UHONDO wa Ligi ya Championship kwa msimu wa 2025-2026, unaendelea tena leo kwa mechi sita za raundi ya nane kupigwa na ushindani umekuwa ni mkubwa, hasa kwa timu kuanzia ya kwanza hadi ya 10, kutokana na kutopishana pointi nyingi.
Vinara wa ligi hiyo, Geita Gold inayoongoza kwa pointi 19, baada ya kuichapa Hausung mabao 3-0, ugenini, inarejea kwenye Uwanja wa Nyankumbu, mjini Geita, kuikaribisha B19 zamani Tanesco, ambayo hadi sasa haijashinda mechi yoyote msimu huu.
Geita inayosaka tiketi ya kurejea tena Ligi Kuu Bara baada ya kushuka msimu wa 2023-2024, imeshinda mechi sita na kutoka sare moja kati ya saba ilizocheza, tofauti na kwa wapinzani wao, B19, ambao hadi sasa imechapwa sita na kutoa sare mmoja tu.
Barberian iliyotoka sare ya bao 1-1, dhidi ya African Sports mechi ya mwisho, itakuwa kwenye Uwanja wa Kituo cha Ufundi cha TFF, Kigamboni, jijini Dar es Salaam kucheza na Polisi Tanzania, iliyolazimishwa pia sare ya bao 1-1 na Transit Camp.
Gunners iliyochapwa bao 1-0, ugenini na Mbuni katika mechi iliyopita, inarejea nyumbani kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma kucheza na TMA ya Arusha, iliyoshangazwa kwa kuchapwa bao 1-0, dhidi ya Stand United ‘Chama la Wana’.
Kwenye Uwanja wa Ilulu Lindi, Bigman iliyoichapa Songea United mabao 2-0, mechi ya mwisho, itabakia nyumbani kucheza na KenGold iliyoshuka daraja msimu uliopita, huku kikosi hicho kikiwa na kumbukumbu ya kufungwa mabao 2-1 na Mbeya Kwanza.
Stand United ‘Chama la Wana’, baada ya kuifunga TMA bao 1-0, ikiwa ni ushindi wa kwanza kwa kikosi hicho tangu msimu huu umeanza, itakuwa Uwanja wa CCM Kambarage Shinyanga kucheza na Mbuni ya Arusha, iliyoifunga Gunners ya Dodoma 1-0.
Stand iliyoshuka daraja msimu wa 2018-2019, ikimaliza nafasi ya 19 na pointi 44, baada ya kushinda mechi 12, sare minane na kupoteza 18, ikifunga mabao 38 na kuruhusu 50, msimu huu imeanza vibaya kutokana na changamoto kubwa hasa ya ukata.
Timu hiyo iliandamwa na ukata mapema tu baada ya kutosafiri kwenda Njombe kucheza na Hausung, katika mechi ya raundi ya nne iliyopangwa kufanyika Novemba 8, 2025, hali iliyochangia kupokwa pointi tatu na mabao matatu na Bodi ya Ligi (TPLB).
Pia, Stand ilitozwa faini ya Sh10 milioni, huku Mwenyekiti wa kikosi hicho, Stivian Antitius, akifungiwa mwaka mmoja kwa kosa la klabu hiyo kushindwa kabisa kufika uwanjani kwa kuzingatia kanuni ya 31:1 (1.1, 1.2, 1.3 & 1.4) ya Championship.
Mechi ya mwisho leo itapigwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora na wenyeji, Mbeya Kwanza iliyoifunga KenGold mabao 2-1, itaikaribisha Songea United, inayoingia ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kuchapwa 2-1, dhidi ya Bigman.
Mbeya Kwanza iliyoshuka daraja msimu wa 2021-2022, ilimaliza mkiani baada ya kikosi hicho kukusanya jumla ya pointi 25, ilianza msimu huu vibaya na kushuhudia ikichapwa mechi zake tatu mfululizo, ingawa hadi sasa imeshinda nne kati ya saba.
Ligi hiyo itaendelea tena kesho Jumanne kwa mechi mbili kupigwa saa 10:00 jioni na Kagera Sugar iliyo nafasi ya pili na pointi 19, baada ya kuifunga B19 bao 1-0, itakuwa kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba kucheza na Hausung ya Njombe.
Hausung iliyopanda daraja msimu huu, imeshinda mechi moja tu na kuchapwa sita kati ya saba ilizocheza, huku kwa upande wa Kagera inayofundishwa na nyota wa zamani wa kikosi hicho, Juma Kaseja ikishinda sita na kutoka sare mmoja hadi sasa.
Kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, African Sports ‘Wanakimanumanu’, iliyoshuka daraja msimu wa 2015-2016, kutokea Ligi Kuu Bara, baada ya mechi ya mwisho kutoka sare ya bao 1-1 na Barberian, itawakaribisha maafande wa Transit Camp.
Kocha Mkuu wa Mbeya Kwanza, Maka Mwalwisi, amesema kadri mechi zinavyoendelea ndivyo ushindani unakuwa mkubwa tofauti na mwanzo, ingawa ni mapema kuzungumzia nafasi ya kikosi hicho kwa sasa ya kurudi tena katika Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao.
“Jambo linaloongeza ushindani zaidi kwa timu zote ni kuamini zina uwezo wa kukaa kileleni kwa sababu ya gepu la pointi lililopo baina yetu kwa sasa, mbio hizi bado ni ndefu hivyo, acha tuone mwisho wake itakuwaje mbele,” amesema Mwalwisi.
