekeleza dhamira yake ya kujenga uchumi jumuishi wa kidigitali na kubadilisha maisha kupitia teknolojia.
