Waziri Aweso Asisitiza Ubunifu na Tafiti Kukabili Changamoto za Maji

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ameziagiza taasisi za Chuo cha Maji kuongeza juhudi katika kufanya tafiti zitakazosaidia kutatua changamoto za sekta ya maji nchini, zikiwemo mabadiliko ya tabianchi, upotevu wa maji na matumizi ya dira za malipo ya kabla (prepaid meters).

Akizungumza leo Novemba 27, 2025 wakati wa mahafali ya 49 ya chuo hicho yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, Waziri Aweso alisema jumla ya wahitimu 881 wamemaliza masomo yao mwaka huu, idadi ambayo imeongezeka ikilinganishwa na miaka iliyopita.

Amezielekeza mamlaka za maji nchini kuhakikisha zinatoa nafasi za ajira kwa wahitimu wa fani mbalimbali kutoka Chuo cha Maji, ili kuongeza ufanisi katika uendeshaji na usimamizi wa miradi ya maji mijini na vijijini.

Aweso ameahidi kuendelea kukiimarisha Chuo cha Maji ili kiwe miongoni mwa vyuo vinavyoongoza nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

“Mbali na kuwapatia nafasi wahitimu, pia Wizara itatoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi watano waliofanya vizuri na kupata alama za juu. Tutatoa ufadhili wa Shahada ya Uzamili kwa wanafunzi hao,” alisema Aweso.

Katika mahafali hayo, Waziri Aweso pia alizindua Bodi mpya ya Chuo cha Maji inayoongozwa na Dkt. Maulid Omar, akiitaka kusimamia kikamilifu utendaji wa menejimenti na kutoa ushauri endelevu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Adam Karia, alisema katika mwaka wa fedha 2024/2025 chuo kimefanya mapitio ya mitaala mitatu na kiko katika hatua za mwisho kukamilisha programu mbili za uanagenzi.