Matarajio ya wadau ujio chuo cha teknolojia ya kidijitali

Arusha. Wadau wa elimu wamepongeza mpango wa Serikali wa kujenga Chuo cha Teknolojia ya Kidijitali, wakisema kitasaidia kuongeza wataalamu wa ndani, kukuza ajira, kuendeleza sekta mbalimbali pamoja na kuimarisha usalama wa nchi.

Wadau hao wamesisitiza kuwa ushirikishwaji mpana wa wadau katika hatua za kuanzisha chuo hicho, ni muhimu ili kiweze kufanya kazi kwa ufanisi na kutoa matokeo chanya kwa Taifa.

Wazo la kuanzishwa kwa chuo hicho lilielezwa na Rais Samia Suluhu Hassan alipozindua Bunge la 13 hivi karibuni, akitaja chuo hicho kama sehemu ya dhamira ya Serikali kufanya maboresho katika sekta ya elimu.

Mhadhiri wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Edsona Nyemalila, anasema kasi ya ukuaji wa teknolojia, inahitaji uwepo wa wataalamu wengi wa ndani, na kwamba chuo hicho kitakuwa chachu ya kufanikisha azma ya Serikali ya kukuza uchumi wa viwanda.

 “Ili kuleta maendeleo kwa vijana na kuwainua kiuchumi, ni lazima kuwekeza kwenye teknolojia. Hatuwezi kukuza viwanda bila kuwa na wataalamu wa kutosha wa teknolojia. Ndoto ya kuendeleza viwanda itatimia tu tukiongeza nguvu kwenye teknolojia,” anasema.

Anasema  chuo hicho kitaongeza wataalamu wa kutengeneza mifumo mbalimbali, kugundua teknolojia mpya na kupunguza utegemezi wa mifumo kutoka nje ya nchi.

“Tumetegemea sana mifumo kutoka nje. Unakuta mtu anatoka China anakuja kutengeneza mfumo, akiondoka ukipata changamoto unamlipa tena arudi kurekebisha. Pia mifumo kutoka nje ipo kwenye hatari kubwa ya kudukuliwa. Lakini vijana wetu wakitengeneza mifumo ya ndani, wataweza kuilinda na kuboresha,” anaongeza kusema.

Anabainisha kuwa chuo hicho pia kitachochea ukuzaji ajira na kuimarisha sekta kama afya, kilimo, uchumi, utalii na biashara.

Akitolea mfano Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), anasema ilianza kwa hatua ndogo lakini sasa ni taasisi kubwa yenye mchango mkubwa katika sayansi na teknolojia.

 “Chuo kipya kitazalisha wataalamu wengi zaidi, hasa kwa kuwa NM-AIST inadahili wanafunzi wachache. Kikianza kwenye ngazi ya cheti, kitatoa wataalamu kuanzia ngazi ya chini hadi juu, ” anaeleza.

Kwa upande wake, mdau wa elimu Profesa Raymond Mosha, anasema kutokana na wingi wa vijana nchini, chuo kimoja pekee huenda kisitoshe kukidhi mahitaji.

 “Kwa idadi ya vijana tuliyonayo, nadhani ingekuwa vyema kuwe na matawi ya teknolojia kwenye vyuo mbalimbali ili kudahili wanafunzi wengi zaidi. Nje ya nchi karibu kila chuo kikuu kina kitengo cha teknolojia ambacho kinawajengea wanafunzi msingi muhimu,” anasema.

Anatoa mfano wa namna anavyofundisha mtandaoni kwa wanafunzi walioko Marekani wakati yeye yuko Tanzania, akisema uzoefu huo unaonesha umuhimu wa wataalamu wa ndani waliobobea katika teknolojia.

Naye Mwalimu wa Shule ya Msingi Enaboishu Olorien, Arumeru, Jenipher Chuwa, anasema kuanzishwa kwa chuo hicho, kutaimarisha matumizi ya Tehama katika sekta ya elimu.

Anasema utekelezaji wa mpango huo utafanikiwa zaidi,  endapo Serikali itashirikiana kwa karibu na wadau mbalimbali wa elimu.

“Jukumu la kuboresha elimu si la walimu pekee au la wizara . Ni suala mtambuka linalohitaji ushirikiano wa wadau wote nchini. Naipongeza Serikali kwa hatua hii, kwani maendeleo ya teknolojia hayaepukiki,” anasema.