KIKOSI cha Yanga kimetua salama nchini jana kutoka Algeria kilipoenda kucheza mechi ya pili ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kutoka suluhu dhidi ya JS Kabylie, huku kocha wa kikosi hicho, Pedro Goncalves akiweka bayana mechi ilikuwa ngumu, ila sare ya ugenini imewabeba.
Yanga iliumana na JS Kabylie Ijumaa iliyopita na kutoka sare hiyo isiyo na mabao iliyoifanya ifikishe pointi nne na kulingana na Al Ahly ya Misri iliyolazimisha sare ya 1-1 ugenini dhidi ya AS Far Rabat ya Morocco iliyofungwa awali bao 1-0 na Yanga zilipoumana visiwani Zanzibar.
Akizungumza mara baada ya kikosi kuwasili mchana wa jana, kocha Pedro alisema haikuwa kazi rahisi kuambulia pointi moja ugenini na kuwapongeza wachezaji kwa jinsi walivyojituma kwa bidii kubwa mbele ya wenyeji ambao walikuwa wametoka kupoteza kwa 4-1 mechi ya kwanza dhidi ya Al Ahly.
“Ilikuwa mechi ngumu na yenye ushindani ila wachezaji walijitoa na ninawapongeza kwa kuweza angalau kupata pointi moja muhimu tukiwa ugenini,” alisema Pedro na kuongeza: “Tunarudi kujipanga kwa mechi za Ligi Kuu kabla ya kucheza tena mechi za CAF dhidi ya Al Ahly.”
Pedro aliyeiwezesha Yanga kufuta unyonge wa kushindwa kushinda katika mechi mbili za kwanza makundi kwa miaka 10 na kuiweka timu hiyo pazuri katika Kundi B linalotajwa kuwa mgumu kwa msimu huu ikiwa haijaruhusu bao lolote.
Msimu uliopita, Yanga ikiwa chini ya kocha Sead Ramovic ilianza na vipigo katika mechi mbili za kwanza za Kundi A ikilala zote kwa mabao 2-0 kutoka kwa Al Hilal ya Sudan na pia dhidi ya MC Alger ya Algeria, wakati msimu wa 2023-2024 ikiwa na Miguel Gamondi ilianza kwa kichapo cha 3-0 mbele ya CR Belouizdad ya Algeria na kutoka sare ya 1-1 na Medeama ya Ghana.
Yanga itavaana na Al Ahly katika mechi mbili mfululizo mapema mwakani ambazo zitatoa dira kwa timu hiyo katika safari ya kusaka tiketi ya robo fainali baada ya msimu uliopita kukwama kwa kumaliza kundini ikiwa na pointi nane nyuma ya Al Hilal na MC Alger.
Kabla ya mechi hizo za CAF, Yanga itacheza mechi mbili za Ligi Kuu ikiwa ni viporo ikiwamo ile ya Desemba 7 dhidi ya Coastal Union ambayo bado haijajulikana itachezwa kwenye uwanja gani kutokana na Mkwakwani kufungiwa na Shirikisho la Soka (TFF) kwa kukosa vigezo vya kutumika kwa mechi za Ligi Kuu.
