:::::::::::
Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, ameielekeza Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kufanya kazi kwa kasi, weledi na ushirikiano ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa Watanzania.
Akizungumza Novemba 28, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake katika Mamlaka hiyo, Waziri Kapinga aliambatana na Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Suleiman Serera, pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Biashara, Sempeho Manongi, ambapo alikutana na Bodi na Menejimenti ya TANTRADE.
Amisisitiza umuhimu wa mifumo ya TEHAMA ndani ya Mamlaka hiyo kusomana ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa za masoko kwa kutumia teknolojia rahisi na rafiki kwa wananchi.
Aidha, ameitaka TANTRADE kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria, huku akihimiza kuhuishwa kwa sheria hizo ili ziendane na mazingira ya sasa ya biashara, hatua itakayosaidia kuvutia wawekezaji na kuimarisha maendeleo ya biashara nchini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TANTRADE, Profesa Ulingeta Mbamba, ameihakikishia Serikali kuwa Mamlaka iko tayari kutekeleza maagizo hayo ili kuchochea maendeleo ya biashara kwa manufaa ya Taifa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE, Dkt. Latifa Khamis, amesema Mamlaka hiyo inaendelea kuboresha huduma zake kwa wananchi, ikiwamo kuanzisha ofisi katika mikoa mbalimbali, hususan ile ya mipakani ambayo ni ya kimkakati katika kukuza biashara.
.jpg)
.jpg)
.jpg)
.jpg)