Dar es Salaam. Wananchi wa Kata ya Mbezi, hususani maeneo ya Msakuzi, Mpiji Magohe, Msumi na Saranga wamemlalamikia Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, kuhusu uhaba wa majisafi na salama unaowakabili kwa miaka mingi, wakimtaka kuwapa mpango wa dharura wa kupata huduma na kutoa suluhisho la kudumu.
Wamesema baadhi ya maeneo yamefikiwa na miundombinu ya maji, lakini huduma hupatikana usiku wa manane hali inayovuruga maisha ya familia na hata kuhatarisha ndoa kutokana na usumbufu wa kuamka usiku kukinga maji.
Pia wamelalamikia kutokuwapo viwango vya wazi vya gharama za kuunganishiwa huduma ya maji, wakieleza baadhi hutozwa kiasi kikubwa, huku wengine wakitozwa kidogo bila maelezo yanayoeleweka.
Wameeleza hayo leo Novemba 28, 2025 mbele ya waziri huyo aliyefanya ziara maeneo hayo akifuatana na viongozi mbalimbali, akiwapo Mbunge wa Kibamba na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki.
Wananchi hao wamesema hulazimika kutumia maji ya visima ambayo hawana uhakika na ubora wake, hivyo kuwa katika hatari ya kupata magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu.
“Waziri hapa Mpiji Magohe tangu nchi kupata uhuru hatujawahi kupata huduma ya maji na hata maeneo ya jirani yaliyofikiwa na huduma maji hayatoki, imekuwa shida kutafuta huduma hii. Waziri umekuja tunataka majibu au hatua za dharura ili tupate huduma,” amesema Beatrice Liwa.
Diwani wa Kata ya Mbezi, Pius Nyantori amesema eneo la Mpiji Magohe hata maeneo machache yaliyofikiwa na mtandao wa maji bado yanakabiliwa na tatizo kwani hutoka usiku pekee.
“Hata sehemu zinazopata huduma hiyo, maji yanatoka usiku badala ya mchana. Tunaomba yatoke mchana ili wananchi waweze kujaza kwenye vifaa vyao,” amesema.
Pia amelalamikia gharama kubwa za kuunganishiwa maji, akieleza biashara ya maji imekuwa kubwa na inawaumiza wananchi wa kipato cha chini.
Mbunge wa Kibamba, Kairuki amesema hata maeneo ya Mpiji Mwisho na Stendi ya zamani hayana huduma ya maji.
“Mbezi Mpiji Makondeni, Torino hakuna huduma ya maji pia. Tunaomba mtuangalie kwa jicho la huruma na ikiwezekana tupate huduma ya dharura ya matenki wakati mikakati ya kudumu ikiendelea kutafutwa,” amesema.
Amesema iwapo mgawo wa maji utalazimika kufanyika, basi ratiba itolewe wazi na maji yatoke mchana kwani usiku wengi wanakuwa wamelala na kushindwa kuyafuata.
Waziri Aweso amekiri kuwepo kwa changamoto ya upatikanaji wa maji katika baadhi ya maeneo ya Kibamba, akitaja maeneo mengine sugu kwa tatizo hilo ni Kinyerezi na Ubungo.
Amesema huenda baadhi ya watendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) wanahusika katika kufanya biashara ya maji kwa masilahi binafsi.
“Niwaombe nisaidieni kufanya kazi kwa weledi. Sikatai biashara ya maboza, lakini inakuwaje maeneo haya yana shida ya maji kila siku na kila mwaka? Mkurugenzi na Katibu Mkuu, naomba lifanyiwe kazi jambo hili,” amesema.
Kuhusu suluhisho la kudumu Mpiji Magohe, ameuagiza uongozi wa Dawasa kukamilisha kazi ya ujenzi wa mradi wa maji wenye thamani ya Sh900 milioni ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa wakati na bila usumbufu.
“Mkurugenzi wa Dawasa na Bodi naombeni simamieni shughuli hii mradi ukamilike haraka, wananchi wapate huduma ya maji. Sihitaji kusikia malalamiko haya,” amesema.
Amesema kukamilika kwa mradi huo kutafungua fursa kwa wananchi kuunganishiwa maji bure, huku malipo yakifanyika kidogo kidogo kupunguza mzigo wa gharama.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mkama Bwire amesema maagizo yote atafanyia kazi ili wananchi wapate huduma.
Waziri Aweso amesema huduma hiyo inapaswa kupangwa kwa ufanisi ili kuepusha usumbufu haitakiwi kutolewa usiku.
“Msivunje ndoa za mama zetu. Inakuwaje Dawasa mnatoa maji usiku kama shughuli za kuwanga? Huo muda mngeutumia kujaza matenki badala ya kutoa maji usiku,” amesema.
Amesema Serikali itanunua pampu mpya ili kuongeza nguvu ya kusukuma maji na kuhakikisha maeneo yote yenye mtandao wa maji yanapata huduma kikamilifu.
Kuhusu gharama, Aweso amesema wizara itakuja na bei elekezi baada ya kubaini kuwepo kwa watumishi wanaojipangia viwango vyao.
“Tunataka mtu kuunganishiwa maji ndani ya siku saba. Hili tutaliwekea utaratibu maalumu,” amesema.
