Bukoba. Diwani wa kata ya Kagondo katika Manispaa ya Bukoba Mkoa Kagera, Acton Rwankomezi ameapishwa kuwa diwani na kuchaguliwa na baraza la madiwani kuwa Mstahiki Meya.
Baraza la madiwani la manispaa hiyo linaundwa na madiwani 20 wakiwemo na wale wa viti maalumu kwenye kata 14.
Rwankomezi ni diwani pekee kijana mwenye umri wa miaka 27 na amekuwa Mstahiki Meya wa kwanza kuchaguliwa katika umri mdogo katika mabaraza yote yaliyopita kuanzia mwaka 1961, kwenye manispaa hiyo ya Bukoba.
Baadhi ya Madiwani katika manispaa ya Bukoba Mkoa Kagera.
Akizungumza baada ya kuchaguliwa leo Jumanne, Desemba 02,2025 Diwani wa kata ya Kagondo, Rwankomezi amesisitiza watumishi wa umma wote wakiwemo madiwani na wakuu wa idara kutenda haki, ili wananchi kupata huduma stahiki.
“Nasisitiza na kumekuwepo tabia ya baadhi ya watumishi wa umma katika manispaa hii kutuhumiwa na wananchi kuchelewesha huduma hivyo naomba tushirikiane tufanye kazi ya kuwahudumia wananchi,”amesema.
Amesema hategemei kutumia umri wake mdogo na ujana wake kuharibu miradi iliyoanzishwa na inayotegemea kuanzishwa ishindwe kutekelezeka katika manispaa hiyo.
Aidha, ameongeza kuwa anaomba pia viongozi wenzake hasa watumishi ambao ni wakuu wa idara mbalimbali wa manispaa kuwapa kipaumbele vijana na kinamama kwenye mikopo ya asilimia 10, ili waweze kuinua uchumi wa manispaa na nchi kwa ujumla.
Awali Mwenyekiti wa uchaguzi huo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Bukoba, Proscovia Mwambi alimtangaza Rwankomezi kuwa Meya na Waajabu Galiatano kuwa Naibu Meya.
Mbunge wa jimbo la Bukoba mjini akisisitiza Amani kwa wananchi na kuomba watumishi wa Umma kuwasikiliza na kutatua migogoro kwenye jamii.
Rwankomezi na Galiatano walikuwa wagombea pekee kwenye uchaguzi huo na wamepigiwa kura za ndiyo 20 kutoka kwa wajumbe ambao ni madiwani wa halmashauri ya manispaa hiyo.
Kwa upande wa Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, Jonhstoni Mtasingwa ameomba kila diwani aliyechaguliwa na wananchi na kuapishwa, kuhakikisha anakuwa kichocheo cha kutatua migogoro kwenye jamii na kuongeza chachu ya mafanikio ya wananchi kwa kusimamia miradi ya maendeleo katika kata yake.
