Dodoma. Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma imeridhia kuendelea kwa shauri la kupinga kufutwa kwa sherehe za Muungano lililofunguliwa na Wakili Peter Madeleka dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Jaji wa Mahakama Kuu Juliana Masabo, leo Desemba 2, 2025 ameagiza upande wa Serikali kupeleka kiapo kinzani mahakamani ifikapo Desemba 5, 2025 na kwamba shauri hilo litasikilizwa Desemba 8, 2025 saa nane mchana.
Mahakama imekubali hoja ya Wakili Madeleka kwamba Rais anaweza kushitakiwa bila kupewa taarifa kwenye kesi hiyo na Jaji akasisitiza kuwa shauri hilo mbali na kuwa katika hati ya dharura, pia litazingatia uharaka wake.
Awali, wakili wa Serikali Yohana Marco aliiomba mahakama itoe siku saba kuanzia leo ili Serikali ipeleke kiapo kinzani, siku ambayo ingeangukia Desemba 9, 2025, jambo ambalo limepingwa vikali na Wakili Madeleka akisema kama Mahakama ingezingatia ombi hilo basi ingekuwa imepoka haki yake, kwani siku hiyo inaangukia kwenye siku inayobishaniwa.
“Mheshimiwa Jaji, nakataa ombi hilo na ningeomba Mahakama yako itazame kuwa, kama ombi la Wakili wa Serikali litakubaliwa basi ile haki yangu inayotafutwa itakuwa imepotea, kwani siku saba zinaangukia tarehe tisa ambayo ndiyo inabishaniwa, naomba umwagize Wakili wa Serikali ndani ya saa 24 awe ameleta kiapo kinzani,” amesema Madeleka.
Hoja ya Madeleka ilianzia kwenye kauli ya Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba ya Novemba 24, 2025 kuwa, Rais amefuta shehere za sherehe za Uhuru wa Tanganyika na badala yake fedha zilizopangwa kugharamia shehere hizo, zinakwenda kujenga miundombinu ya Serikali ambayo iliharibiwa kwenye maandamano ya Oktoba 29, 2025.
Madeleka Novemba 26, 2025 alifungua shauri la maombi ya ruhusa ya mahakama kufungua shauri la mapitio ya mahakama kupinga uamuzi huo na shauri hilo lilipangwa kusikilizwa upande mmoja na Mahakama mbele ya Jaji Juliana Masabo.
Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali baada ya kupata taarifa hizo ulifika mahakamani na kupinga shauri hilo kusikilizwa upande mmoja, ukaomba shauri liahirishwe mpaka wao watakapopewa nakala ya nyaraka husika.
Katika hati ya maombi ya shauri hilo aliyoiwasilisha mahakamani, Madeleka anaomba ruhusa ya mahakama hiyo ya kufungua shauri la kupinga uamuzi huo kwa utaratibu wa mapitio ya mahakama, kuomba amri tatu ikiwemo ya kufuata uamuzi wa Rais wa kufuta shehere za Uhuru, kwani haukuwa halali wala wa maana, amri ya kumlazimisha Rais kutekeleza wajibu wake na amri ya zuio dhidi yake.
Katika kiapo chake, Madeleka anasema yeye ni raia wa Tanzania na mkazi wa Jiji la Dar es Salaam, hivyo anayo haki ya kusherehekea sherehe hizo chini ya utaratibu wa Serikali kwa mujibu wa sheria na kwamba sherehe zisipofanyika, haki zake zitaguswa kwani yeye ni mnufaika.
