SERIKALI YATANGAZA MIKAKATI 8 KUVUTIA UWEKEZAJI, KUONGEZA AJIRA KWA VIJANA


 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo ametangaza mikakati mahsusi nane ya serikali yenye lengo la kuongeza uwekezaji na kupanua fursa za ajira kwa vijana nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) pamoja na kongamano la uwekezaji jijini Dar es Salaam, Prof. Kitila alisema serikali imejipanga kuweka mifumo na programu maalum za kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika sekta ya uwekezaji.

Amesema miongoni mwa hatua hizo ni kuanzishwa kwa Kituo Maalum cha Kuhudumia na Kuwezesha Wawekezaji Vijana (Youth Investors Resource Centre) kitakachotoa mafunzo na huduma za uwezeshaji. Kituo hicho kitakuwa Mabibo jijini Dar es Salaam na kitakuwa na uwakilishi katika ofisi za TISEZA mikoani.

Prof. Kitila alibainisha kuwa kituo hicho kinatarajiwa kuzinduliwa kabla ya mwisho wa mwaka huu, sambamba na programu maalum ya kuwawezesha vijana kuanzisha uwekezaji wa viwanda katika maeneo mbalimbali yaliyotengwa mahsusi nchini.

Katika hatua nyingine, serikali imetenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji wa vijana wakiwemo wahitimu wa vyuo vikuu na vyuo vya ufundi. Maeneo hayo ni Dodoma (Nala, ekari 100), Pwani (Kwala, ekari 20), Mara (Bunda, ekari 100), Ruvuma (Songea, ekari 100) na Bagamoyo (ekari 20).

Ameongeza kuwa programu hiyo itahusisha mafunzo, upatikanaji wa ardhi, uunganishwaji na wazalishaji wa mitambo na malighafi, pamoja na kuwaunganisha vijana na benki washirika kama Azania Bank, TCB na CRDB.

Aidha, serikali imepanga kusogeza huduma za TISEZA katika kila mkoa ifikapo mwaka 2028, ambapo kutakuwa na kituo maalum cha kutangaza na kuwezesha uwekezaji kwa kushirikiana na TAMISEMI.

Wakati huo huo, baadhi ya wananchi wamejitokeza kutoa maoni kuhusu utekelezaji wa mikakati hiyo, wakisisitiza umuhimu wa kuzijumlisha halmashauri katika kupanga na kutekeleza ajira kwa vijana, huku wengine wakitaka uongozi kuongeza kasi katika kutafuta suluhisho la changamoto za vijana.