Njombe. Tabia ya kuchukua mikopo bila kuwashirikisha wenza inatajwa kuwa chanzo cha migogoro mingi na wakati mwingine kusababisha kuvunjika kwa ndoa na watoto kulelewa na mzazi mmoja, changamoto iliyoshuhudiwa katika halmashauri ya mji wa Makambako mkoani Njombe.
Hali hiyo hujitokeza baada ya mmoja wa wanandoa kuchukua mikopo kwenye vikundi bila ya kumshirikisha mwenza wake na baadaye kushindwa kulipa, jambo linalosababisha dhamana iliyowekwa kupigwa mnada.
Hayo yamesemwa leo Novemba 28, 2025 na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Magegele, kata ya Kivavi, Victor Nyato wakati akizungumza na waandishi wa habari huko Makambako mkoani Njombe.
Amesema baadhi ya wanaume wamelalamikia kitendo cha wanawake zao kujiingiza kwenye mikopo bila kuwashirikisha na kuanza kuuza vitu vya ndani hasa mahindi na mifugo ili kulipa madeni hayo.
Amesema licha ya wanawake hao kulalamikiwa na wanaume zao, kwa upande wao wamedai kuwaachiwa majukumu ya kimalezi na wanaume hali ambayo imesababisha wengi wao wajiingize kwenye vikundi vingi vya kuweka fedha na kukipa mikopo ili kuhudumia watoto.
“Huko majumbani kuna siri nyingi wanawake wengi wamekuwa wakibeba mizigo mikubwa ya kulea familia wanaume wengi wamekuwa hawashiriki kwa wakati siyo wote ni baadhi,” amesema Nyato.
Amesema kutokana na changamoto ambazo amezipokea kutoka pande zote mbili, serikali ya mtaa huo itaweka utaratibu wa kundi la wanaume na wanawake kukutana kila baada ya miezi mitatu ili kujadili changamoto zao na kuona namna ya kuzitatua, lengo likiwa ni kuhakikisha jukumu la malezi linatekelezwa na wazazi wote wawili.
Kwa upande wa wanaume wa mtaa wa Magegele, wakiwakilishwa na Hamshidina Ndendya, wamesema wapo baadhi ya wanaume hawashiriki malezi ya watoto lakini kilio kikubwa cha wanandoa ni wanawake kujihusisha na mikopo umiza bila kuwashirikisha, hali inayosababisha migogoro ndani ya familia.
“Tunatakiwa kujenga umoja wenye nguvu wa wanaume, tufike sehemu tusimame kama baba kwenye familia ili tutengeneze familia iliyo bora,” amesema Ndendya.
Nao baadhi ya wanawake wa mtaa huo wa Magegele akiwemo Dorah Julius, amesema wengi wao wanajiingiza kwenye vikundi na mikopo kutokana na wanaume kutotimiza wajibu wao.
“Saa nyingine vikundi hivi vinatusaidia kusomesha watoto, pia, kutunza mazao au kutoa msaada kwa ndugu zake,” amesema Julius.