::::::::
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema Kumekuwepo na ongezeko la Joto katika baadhi ya maeneo hapa nchini hususan yale yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka kwa miezi ya hivi karibuni.
Hali hiyo imesababishwa na kusogea kwa Jua la Utosi sambamba na upungufu wa mvua unaojitokeza katika maeneo hayo.
Kupitia taarifa iliyotolewa na TMA imesema kuwa Kwa kawaida vipindi vya Jua la Utosi nchini hufikia kilele mwishoni mwa mwezi Novemba wakati Jua la Utosi likiwa linaelekea kusini (Tropiki ya Kaprikoni) na hali hiyo hujirudia tena mwezi Februari wakati Jua la Utosi likiwa linaelekea kaskazini (Tropiki ya Kansa).
Aidha amesema Jua la Utosi huambatana na hali ya ongezeko la Joto kwa sababu uso wa Dunia katika eneo tajwa huwa karibu zaidi na Jua kuliko maeneo mengine.
Katika kipindi cha mwezi Novemba, 2025 hali ya ongezeko la Joto imeendelea kujitokeza katika baadhi ya maeneo nchini, ambapo hadi kufikia tarehe 27 Novemba, 2025 kituo cha hali ya hewa cha Moshi (Kilimanjaro) kiliripoti kiwango cha juu zaidi cha nyuzi joto 35.7°C mnamo tarehe 21 Novemba, 2025 ikiwa ni ongezeko la nyuzi joto 4.2°C ukilinganisha na wastani wa muda mrefu kwa mwezi Novemba katika kituo hicho.