Mashujaa, Coastal patachimbika Kigoma | Mwanaspoti

WAGOSI wa Kaya iliyotoka kuopata ushindi wa mabzo 2-0 nyumbani, imesafiri hadi Kigoma tayari kwa pambano la Ligi Kuu Bara dhidi ya wenyeji wao, Mashujaa huku namba zikiwabeba.

Pambano hilo pekee la Ligi Kuu kwa leo litapigwa Uwanja wa Lake Tanganyika, mjini humo kuanzia Saa 10:00 jioni,  huku wenyeji wakiwa na kumbukumbu ya kulazimishwa suluhu na Dodoma Jiji katika mechi iliyopita uwanjani hapo.

Hili ni pambano la tano kwa timu hizo kukutana katika Ligi tangu Mashujaa ilipopanda daraja, huku rekodi zikionyesha, wenyewe wamekuwa wanyonge mbele ya Wagosi wa Kaya  Lake Tanganyika.

Katika mechi mbili zilizopigwa uwanjani hapo, ikiwamo ya msimu uliopita Mashujaa haijawahi kutoka na ushindi mbele ya mabingwa hao wa zamani wa Ligi  Kuu Bara.

Mara ya kwanza kukutana uwanjani hapo ni Aprili 12, mwaka jana, mechi ya  duru la pili la ligi ya msimu wa 2023-2024 na wenyeji walicharazwa mabao 2-1 ikishindwa kulipa kisasi cha kukandwa pia mabao 2-0 katika mechi ya duru la kwanza iliyochezwa Oktoba 25, 2023.

Mechi ya msimu uliopita kwenye uwanja huo iliyopigwa Februari 11 mwaka huu, timu hizo zilitoka suluhu baada ya mechi ya duru la kwanza Coastal Union kukubali kipigo cha bao 1-0.

KIGO 01

Rekodi zinaonyesha katika msimu huu wa 2025-2026, Mashujaa imecheza mechi tano nyumbani na  haijapoteza yoyote, imetoka sare mbili na kushinda tatu, huku Wagosi ikicheza mbili tu za ugenini na haijatoka na ushindi wowote hadi sasa.

Coastal iliyocheza mechi sita hadi sasa tofauti na Mashujaa inayoshuka uwanjani leo kwa mara ya tisa, katika mechi hizo mbili za ugenini imepoteza moja mbele ya Dodoma Jiji na suluhu na Mtibwa Sugar.

Mashujaa inayonolewa na kocha Salum Mayanga itaendelea kuwategemea nyota kama Baraka Mtuwi, Salum Kihimbwa, David Olomi, Ismail Mgunda, Mundhir Vuai na Jaffar Kibaya ili kusaka pointi tatu zitakazoifanya ifikishe pointi 15 kama ilizonazo Pamba Jiji iliyokuwa kileleni (kabla ya mechi za jana).

Mashujaa ina pointi 12 ikishika nafasi ya tatu, huku Coastal Union imevuna pointi nane katika mechi sita na ilikuwa nafasi ya tisa (hii kabla ya mechi za jana).

KIGO 02

Hata hivyo, wenyeji watakuwa na kibarua kizito mbele ya Wagosi wanaonolewa na Mohammed Muya iliyotoka kushinda nyumbani kwa mabao 2-0 yote yakifungwa na Mabad Maulid ambaye ataongoza safu ya ushambuliaji ya mabingwa hao wa Bara wa msimu wa 1988.

Mbali na Maabad, Coastal pia ina nyota wengine kama Bakar Msimu, Cleophas Mkandala, Ally Msengi, Athuman Masumbuko ‘Makambo JR’ mwenye mabao mawili pia na Meshack Abraham ili kuibana Mashujaa katika mechi hiyo na kama itashinda itafikisha pointi 11.

Makocha wa timu hizo, wametambiana mapema kwamba dakika 90 zitaamua kwani kila moja ameliandaa jeshi lake vizuri kwa ajili ya pambano hilo linalosubiriwa kwa hamu na mashabiki.