Pantev ataja mambo matatu vipigo mfululizo CAF

MENEJA Mkuu wa Simba, Dimitar Pantev, ametoa kauli iliyoashiria kuumizwa na matokeo ya kupoteza mechi mbili za kwanza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku akitaja mambo matatu yaliyochangia hilo.

Simba imeanza hatua hiyo ya makundi kwa kufungwa nyumbani bao 1-0 dhidi ya Petro Atletico, kisha imechapwa 2-1 na Stade Malien ugenini. Matokeo hayo yameifanya kuburuza mkia bila ya pointi katika Kundi D linaloongozwa na Petreo Atletico na Stade Malieni zenye pointi nne kila moja, huku Espérance de Tunis ina mbili.

Katika vitu ambavyo Pantev amevitaja, kwanza kuna mchakato wa kubadili vitu ndani ya kikosi unaohitaji muda, pili walifanya mazoezi muda mrefu na kundi dogo la wachezaji kutokana na uwepo wa Kalenda ya FIFA wiki chache kabla ya kuanza hatua ya makundi, na tatu wachezaji wa Simba walicheza chini ya kiwango.

Akizungumza muda mchache baada ya jana Jumapili Novemba 30, 2025 kufungwa 2-1 na Stade Malien mechi ikichezwa nchini Mali, Pantev amesema: “Sio rahisi kuzungumza baada ya mechi kama hii. Sitafuti kujitetea. Najua kila mchezaji amejitahidi. Labda haukuwa mchezo wetu. Haikuwa siku yetu.

Pantev raia wa Bulgaria aliyetua Simba Oktoba 6, 2025, siku chache baada ya klabu hiyo kuachana na Msauzi, Fadlu Davids aliyetimkia Raja Casablanca ya Morocco, ameendelea kwa kusema: “Hata hivyo tangu nimefika hapa nimekuwa nikieleza kuwa kuna mchakato.

“Naamini katika mchakato huu, naamini hata watu wengine wanaoiendesha hii klabu wanaamini kwenye mchakato huu kwa sababu walinileta hapa kujaribu kubadilisha kitu kwenye timu. Miezi miwili haitoshi, lakini timu kama Simba hakuna muda siku sita, kumi au karibia 15.”

Pantev amebainisha kwamba, katika maandalizi kuelekea mechi hizo mbili za kwanza hatua ya makundi, kikosi kilifanya mazoezi muda mwingi kikiwa na wachezaji wachache kutokana na uwepo wa Kalenda ya FIFA, hivyo hilo kwa kiasi fulani limechangia matokeo mabaya lakini anaamini watarudi wakiwa imara zaidi.

“Tumefanya mazoezi bila wachezaji waliokuwepo timu ya taifa. Wamekuja muda mfupi. Najua kila mtu amechukia hususani mashabiki. Nawaelewa kwa sababu wana matarajio makubwa. Natumaini kila mchezaji na viongozi tutafanya bidii na kuja na kiwango bora kwa siku zijazo.

“Unajua tatizo hili si la sasa. Ni la muda mrefu. Hata kwenye mechi zilizopita za CAF hatukufunga. Na nilipofika haijawa rahisi kufunga. Kama hufungi huwezi kukusanya alama.”

Mwisho Pantev amewaangushia zigo wachezaji akisema kikosi cha Simba kina ubora kushinda wapinzani wao, lakini walicheza chini ya kiwango.

“Tatizo kubwa wachezaji wetu wengi wamecheza chini ya kiwango chao. Timu yetu ina ubora mkubwa kuliko timu ya wenzetu. Nimechukia kwa sababu tumeshindwa kufunga. Lakini ndio mpira,” amesema Pantev.

Simba baada ya kumalizana na Stade Malien, kati ya Januari 23 na 25, 2025 itakuwa Tunisia kukabiliana na Esperance, kisha zitarudiana jijini Dar kati ya Januari 30 na Februari 1, 2026.

Baada ya hapo, Simba itakwenda Angola kucheza dhidi ya Petro Atletico kati ya Februari 6 na 8, 2026, itamalizia hatua ya makundi nyumbani dhidi ya Stade Malien kati ya Februari 13 na 15, 2026.

Kwa sasa, Simba inapambana kurudi kwa nguvu na kufuzu robo fainali ili kutotibua rekodi yake katika mashindano ya CAF kwani tangu msimu wa 2018-2019, imefuzu makundi mara saba. Katika mara sita ilizowahi kucheza makundi kabla ya msimu huu, zote imefanikiwa kuvuka na kucheza robo fainali.