Ridhiwani: Nipo tayari kuhojiwa kuhusu tuhuma za vituo vya Lake Oil

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amesema yuko tayari kuhojiwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ili kuweka wazi tuhuma zinazomkumba kuhusu umiliki wa vituo vya mafuta vinavyodaiwa kuwa vya Lake Oil.

Akizungumza na watumishi wa wizara hiyo jijini Dodoma, Novemba 26, 2025, Ridhiwani amesema taarifa kuhusu maadili ya watumishi wa umma zinafaa kuwa wazi na pale panapokuwa na mashaka, wahusika waitwe kuhojiwa na ushahidi ukawe wazi kwa umma. 

“Malalamiko juu ya viongozi yamekuwa mengi sana; haijulikani lipi ni kweli na lipi si kweli,” amesema.

Waziri alisema mfano wa maandamano yaliyofanyika juzi uliibua malalamiko kuhusu maadili ya viongozi, akirejea ripoti kwamba kuna mtu anayeitwa Ali Edha Awadh, ambaye vituo vyake vya petroli vya Lake Oil vimehusishwa na kumilikiwa na Waziri. Ridhiwani amewataka wajumbe wa tume ya maadili wamuite bila hofu ili aeleze ukweli.

Pia, amependekeza tume ifanye uchunguzi wa kina kabla ya kukutana na waandishi wa habari na kuwasilisha ushahidi wa ziada ambao, anasema, unaweza kusaidia kuwapa wananchi taarifa sahihi na uhakika.