Sharia ya unyonyeshaji inayoharamisha kuoana

Kunyonyesha ni jambo nyeti na lenye athari kubwa katika uhusiano baina ya watu. Hutengeneza hukumu (sharia) nyingi na mtu ataulizwa mbele ya Allah.

Mwanamke Muislamu asimnyonyeshe mtoto wa mama mwingine bila dharura. Na ikibidi Inapasa ifanyike katika hali iliyo wazi na uwepo wa mashahidi, kadhalika ijulikane baina ya familia zote mbili (familia ya mama mzazi na mama mwingine wa kunyonyesha).

Mwanamke anayenyonyesha awe mwaminifu katika dini, tabia na afya. Inapasa aweke kumbukumbu ya watoto aliowanyonyesha ili kuepusha ndoa zisizofaa. Wazazi wa nasaba (asili) wawe na jukumu la kumueleza mtoto wao kuhusu kunyonyeshwa huko. Mtoto akikua hapaswi kubeza jambo hili bali ajiepushe hata kwa shaka ndogo.

Unyonyeshaji wa watoto wengine hutengeneza uhusiano wa kindugu sawa na ule wa damu (kinasaba) kati ya familia asili ya mtoto anayenyonyeshwa na familia nyingine (isiyokuwa asili) ya mama aliyemnyonyesha.

Kama aliyenyonya ni mtoto wa jinsi ya kiume, basi ni haramu mtoto huyo kuwaoa wanawake tisa wafuatao: Mosi, mwanamke aliyemnyonyesha (mama wa kunyonya) kwa sababu ni mama yake kwa kitendo cha kunyonya ziwa lake. Allah Mtukufu amesemaNa mama waliowanyonyesha (ni haramu kuwaoa)….” (4:23).

Pili, mabinti wa mama mnyonyeshaji aliowazaa na mume wake wa sasa au wa zamani, kwa sababu hawa wanakuwa dada zake kwa kunyonya ziwa moja. Allah Mtukufu anasema:

“ Mmeharamishiwa…na dada zenu kwa kunyonya” (4:23). Tatu: ndugu wa kike wa mama aliyenyonyesha; kwa sabau hawa wanakuwa mama zake wadogo au wakubwa kwa kunyonya. Nne: Wajukuu wa mama myonyeshaji; kwa sababu hawa wanakuwa mabinti wa dada zake kwa kunyonya.

Tano. Mama mzazi wa mnyonyoshaji; kwa sabbau anakuwa bibi yake mzaa mama kwa kunyonya. Sita; Dada wa mume mnyonyeshaji; kwa sababu anakuwa shangazi yake kwa kunyonya. Saba: Binti wa mtoto wa kiume wa mama aliyemnyonyesha; kwa sabbau anakuwa ni binti wa kaka yake kwa kunyonya. Nane: binti wa mume aliyemnyonyesha, huyu anakuwa dada yake kwa kunyonya upande wa baba. Tisa: Mke mwingine wa mume aliyemnyonyesha, huyu anakuwa mke wa baba yake kwa kunyonya.

Na kama mtoto aliyenyonya ni wa jinsi ya kike, basi ni haramu mtoto huyo kuolewa na wafuatao: Mosi. Mume  wa mnyonyeshaji; kwa sababu ni kama baba yake wa asili (nasaba). Pili, ndugu zake mume mnyonyeshaji; kwa kuwa ni ami zake kwa kunyoya. Tatu: Baba mzazi wa mume mnyonyeshaji, kwa kuwa ni babu yake kwa kunyoya,  Mtume wa Allah amesema: 

“Unyonyeshaji unaharamisha yale (mambo) yanayoharamishwa na nasaba.” (Bukhar na Muslim). Ikiwa watoto wawili wamenyonya kwa mama mmoja (ambaye kiasili si mama yao mzazi), basi nao ni haramu kuona, wanakuwa ni ndugu wa kunyonya ziwa moja.

Hapa ni vema ikafahamika wazi kwamba sharia hii inamuhusu mtoto aliyenyonya tu, na wala haiwagusi ndugu zake wengine ambao hawakunyonya naye ziwa moja.

Kunyonya kunathibitika kwa ushahidi wa mwanamke mmoja muadilifu, ambaye hana tuhuma wala maslahi binafsi katika jambo hilo. Hadithi ya Uqbah bin al-Harith ambaye alimwoa binti wa Ihab. Kisha mwanamke moja akaja na kusema: “Niliwanyonyesha nyote wawili.” Akataja jambo hilo kwa Mtume wa Allah, Hapo Mtume akamkataza kuendelea kuishi naye.

(Bukhari na Muslim). Ikiwa mwanaume amemuoa mwanamke ambaye ni haramu kwake kwa sababu ya kunyonya ziwa moja bila kujua, kisha akaishi naye: Wakapata watoto, nasaba yao inahesabiwa kwa baba na mama, na watoto hao wanawarithi wazazi wao, ila mume na mke hawarithiani.

Mwanamke atakaa eda baada ya talaka au kuachana, kisha anaweza kuolewa tena. Kuharamishwa kwa sababu ya uhusiano wa ndoa kwa sababu ya ukwe (muswahaara) kunabaki vilevile. Hivyo mwanamume hawezi kuoa wazazi au watoto wa mwanamke huyo, wala yeye hawezi kuolewa na wazazi au watoto wa mume huyo.

Masharti ya unyonyeshaji unaoharamisha

Mosi. Uwepo Uhakika wa kupita maziwa kutoka kwa mama (mnyonyeshaji)  kwenda kwa mtoto. Ikiwa kuna shaka, hakuna hukumu (sharia) ya uharamu. Pili, Maziwa yaingie tumboni mwa mtoto, kwa kunyonya moja kwa moja au kumiminwa mdomoni au puani.

Tatu, Mtoto awe chini ya miaka miwili. Allah amesema: Na mama huwanyonyesha watoto wao kwa miaka miwili kamili.” (2: 233). Nne, Kunyonyeshwa kuwe ni mara tano kamili au zaidi  kwa mujibu wa kauli yenye nguvu zaidi miongoni mwa wanazuoni si chini ya hapo.

Hukumu zinazohusiana na unyonyeshaji

Undugu wa kunyonya ziwa moja na  ule wa nasaba (asili) sharia zao zinafanana katika upande wa uhalali wa kuangaliana, kusafiri pamoja, kukaa faragha na kusalimiana kwa kukumbatiana. Na zinazotofautiana kwamba hakuna urithi kwa sababu ya undugu wa kunyonya pamoja.

Na wala hakuna wajibu wa kutoa nafaka (matunzo) baina ya ndugu wa kunyonya pamoja. Baba wa kunyonyonya hawezi kuwa msimaizi (walii) katika ndoa ya binti yake wa kunyonya.