Maulid ashinda umeya manispaa ya Kigoma

Kigoma. Diwani wa kata ya Mwanga Kusini, Manispaa ya Kigoma Ujiji, Mussa Maulid amechaguliwa kuwa Meya wa Manispaa hiyo kwa kupata kura 24 za ndiyo kati ya kura 25 za madiwani waliohudhuria kikao cha baraza hilo.

Uchaguzi huo umeenda sambamba na kuwaapisha madiwani wa halmashauri hiyo, leo Jumanne, Desemba 2, 2025 mjini Kigoma katika ukumbi wa NSSF ambapo wajumbe wa baraza la madiwani wa manispaa hiyo kwa umoja wao walimchagua diwani huyo.

Maulid amechaguliwa kuwa meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa kupata kura 24 za ndiyo kati ya kura 25 za madiwani waliohudhuria baraza hilo ambapo alipata kura moja ya hapana.

Madiwani wa halmashauri ya Manispaa ya Kigoma ujiji wakila kiapo leo Jumanne , Desemba 2, 2025

Akitangaza matokeo hayo ofisa tawala kutoka ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Dollar Buzaire amemtangaza Mgeni Kakolwa kuwa Naibu Meya wa manispaa hiyo kwa kupata kura 24 za ndiyo na moja ya hapana.

Msimamizi huyo wa uchaguzi amewataka madiwani hao kusimamia viapo vyao kwa kuhakikisha wanasimamia maadili, nidhamu na kujituma ili kuleta maendeleo kwa wananchi wa manispaa hiyo akiwataka kuzingatia suala muhimu la ukusanyaji mapato ya halmashauri.

Madiwani wa halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, wakiwa ukumbini wa mikutano mjini Kigoma kwaajili ya kikao cha kuapishwa na kufanya uchaguzi wa kumchagua Meya na Naibu Meya.

Akizungumza  baada ya kuchaguliwa Maulid amesema ataenda kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri ya manispaa hiyo ili kuhakikisha yanafika Sh500 milioni kutoka Sh400 milioni kwa mwezi.
“Kwa kipindi changu cha miaka mitano cha kuongoza halmashauri ya manispaa yetu ya Kigoma Ujiji, nitahakikisha nasimamia makusanyo ya ndani kwa kuongeza mapato ya kila mwezi, lakini pia nitahakikisha nachochea miradi ya maendeleo kwa wananchi,” amesema Meya Maulid.