Kuzaa tunaweza, tunashindwaje kusomesha? | Mwananchi

Dar es Salaam. Watanzania tuna msemo mmoja maarufu: “Kuzaa si kazi, kazi ni kulea.” Lakini leo hii msemo huu unaonekana kugeuzwa mzaha.

Tunaona watu wengi wakijitosa kwenye starehe ya tendo la ndoa bila kujiuliza matokeo yake. Wengine wanazaa watoto kana kwamba ni jambo la kawaida, lakini hawana maandalizi ya kisaikolojia, kifedha wala kiakili ya kuwalea.

Matokeo yake ni kizazi kinachokua bila malezi, watoto wanaojilea wenyewe, na jamii inayokumbwa na matatizo makubwa ya nidhamu na ukosefu wa maarifa.

Swali  linabaki kama kuzaa tunaweza, tunashindwaje mengine muhimu kama kulea, kusimamia elimu, na kuhakikisha watoto wanakuwa raia wema?

Leo hii ukiingia shuleni, mwalimu ndiye anayeonekana kubeba mzigo mzima wa malezi ya watoto. Wazazi wengi wamejitenga kana kwamba kazi yao ni kuhakikisha mtoto anazaliwa, basi imekwisha.

 Walimu wanakabiliana na watoto wasio na nidhamu, wasioweza kutii, na wasiokuwa na msingi wa heshima. Si ajabu kusikia walimu wakilalamika kuwa shule zimegeuka sehemu za kufundisha masomo na kulea kwa wakati mmoja.

Jumatatu asubuhi unakutana na mwanafunzi mwenye sare chafu, viatu vimeoza, na hana hata madaftari ya kutosha. Swali la kwanza linaibuka: huyu anatoka katika familia kweli?

Yuko nyumbani, lakini je, kuna mzazi anayemfuatilia? Au ameachwa kama ndege aliyeachiwa mabawa yake ajitafutie? Mwanafunzi kama huyu anapoingia darasani tayari ameshabeba mzigo wa huzuni na kushindwa. Ni vigumu kutarajia kama atazingatia masomo.

Uhalisia ni kwamba watoto wengi leo hawana msaada wa malezi. Wengi wanalelewa mitaani kuliko majumbani. Wanajifunza maadili mitaani, kupitia makundi ya marafiki, mitandao ya kijamii, na vichochoroni. Wazazi ambao walipaswa kuwa walinzi wa kwanza wa maadili na dira, wamelala usingizi wa ajabu.

Matokeo ya hali hii yanaonekana wazi. Kwanza, nidhamu shuleni imeporomoka. Kuna ongezeko kubwa la watoto wanaowajibu vibaya walimu, kupigana shuleni, na hata kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya.

Hii yote ni kwa sababu msingi wa malezi haupo. Pili, ufaulu shuleni unaporomoka kwa kasi. Mtoto anayekosa uangalizi wa karibu nyumbani, asiyesimamiwa kufanya kazi za shuleni, hawezi kushindana na wenzake.

Tunaposhuhudia wimbi la watoto  kuacha masomo au kufeli mitihani ya kitaifa, si walimu pekee wanaopaswa kulaumiwa, bali wazazi ambao walishindwa kuwajibika.

Jamii yetu inakumbwa na mtazamo potofu kwamba jukumu la malezi ni la shule pekee. Wazazi wengi wanaamini alimradi mtoto anaenda shuleni, basi ameshalelewa.

Hili ni kosa kubwa. Malezi makuu ya mtoto yanapaswa kuanzia nyumbani. Shule inakuja tu kukamilisha jukumu la kitaifa la elimu, lakini haibadili nafasi ya mzazi.

Watoto wanapokua bila malezi ya nyumbani, wanakua bila dira. Wanakosa heshima, wanakosa msimamo, na wanajikuta wakikumbatia maadili mabaya.

 Ndiyo maana leo tunaona vijana wengi wakiwa na hasira zisizo na sababu katika jamii, wakijihusisha na uhalifu, au wakikimbilia njia za mkato kupata maisha bora. Hii siyo kasoro ya walimu, bali ni udhaifu wa wazazi na jamii kwa ujumla.

Lakini je, tukiwa wazazi tunaweza kufanya nini? Hatua ya kwanza ni kubadili mtazamo. Kuzaa mtoto si mwisho wa safari, bali ni mwanzo wa jukumu zito. Wazazi wanapaswa kufahamu kwamba malezi ni kazi ya kila siku.

Inahitaji muda, kujitoa, na pia nidhamu ya mzazi mwenyewe. Mtoto hufuata zaidi mfano wa mzazi kuliko maneno yake.

Hatua ya pili ni kusimamia masuala ya elimu kwa makini. Wazazi wanapaswa kuhakikisha watoto wao wanaenda shuleni wakiwa na mahitaji yote ya msingi kama chakula, sare safi, na vifaa vya kusomea.

Si lazima uwe tajiri ili kumhudumia mtoto wako; kinachohitajika ni dhamira ya kweli na kupanga vipaumbele.

Hatua ya tatu ni kushirikiana kwa karibu na walimu. Ni kosa kubwa kwa mzazi kutojua hata jina la mwalimu wa darasa la mtoto wake, au kutofika shuleni kabisa kujua maendeleo ya mtoto.

Hali hii inafanya mtoto kujiona yuko huru, asiye na mtu anayemfuatilia. Ushirikiano mzuri kati ya wazazi na walimu unaweza kusaidia kumjenga mtoto vizuri zaidi.

Tukizingatia haya, matokeo yake ni makubwa kwa taifa. Kwanza, ufaulu shuleni utaongezeka. Mtoto anayesimamiwa nyumbani ni rahisi kufaulu kwa sababu anakuwa na nidhamu ya kujisomea na kusikiliza walimu.

Pili, nidhamu kwa ujumla itaimarika. Watoto watakua na heshima kwa walimu na kwa jamii. Hatimaye, tutakuwa na taifa lenye nguvu kazi bora, watu waliokomaa kiakili, kimaadili na kielimu.

Swali la msingi linabaki: kwa nini tuwe hodari kwenye starehe ya kuzaa, lakini tushindwe kulea? Kama jamii, tunapaswa kujitazama upya. Hatupaswi kuendelea kulea kizazi kinachojilea chenyewe.

Tusipoamka sasa, kesho tutakumbwa na wimbi la vijana wasio na nidhamu, wasio na elimu bora, na wasioweza kuchangia katika maendeleo ya taifa.  Kizazi cha kuharibu mali za umma au wananchi kwa sababu ya hasira binafsi.

Watoto ni urithi na rasilimali kubwa zaidi ya taifa lolote. Tukiwalea vizuri, tutakuwa na taifa imara lenye watu bora. Tukiwatelekeza, tutakuwa na taifa dhaifu, linaloelemewa na matatizo.

Kuzaa tunaweza, ndiyo. Lakini hebu tuoneshe pia tunaweza kulea, kuelimisha, na kusimamia kizazi chetu. Hapo ndipo tutaweza kusema kweli tunalijenga Taifa letu.