Machifu Mbeya wataka watekaji washughulikiwe

Mbeya. Viongozi wa kimila mkoani Mbeya, machifu, wamelaani vurugu zilizotokea Oktoba 29, huku wakiiomba Serikali kuwachukulia hatua watekaji na kusikiliza kilio cha vijana.

Wakati huohuo, umoja wa waendesha bajaji jijini humo umetangaza msimamo wao kuhusu taarifa zinazosambaa mitandaoni kuhusiana na Desemba 9 mwaka huu.

Oktoba 29 mwaka huu, baadhi ya Watanzania walishiriki Uchaguzi Mkuu wa kuwachagua madiwani, wabunge na rais.

Hata hivyo, siku hiyo iligubikwa na maandamano yaliyochochea vurugu zilizopelekea uharibifu wa mali za umma na binafsi, pamoja na kupoteza maisha ya watu.

Wakizungumza leo Desemba 2,2025  jijini Mbeya, viongozi hao wamesema wanalaani na kukemea matukio ya vurugu yaliyotokea Oktoba 29, ambayo yalisababisha kusimama kwa shughuli za kiuchumi.

Pia, wamewataka wale waliohusika kuhamasisha machafuko hayo kuhakikisha vitendo hivyo havijirudii.

Katibu wa Machifu wa Kingdom ya Lyoto, Michael Yilanga, amesema kuwa kama mmoja wa waathirika waliopoteza wajukuu wawili katika vurugu hizo, hakubaliani na matukio ya aina hiyo.

Ametoa wito kwa Serikali kusikiliza na kushughulikia kilio cha vijana ili kuzuia kurudiwa kwa hali kama hiyo.

Amebainisha kuwa uwepo wa maandamano unachangia kudhoofisha uchumi, akitolea mfano tukio la Oktoba 29 ambalo lilisababisha kusimama kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Yilanga amesema kuwa yeye kama mwalimu hakuweza kwenda kazini kwa siku tano kutokana na athari za vurugu hizo, na kuwasihi vijana kuwa wavumilivu.

 “Hiki kilichotokea kiwe funzo, kila mmoja aliathirika kwa nafasi yake, tungeomba kutembea kila kata tutoe elimu, niiombe Serikali isiwapuuze vijana, hao wanaotekwa bila kujulikana ndio sababu, mamlaka ziwashughulikie ili tuondoe haya yote,” amesema Yilanga.

Ameongeza kuwa zipo athari za vurugu akibainisha kuwa kama ingefanyika majadiliano huenda isingefika hatua hiyo, akifafanua kuwa kati ya wajukuu zake waliopigwa Ilolo na Uyole mmoja hajaonekana.

“Yule aliyepigwa Ilolo tulizika, ila wa Uyole hadi leo hajaonekana, vijana wasirudie hii hali, kuna umuhimu wa kujadiliana, kuna ndugu zetu wanatekwa sasa wanapokwenda hawajulikani, hili ndio inawapa vijana hali hiyo.”

Naye Chifu wa Mkoa huo, Rocket Mwashinga (80) amesema kilichotokea Oktoba 29 ilikuwa ni mshangao, ajabu na aibu kwa Tanzania kwa kuwa katika historia hakijawahi kutokea akieleza kuwa wanaomba lisijirudie.

“Tuliona Serikali ilivyopambana kudhibiti vurugu hizo na tunaomba kuwapo utulivu kwa kuwa Tanzania ndio nchi pekee kimbilio la wengine kwa amani iliyopo, kwa umoja wetu tunakemea tukio hilo.

“Tunawaomba vijana wenye dukuduku wawasilishe kilio chao kwa mamlaka kwa kuwa tayari Rais Samia Suluhu Hassan ameteua wizara maalumu kushughulikia maendeleo yao, wakitaka maandamano wabebe mabango na siyo silaha za jadi,” amesema Chifu Mwashinga.

Naye Mwenyekiti wa Bajaji jijini Mbeya, Lucas Mwakyusa amesema yanayosambazwa mitandaoni kuhusu uwapo wa vurugu Desemba 9, vijana wanapaswa kuyapuuza na kuendelea na shughuli zao za kujiingizia kipato.

“Sisi kama umoja wa waendeshaji na wamiliki wa bajaji hatujapewa maelekezo na vyombo vya usalama kwamba tusifanye kazi kwa tarehe yoyote, kwa maana hiyo tunahamasisha amani, utulivu na mshikamano.”

“Tanzania ni yetu, tusifuate mkumbo wa namna yoyote na hayo yanayoendelea kwenye mitandao tuyapuuze, tusiongozwe na mihemko, amani ikitoweka sisi ndio tunaathirika,” amesema Mwakyusa.

Mmoja wa waendesha bajaji jijini humo, Mussa Mwalyosi amesema yaliyotokea Oktoba 29 yawe sehemu ya funzo kwa vijana na wananchi kwa ujumla kwakuwa shughuli zote zilisimama.

“Tusikubali kugawanywa kwa masuala ya itikadi za vyama wala dini, tuhamasishane kulinda amani ya nchi, tukumbuke Oktoba 29 kilichotokea hali ilikuaje kwa kuwa wengi tunategemea kutoka ndio tupate riziki” amesema Mwalyosi.