MENEJA wa Yusuph Athuman anayekipiga Napsa Stars inayoshiriki Ligi Kuu ya Zambia, Hon Simbeye amesema kama mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga ataendelea kupata nafasi ya kucheza huu unaweza kuwa msimu wake bora.
Kabla ya kutimkia Zambia msimu uliopita alisajiliwa na Yangon United inayoshiriki Ligi Kuu Myanmar kabla ya kurejea Tanzania na kumaliza mkataba wake na Fountain Gate ambako huko kote hakucheza.
Akizungumza na Mwanspoti, Simbeye amesema Athuman anaweza kurudisha kiwango chake cha zamani kama ataendelea kupewa nafasi katika kikosi hicho kilichopo nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi.
Aliongeza licha ya kukaa muda mrefu nje ya uwanja lakini ameonyesha kiwango kizuri akitoa asisti tatu kwenye mechi nane alizocheza hadi sasa.
“Nafikiri akiwa hapa anaweza kurudi kwenye kikwango chake, alikuwa nje ya uwanja kwa takribani msimu mzima lakini hadi sasa ameonyesha kiwango kizuri na kama ataendelea kucheza nafikiri atarejesha kujiamini zaidi,” amesema Simbeye na kuongeza
“Ligi ya Zambia inakua kwa sasa, naamini ushindani anaoupata hapa utamsaidia baadae kwani kiwango alichoonyesha kimefanya nianze kupata ofa kutoka Ligi ya Tanzania na Ligi daraja la kwanza Afrika Kusini.”
Hadi sasa Athuman amecheza mechi nane akitoa asisti tatu huku chama lake likiwa nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi na pointi 12, kwenye mechi 12 imeshinda mbili, sare sita na kupoteza nne.
