Milioni 500 za NMB zilivyorejesha tabasamu kwa watoto 125 JKCI

Dar es Salaam. Jumla ya watoto 125, wamepata msaada wa upasuaji na matibabu ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kipindi cha Novemba mwaka 2024 hadi Novemba 2025, baada ya Benki ya NMB kutoa kiasi cha Sh500 milioni.

Benki hiyo imetoa kiasi cha Sh1 bilioni kwa ajili ya kuiwezesha taasisi hiyo kutoa matibabu ya moyo ya watoto 250 katika kipindi cha miaka minne, hatua iliyosaidia kubadili maisha ya familia zisizojiweza nchini.

Ahadi hiyo, iliyotolewa Novemba 2 mwaka jana, inalenga kugharamia upasuaji na matibabu ya watoto wanaokabiliwa na magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo na matatizo mengine ya mfumo wa moyo, hususani wale wanaotoka katika familia zenye kipato duni.

Jana, Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, aliongoza ujumbe wa maofisa waandamizi wa benki hiyo kutembelea JKCI, ambapo alitangaza kuwa benki hiyo imeshatoa Sh500 milioni, sawa na nusu ya ahadi yote.

Kwa mujibu wa Zaipuna, kiasi hicho kimesaidia kuwezesha upasuaji na matibabu ya moyo ya watoto 125.

“Tunawashukuru sana JKCI kwa kazi yao ya kipekee ya kufanya upasuaji huu na tunaahidi kuendeleza ushirikiano huu ili kuwasaidia Watanzania hasa familia zisizojiweza kupata matibabu na huduma stahiki,” alisema.

Aliongeza kuwa kiasi kingine cha Sh250 milioni kitatolewa Januari mwakani ili kuhakikisha mchakato wa matibabu magonjwa ya moyo ya watoto unaendelea na kufanyika bila kukwama.

Zaipuna pia alisisitiza kuwa msaada wa NMB hauishii kwenye fedha pekee.

Benki hiyo itaendelea kuimarisha ushirikiano wake na JKCI, Heart Team Africa Foundation, na Global Medicare ili kupanua wigo wa huduma, kuongeza kasi ya upasuaji, na kuimarisha miundombinu ya huduma za moyo kwa watoto.

Moja ya mapendekezo na maombi aliyoyapokea ni suala la kuanzisha “Recovery House” kituo maalumu cha kuwapokea watoto wanaosubiri upasuaji au kuendelea na matibabu ambacho kitasaidia kupunguza mzigo wa kifedha na changamoto za makazi kwa familia kutoka maeneo ya mbali.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge, amesema NMB imekuwa mdau namba moja katika kusaidia familia zisizojiweza kupata huduma muhimu za moyo.

Bingwa huyo wa magonjwa ya moyo alibainisha kuwa mchango wa benki hiyo umeongeza ufanisi wa huduma, kupunguza muda wa kusubiri na kuongeza idadi ya watoto wanaoweza kutibiwa kila mwaka.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Heart Team Africa Foundation, Dk Naizihijwa Majani, alisema ufadhili wa NMB umewanufaisha watoto kutoka mikoa 20.

“Kati ya watoto 185 waliofanyika upasuaji mwaka huu, 125 wamefadhiliwa na NMB, jambo linalothibitisha ukubwa wa uhitaji na thamani ya msaada unaotolewa kwa wakati,” alibainisha.

Kwa akina mama Veronica Temba na Asimina Issa kutoka Kilimanjaro, wamesema msaada huo umekuwa mwanga wa matumaini.

Wakiwa hawana uwezo wa kugharamia upasuaji wa moyo, waliuelezea mchango wa NMB kama “baraka ya kweli” kwa familia zao.