Kulia ni Mkurugenzi wa halmashauri ya Biharamulo, Innocent Mukandala na Kushoto ni Mwenyekiti Apolinary Mugarula.
Mkuu wa wilaya ya Biharamulo,Sacp Advera Bulimba
Mbunge wa Jimbo la Biharamulo,Mhandisi Ezra Chiwelesa.
…………
BIHARAMULO
ZAIDI ya Shilingi milioni 111,671,167.98 zimetolewa na halmashauri ya wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera kwaajili ya vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu likiwa ni takwa la serikali kwa kila halmashauri nchini.
Hayo yamo kwenye taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya halmashauri hiyo kuanzia Julai hadi November 2025/26 baada ya Baraza la Madiwani kuvunjwa rasmi ili kupisha uchanguzi mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani nchini.
Katika ripoti hiyo ya Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo kwenye kikao cha kwanza cha Baraza la Madiwani hao, Innocent Mukandala, amesema katika kipindi cha mwezi Julai hadi Novemba halmashauri imetekeleza miradi mbalimbali ikiwemo utoaji wa fedha kwa makundi maalumu.
Hatua hiyo ni njia moja ya kuondoa umaskini wa vipato kwa jamii na kwamba walionufaika na pesa hizo wanapaswa kutambua kuwa ni mkopo usio na riba na kwamba wanapaswa kuzalisha na kurejesha fedha hizo kwa kadri ya mikataba yao.
Utekelezaji huo unaenda sambamba na ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha makundi ya wanawake, Vijana na wenye ulemavu wananufaika na mikopo ya aslimia 10 zinazotolewa na halmashauri nchini kote.
Mbali na hilo pia takribani milioni 130 zimepokelewa na kwaajili ya ujenzi wa Bweni kwenye shule ya Sekondari Biharamulo ambapo ujenzi wake umefikia hatua ya upauaji.
Kadhalika mkuu wa wilaya hiyo, Sacp, Advera Bulimba, amewataka Madiwani waliokula kiapo kwenye halmashauri hiyo, kushirikiana na wananchi na kujiepusha kuwagawa katika maendeleo ili kujenga usawa na Demokrasia kwa wote.
Amesema muda wa uchaguzi umekwisha na kwamba ni wakati sahihi wa kuwaunganisha wananchi kimaendeleo na kutumia lugha rafiki ili kuondoa ukakasi unaotokana na kauli za viongozi.
Hata hivyo, Mbunge wa Jimbo la Biharamulo, Mhandisi Ezra Chiwelesa, amewataka watumishi wa halmashauri hiyo kupanga mipango ya maendeleo kuendana na Ilani ya CCM ili kuondoa mkanganyiko wa utekelezaji wa miradi hiyo kwa jamii.
Kadhalika amesema maendeleo yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita umetokana na usimamizi mzuri wa watumishi, Madiwani na Mbunge wa Jimbo hilo huku akiwasisitiza Madiwani kuziishi ahadi walizotoa kwa wananchi wao.
