Kikosi cha Simba kimerejea mapema asubuhi ya leo kikitokea Bamako, Mali kilipoenda kucheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Stade Malien na kupoteza kwa mabao 2-1.
Kipigo hicho kilikuwa ni cha pili mfululizo Simba katika makundi ya michuano hiyo baada ya kile cha kwanza cha bao 1-0 nyumbani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa mbele ya Petro de Luanda uliochezwa Novemba 23, 2025.
Kupoteza mechi hizo mbili kunaifanya Simba kuwa ya mwisho katika msimamo wa kundi D kwa kutokuw na pointi, huku Petro ikiongoza kwa pointi 4, sawa na Stade Malien iliyopo nafasi ya pili zikitofautiana idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa na Esperance ikiwa ya tatu kwa pointi mbili kila moja ikicheza mechi mbili hadi sasa.
Akizungumza katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere l, Meneja wa timu hiyo Dimitar Pantev amesema licha ya kupoteza michezo miwili bado wana nafasi ya kufanya vizuri na kufikia malengo ya klabu ya kuvuna hatua hii ya makundi (kufuzu robo fainali) CAFCL.
“ Haukuwa mchezo mwepesi, licha ya kuwa tulitengeneza nafasi nzuri za kupata matokeo kama tatu na hatukuzitumia, tulifanya makosa wakatuadhibu ndio ni matokeo ya mpira wa miguu,” amesema Pantev na kuongeza;
“Kushindwa kutumia nafasi tulizotengeneza siwezi kusema ni suala la kimbinu au saikolojia, labda hatukuwa bora zaidi kiwanjani hata ukitazama wachezaji ni wazoefu katika aina hii ya mashindano, ila ni jambo ambalo tunatakiwa kulifanyia kazi katika kiwanja cha mazoezi ili tuwe bora zaidi.”
“Siwezi kuwalaumu wachezaji wangu kwamba nikijitoa kwa kila kitu na wao kushindwa kuyafanyia kazi maelekezo, lakini jambo kama hili likitokea huenda kila mtu anamakosa yake, mimi kama kocha, wasaidizi wangu au wachezaji wenyewe, tuna muda wa kutathimini upya kuelekea michezo ijayo,” amesema Pantev na kuongeza;
“Nafahamu haitakuwa rahisi katika michezo minne iliyobaki, ila tutapambana kufikia malengo ya klabu, kwani kufika robo fainali ya mashindano haya ni moja ya malengo yetu.”
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Crescentius Magori akiwa mmoja wa msafara wa viongozi waliosafiri na timu amewataka mashabiki kutokana tamaa, kwani viongozi pamoja na benchi la ufundi litaendelea kupambana kuangalia warekebishe wapi.
“Mashabiki wasiikatie tamaa timu yao, tumecheza mechi mbili tumepoteza zote zimebaki nne mkononi, kila mtu atafanya linalowezekana na kuona wapi tulikosea na kurudi kuona wapi tunatekebisha ili kufanya vizuri zaidi”.
Baraka Mpenja, Mwandishi na mtangazaji wa soka wa kampuni ya Azam TV alikuwa mmoja wa waandishi wa habari waliosafiri na timu hiyo kwenda Mali.
Akiwa huko alihudhuria mazoezi na kuzungumza na benchi la ufundi kabla na baada ya mechi hiyo dhidi ya Stade Malien.
Mpenja amesema licha ya kuwa Simba ilifanya maandalizi mazuri wapinzani wao pia walijiandaa vyema na sio mpinzani wa kubeza.
Amesema kwa hali iliyofikia sasa wachezaji wa klabu hiyo wanatakiwa kujitathimini na kuipambania nembo ya klabu hiyo.
“Simba na Malien zilifanya maandalizi bora sana kabla ya mchezo nilihudhuria mazoezi yao, lakini Malien ilionekana kuwa bora zaidi kiwanjani na hata kupata ushindi,” amesema Mpenja na kuongeza;
“Walikuwa wakishambulia kwa nguvu na kucheza kwa kasi sana tofauti na Simba, wakati Simba wakishambulia Malien walitumia nguvu kubwa kukaba na wakiupata mpira walishambulia kwa kasi kubwa.”
“Kwa upande wa Simba wao ilikuwa tofauti, walikuwa na nafasi nyingi ambazo wangezitumia wangepata faida, walikuwa vibaya sana kipindi wakinyang’anywa mipira baadhi ya wachezaji walikuwa kama abiria wakishindwa kuutafuta mpira na kurudisha kwenye himaya yao.”
Mpenja ameongeza kwa kusema, shida ya Simba sio kocha kama wengi wanavyodhani, kwani timu hiyo inatengeneza nafasi na tuliona katika mechi zote na kuwa na nafasi rahisi kufunga zilitengenezwa lakini hazikutumika.
“Shida ya Simba sio kocha, kwani tunaona timu ikitengeneza nafasi na wachezaji kushindwa kuzitumia, kocha hakufundishi kufunga bali utashi wa mshambuliaji mwenyewe, shida Simba ipo katika kupambana.”
“Baadhi ya wachezaji Simba hawapambani kutafuta matokeo mazuri, wengine wamekuwa kama watalii uwanjani, huwezi kupata ushindi kwa kutembea kiwanjani, namna wanavyocheza wakipoteza mipira sio kwa kupambana na hii itabidi kubadilika na hapa ndipo ilipo tofauti ya Simba na Yanga. Yanga wanacheza jihadi sana na matokeo yake yanaonekana,” Mpenja amesisitiza.
“Wachezaji wa Simba wanatakiwa kujua wanacheza katika timu kubwa namba tano kwa ubora Afrika, kuishia hatua ya makundi ni fedheha kwa kiwango walichoonyesha kwa miaka ya hivi karibuni.”
Baada ya kurejea nchini, Simba sasa itacheza mechi mbili za Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbeya City na Azam FC kabla ya kupisha maandalizi na mashindano ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 yatakayoanza Desemba 21 hadi Januari 18 mwakani na baada ya hapo itaendelea na CAFCL ambapo itakuwa nyumbani dhidi ya ES Tunis.