Dar es Salaam. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimeanza safari ya kutekeleza mkakati wa kutoa elimu kidijitali kwa kuunganisha kampasi zake zote kwa teknolojia na mawasiliano ili kutoa nafasi kwa shughuli za kitaaluma kufanyika popote.
Hatua hii ni utekelezaji wa mpango wa miaka 10 (2022- 2032) wa kukifanya chuo hicho kuwa kampasi janja unaolenga kuimarisha miundombinu ya tehama ili kuboresha ufundishaji na utoaji wa huduma mbalimbali kwa sababu tumeweka msisitizo mkubwa kwenye kufundisha na kujifunza kwa kupitia tehama.
Kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) leo Novemba 28,2025 chuo hicho kimesaini mikataba 12 yenye thamani ya Sh10.3 bilioni kwa ajili ya kufunga samani na miundombinu ya tehama kwenye majengo 21 ya chuo hicho.
Ufungaji huo wa vifaa vya teknolojia na miundombinu unahusisha majengo mapya 21 kwenye maeneo mbalimbali ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kampasi zake zilizopo Dar es Salaam, Lindi, Kagera na Zanzibar.
Makamu Mkuu wa chuo hicho Profesa William Anangisye amesema lengo la UDSM ni kuimarisha miundombinu ya tehama kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma ikiwemo kufundisha na kujifunza kwa njia za kisasa.
Amesema utekelezaji wa mradi wa HEET unafanyika sambamba na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050 ambavyo vyote vinalenga katika kuimarisha uchumi wa viwanda ili kuendana na uchumi wa kati, na kuongeza fursa za ajira kwa makundi mbalimbali hususan vijana.
Aidha amesema mradi huo unarandana na Dira ya UDSM 2061, Mpango Mkakati wa Chuo 2020/21-2024/25 na Mpango wa 2022-2032 wa Kufanya UDSM kuwa Kampasi Janja.
“Mahitaji ya utekelezaji ni makubwa, hivyo mradi wa HEET unachangia asilimia 60 tu ya UDSM Smart Campus Roadmap (2022-2032), chuo kimejipanga kuimarisha miundombinu ya tehama ili kuboresha ufundishaji na utoaji wa huduma mbalimbali kwa sababu tumeweka msisitizo mkubwa kwenye kufundisha na kujifunza kwa kupitia tehama,” amesema Profesa Anangisye.
Akizungumza kwenye hafla hiyo ya utiaji saini mikataba mwenyekiti wa baraza la chuo hicho Balozi Mwanandi Maajar amepongeza hatua hiyo ya kuwekeza kwenye miundombinu ya tehama kwa kile alichoeleza inaenda kuchagiza kwenye utekelezaji wa mitaala mipya.
“Ninafurahi pia kuona kwamba chuo kinatambua umuhimu wa matumizi ya tehama kama nyenzo muhimu katika kufundishia na kujifunzia. Mitaala mipya mliyoiandaa haitakuwa na tija ikiwa hakutakuwa na miundombinu thabiti ya kuwezesha matumizi ya mbinu za kisasa za kufundishia na kujifunzia.
“Nimekua nikifuatilia kwa karibu mikakati ya chuo kwenye kumaliza tatizo la mtandao wa intaneti chuoni kwani chuo chetu ni kikongwe, hivyo kinapaswa kuwa mfano kwa vyuo vingine hususani kwenye matumizi ya tehama na ubora wa wahitimu wake”.
Balozi Maajar amesema baraza lina imani kubwa kuwa kampuni zilizosaini mikataba na kuzitaka kuwa wanao wajibu mkubwa wa kwenda kutekeleza majukumu yao katika viwango na ubora huohuo tuliojiwekea.
“Tunayo matarajio kuwa kampuni hizi zitatekeleza wajibu wao kwa weledi na ufanisi wa hali ya juu, kwani Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimeweka mikakati thabiti ya kuhakikisha stahiki na rasilimali zinazohitajika katika utekelezaji wa majukumu yenu zinapatikana kwa kadri ya makubaliano na kwa wakati,” amesema Balozi Maajar.
Mtaalamu wa Teknolojia ya Habari, Catherine Mushi amesema hatua ya UDSM kuwekeza kwenye miundombinu ya kisasa ya tehama inaendana na mabadiliko ya kimataifa ya utoaji maarifa.
Amesema kupitia tehama itaimarisha uwezo wa wahadhiri kutumia mfumo jumuishi wa ufundishaji, na wanafunzi watanufaika kwa kupata masomo popote kwa ufanisi,” amesema.
“Dunia inaelekea kwenye matumizi makubwa ya mifumo ikolojia ya kidijitali. Vyuo vikuu vinavyowekeza sasa ndiyo vitakuwa kitovu cha ubunifu, tafiti zenye tija na ufundishaji unaozingatia ushindani wa kimataifa” amesema Catherine.
Catherine amebainisha kuwa mpango wa huo wa Kampasi Janja unaipa Tanzania nafasi ya kuwa kitovu cha elimu ya juu katika ukanda huo.
“Vyuo vingi leo vinashindana sio kwa ukubwa wa majengo, bali kwa ubora wa mifumo ya tehama. UDSM ikikamilisha asilimia 100 ya Smart Campus Roadmap, kitakuwa miongoni mwa taasisi chache barani Afrika zinazowezesha huduma zote ujifunzaji, utafiti na utawala kupatikana kidijitali,” amesema.
Mdau wa elimu ya juu ambaye pia ni mhadhiri mstaafu Dk Joyce Mshiko amesema mabadiliko ya kuelekea ufundishaji wa kidijitali yanahitaji pia uwekezaji katika mafunzo ya wahadhiri.
“Miundombinu ni msingi, lakini mafanikio makubwa yatapatikana ikiwa wahadhiri watajengewa uwezo wa kutumia zana kama Learning Management Systems (LMS), maabara pepe, na mfumo wa darasa la mseto (blended learning). Katika hilo, UDSM inaonekana kuchukua hatua sahihi,” amesema.