WAFANYAKAZI WA NYUMBANI MWANZA WAPATIWA ELIMU YA KUTAMBUA HAKI NA WAJIBU WAO

:::::::

SHIRIKA la Kazi Duniani (ILO),WoteSawa kwa kushirikiana na Chama cha Wafanyakazi wa Nyumbani,Hifadhi,Hotelini,Huduma za Jamii na Ushauri (CHODAWU),limewakutanisha Wafanyakazi wa nyumbani takribani 100 Mkoani Mwanza kwa lengo la kuwapatia maarifa ya kuwasaidia kutambua haki zao na kuboresha mazingira yao sehemu za kazi kupitia Mradi wa Kuboresha Utambuzi na Mazingira ya Kazi kwa Wafanyakazi Nyumbani Tanzania kama Watoa Huduma.

Akizungumza jana jijini Mwanza,wakati wa Ufunguzi wa Mafunzo kwa Wafanyakazi hao wa Nyumbani,Mratibu wa Mradi wa Kuboresha Utambuzi na Mazingira ya Kazi kwa Wafanyakazi Nyumbani kama Watoa Huduma kutoka ILO Ofisi ya Afrika Mashariki,Chiku Semfuko alisema wafanyakazi wa nyumbani ni kama wafanyakazi wengine na sheria za kazi zimeweza kuwatambua.

Alisema licha ya sheria kuwepo lakini bado kundi hilo linakabiliwa na changamoto mbalimbali bado wanaumuhimu wa kupatiwa elimu ya kujua haki zao na kutambua wajibu wao mahali pa kazi.

”Kupitia mafunzo haya tunayoendelea kuyatoa kwa Wafanyakazi wa nyumbani, tunajaribu kuweka mazingira wezeshi ili tuboreshe mazingira yao ya kazi.

”Kiukweli kazi za ndani ni ngumu,wengi wetu tunafanya kazi Ofisini na tunafanya kazi kwa utulivu kwa sababu tunajua nyumbani kuna mtu ambaye anatusaidia kwa utulivu na kufanya kazi ya usafi,kuangalia watoto,Ulinzi na wakati mwingine ni Mkufunzi hivyo tunapaswa kuheshimu kazi zao na kuwaweka katika mazingira mazuri,”alisema.

Semfuko alisema ILO inafanya kazi na taasisi tofauti tofauti kama Shirika la Wotesawa kwa sababu wafanyakazi wa nyumbani wapo kila sehemu hivyo wameona ni bora kuunganisha juhudi zao kwa pamoja ili kuleta uelewa zaidi na kubadilisha taswira zilizopo kwa wanajamii kuona wafanyakazi wa nyumbani kama ni wezi na hawastahili kupata haki zao.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Sheria kutoka CHODAWU Taifa,Asteria Gerald alisema miongoni mwa jitihada ambazo CHODAWU inaendelea kuzifanya ni pamoja na kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa nyumbani nchi nzima.”Wiki iliyopita tulikuwa na kundi la wafanyakazi wa nyumbani kutoka mikoa mbalimbali Mkoani Arusha na tulihakikisha kwamba tunatengeneza kundi la waelimisha rika ambao ni wafanyakazi wa nyumbani wenyewe.

”Ni vigumu sana kwa jamii kuongelea kundi fulani wakati wenyewe hawapo,kwahiyo tumewatengeneza wafanyakazi wa nyumbani kama waelimisha rika ambao wao wenyewe watakuwa waelimishaji wa wafanyakazi wa nyumbani wenzao juu ya haki zao na wajibu wao mahali pa kazi.

“Tumekuja na Waelimisha rika wanne ambao wanatoa mafunzo yatakayowajengea uwezo kufahamu haki zao ili nao wakawe mabalozi wa kuelimisha wafanyakazi wa nyumbani wengine wa mkoa wa Mwanza,”amesema. 

Gerald alisema CHODAWU imeendelea kupambana kuhakikisha kwamba wafanyakazi wa nyumbani nchini kote wanapata elimu na elimu hiyo kwa kutumia semina au mafunzo mbalimbali huku kuwapeleka wafanyakazi hao katika Vyuo vya Veta na kupatiwa elimu

”ILO kwa kushirikiana na vyuo mbalimbali wanapambana kuhakikisha wafanyakazi wa nyumbani wanakuwa ni wafanyakazi ambao wataalamu wa kazi za nyumbani ambapo kwa mara ya kwanza mwaka huu tumeingia mwanza na kuhakikisha tunaondoa dhana mbaya kwa jamii juu ya wafanyakazi hao,”alisisitiza

Alisema kupitia mafunzo na semina hizo zinazoendelea kutolewa kwa kundi hilo Chodawu inatarajia kupata Wafanyakazi wa Nyumbani ambao wanajua wajibu wao,sheria na kanuni zinazowaongoza katika kazi zao.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la WOTESAWA kutoka Mkoani Mwanza,Angela Benedicto alisema wafanyakazi hao waliohudhuria mafunzo hayo wapo katika makundi mawili ikiwemo kundi la Wamama wanaofanyakazi za nyumbani kwenda na kurudi na kundi la pili ni la wasichana wanaoishi na mabosi zao lengo likiwa kuwajengea uwezo wa kufahamu haki zao,wajibu,Mikataba na Sheria zinazowahusu.

”Hii yote ni kuhamasisha kazi za staha na kuvunja ukatili kwa kazi za nyumbani na kutaka kuwepo kwa mahusiano mazuri kati ya mwajiri na mwajiriwa katika kila mmoja kutambua wajibu wake na kutekeleza ipasavyo,”alisema

Moja ya Wafanyakazi hao kutoka Mkoani Mwanza,Elizabeth John alisema wafanyakazi wa nyumbani wanapitia changamoto nyingi sana ikiwemo baadhi ya waajiri wanakuwa wanawanyanyasa kwa kuwacheleweshea mishahara yao na kushindwa kuwalipa kwa wakati.





 Mwishoooo