Azam FC, Singida Black Stars kuliamsha upya Ligi Kuu

BAADA ya kumaliza majukumu ya mechi za kimataifa, wawakilishi wanaoshiriki hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, Azam FC na Singida Black Stars kesho watarudi katika Ligi Kuu kuanza kusaka pointi za kuwaweka pazuri.

Azam ambayo imepoteza mechi mbili mfululizo za Kundi B mbele ya As Maniema ya DR Congo na Wydad Casablanca ya Morocco, itakuwa mwenyeji wa mechi ya nne kwa timu hiyo katika Ligi Kuu ya msimu huu dhidi ya Singida Black Stars iliyoambulia pointi moja katika mechi za Kundi C la Shirikisho Afrika.

Singida ilitoka suluhu juzi usiku kwenye Uwanja wa New Amaan, visiwani Unguja mbele ya Stellenbosch ya Afrika Kusini baada ya awali kupoteza 2-0 ugenini Algeria mikononi mwa CR Belouizdad. Baada ya mechi tatu za kwanza za Ligi Kuu Bara, Singida ina pointi 7, ikishinda mbili na sare moja na sasa kesho itakuwa Azam Complex.

AZA 01

Hilo litakuwa pambano la tisa kwa timu hizo kukutana katika Ligi Kuu tangu 2020 Singida ikifahamika kama Ihefu kabla ya msimu uliopita kubadilisha jina kuwa Singida BS, huku rekodi zikionyesha timu hiyo imeshinda mara mbili tu mbele ya Azam ikiwamo mechi ya mwisho la msimu uliopita.

Katika mechi nyingine sita kati ya timu hiyo, Azam imeibuka mbabe na hakuna pambano lolote lililowahi kuisha kwa sare, hali inayoonyesha kuwa hata pambano la kesho yeyote atakayekaa kizembe ataumia mbele ya mpinzani kutokana na aina ya vikosi na makocha walionao.

AZA 03

Singida ipo chini ya kocha Miguel Gamondi ilihali Azam ina Florent Ibenge, ambaye ni mgeni wa Ligi Kuu kulinganisha na mwenzake aliyewahi kuinoa Yanga misimu miwili iliyopita na kutwaa nayo mataji kadhaa kabla ya kusitishiwa mkataba mwaishoni mwa mwaka jana.

Rekodi zinaonyesha katika mechi nne zilizopita kwenye Uwanja wa Azam, Singida (zamani Ihefu) haijawahi kuonja ushindi wowote, kwani mechi mbili ilizoshinda ilikuwa kwao na nyingine kama hizo ilipoteza kwa Wanalambalamba wanaojivunia kiungo mshambuliaji, Feisal Salum ‘Fei Toto’.

AZA 02

Mapema mara baada ya pambano la Wydad lililopigwa Zanzibar, kocha Ibenge alikiri kikosi hicho kwa sasa kimeimarika na wachezaji wanapambana uwanjani, licha ya kutopata matokeo mazuri ambayo yamemuumiza, lakini anajipanga kwa mechi hizo za Ligi ili kuwa vizuri zaidi.

AZA 04

Gamondi aliyeiwezesha Singida kutwaa ubingwa wa Kombe la Kagame 2025 na kuiingiza hatua ya makundi ya michuano ya CAF kama alivyofanya Ibenge kwa Azam, amekuwa akisisitiza kwamba malengo ya klabu hiyo kwa msimu huu mbali na kufanya vyema michuano ya kimataifa, pia kufunika katika Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho (FA).

“Tuna kikosi bora na chenye wachezaji wazoefu wanaoweza kukupata matokeo mazuri, kila mechi mbele yetu iwe ya Ligi Kuu au kimataifa ni muhimu kwetu na tutakabiliana na mpinzani jinsi alivyo kwa sababu tuna malengo makubwa kote,”  Gamondi.