Mabosi Simba wamuweka mtu kati Mpanzu

SIMBA inarejea nchini leo Jumanne ikitokea Mali ilikopoteza mechi ya pili ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufungwa mabao 2-1 na Stade Malien, ambapo kama ilivyo kwa mashabiki kuwashtukia wachezaji kupoteza viwango, ndivyo ilivyo kwa mabosi wa klabu hiyo walioamua kuwakalisha kitimoto baadhi ya nyota wa timu hiyo wakianza na winga Ellie Mpanzu.

Wekundu wa Msimbazi waliopo Kundi D la michuano hiyo walianza kwa kunyukwa bao 1-0 nyumbani wiki iliyopita kabla ya juzi usiku kupasuka tena mjini Bamako, Mali na kuzidi kuwakata stimu viongozi, mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo hasa kutokana na baadhi ya wachezaji kuonekana kucheza kichovu na kukosa umakini uwanjani kitu kilichowashtua wengi.

Mabosi wa Simba, ukiacha kocha Dimitar Pantev ambaye bado hawajamuelewa sawasawa, wameshtuka kuwa, kuna tatizo lipo kwa wachezaji ambao ni kama wamepoteza utulivu wakikosa sana nafasi.

MPA 01

Kushtukia hilo tu mabosi wa Simba wameanza vikao vizito na mastaa wa timu hiyo akitangulia winga Mkongomani Ellie Mpanzu ambaye walishakaa naye siku moja kabla ya mechi hiyo dhidi ya Malien na matunda yalionekana licha ya timu kupoteza kwa mabao 2-1.

Bosi mmoja wa Simba aliliambia Mwanaspoti kuwa katika kikao hicho, Mpanzu amefunguka mengi kisha pande hizo mbili kumtuliza wakimtaka kuanza upya, akiongeza: “Kama ulifuatilia kwa makini, winga huyo alionekana amebadilika licha ya timu hiyo kupoteza.

MPA 02

“Unajua weka mbali tatizo la kocha wetu, kuna nyakati lazima tuwaangalie na hawa wachezaji wetu wanavyochangia mambo kuwa magumu katika timu, matokeo ambayo tunayapata si kama hatutengenezi nafasi.”

Bosi huyo wa ndani ya bodi ya Simba aliongeza; “Tulianza na Mpanzu, kuna mambo tumemwambia naye amekiri kwamba ameshuka kidogo, yapo mambo ambayo hatuwezi kuyaweka wazi, lakini tutayafanyia kazi huku ndani na alichoahidi ni kwamba baada ya kikao hicho ataaanza kupambana zaidi.”

MPA 03

Mbali na Mpanzu, baada ya mechi hiyo ya Bamako, mabosi hao wakajifungia na mshambuliaji Jonathan Sowah huku naye akieleza namna alivyokutana na wakati mgumu tangu atue ndani ya kikosi hicho akitokea Singida Black Stars.

“Tumeongea pia na Sowah, naye alikuwa na yake yanayomsumbua tumemshusha presha na kumwambia atulize akili acheze kila atakapopewa nafasi na makocha, tutawafikia taratibu ili tutafute tiba ya mkwamo ambao umetuganda mpaka sasa,” amesema kigogo huyo na kuongeza wanaendelea na vikao kwa mastaa hao wakimlenga kwa sasa Jean Charles Ahoua.

MPA 04

“Tunafanya hivi kwa lengo la kurejesha makali ya timu, kwani wachezaji wote hawa wana ubora wa hali ya juu na uwezo wa kuibeba timu, lakini kwa siku za hivi karibuni wanaonekana wa kawaida, ndio maana tumeshtuka na kuzungumza nao,” amesema.

Simba kwa sasa inajiandaa kwa mechi za mwakani dhidi ya Al Ahly ya Misri itakayocheza nayo ugenini na nyumbani kisha kumalizia mbili za mwisho za kundi hilo kwa kuifuata Petro Atletico na kuikaribisha Malien watakayofunga nayo hesabu na kuamua hatma ya robo fainali.