Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah
Kairuki amesema Serikali itahakikisha huduma za mitandao na mawasiliano katika
miundombinu ya usafiri wa mwendokasi zinarejea kikamilifu kama ilivyokuwa
awali.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa utekelezaji wa maagizo ya
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, kuhusu kurejeshwa kwa huduma za usafiri
katika njia ya Kimara, Waziri Kairuki amesema wizara yake imejipanga
kuhakikisha huduma hizo zinakuwa imara na za uhakika kwa watumiaji.
Amefafanua kuwa Serikali haitakubali kuwepo kwa
ucheleweshaji au mkwamo wowote utakaoathiri ufanisi wa mfumo wa usafiri wa
mwendokasi, ambao unategemewa na maelfu ya wananchi jijini Dar es Salaam.
Katika ziara hiyo, Waziri Kairuki aliambatana na Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe, ambaye pia
amesema Serikali inafanya kazi kwa karibu kuhakikisha maboresho yanayofanyika
ndani ya mfumo wa mwendokasi yanawanufaisha moja kwa moja wananchi.