Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametoa msimamo wa Serikali anayoiongoza, akisema haitakubali kupangiwa cha kufanya, wala kupewa masharti na yeyote, badala yake ataongoza kwa misingi ya Katiba na sheria.
Msimamo huo wa Rais Samia, unajibu matamko ya wadau mbalimbali likiwamo la Bunge la Ulaya (EU), lililoitaka Tanzania kumtoa mahabusu bila masharti Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu ili iendelee kuipa misaada Tanzania.
Lakini, kauli hiyo pia inajibu makundi mengine katika mitandao ya kijamii, yanayotoa masharti ya maridhiano na Serikali, ikiwamo ikubali kuwawajibisha waliohusika na mauaji ya watu siku ya maandamano yaliyozaa vurugu Oktoba 29, mwaka huu.
Msimamo huo wa Rais Samia pia, umetokana na matamko na masharti yanayotolewa na wadau mbalimbali likiwamo Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) baada ya tukio la Oktoba 29 kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali za watu binafsi na umma.
Rais Samia ametoa msimamo huo leo, Jumanne Desemba 2, 2025 alipozungumza na wazee wa Jiji la Dar es Salaam katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC).
Ametumia dakika 60 kuzungumzia masuala mbalimbali.
Rais Samia amesema kumeibuka wadau wa kimataifa wanaoipangia Tanzania mambo ya kufanya, akihoji wao ni kina nani hasa hadi waipangie nchi huru.
Amesema Tanzania ni nchi huru na sio koloni la yeyote kwa sasa.
Amesema mataifa yanayoipangia nchi cha kufanya mara kadhaa yanakumbwa na hali kama hiyo, lakini hayapangiwi cha kufanya.
“Who are you (wewe ni nani),” amehoji Rais Samia kwa wale wanaotaka kuwapangia Watanzania cha kufanya huku akionesha mshangao.
“Nataka niwaambie ndugu zangu, kawaida mwanamke mzuri ndiye anayepiganiwa, uongo kweli? Utakuta watu wanafokeana wanapigana ukicheki majanadume mawili yanapigana katikati kuna mwanamke mzuri.
“Sasa nchi yetu hii, Mungu ametuumba vizuri, katuweka pazuri sana. Kama navyowaambia Tanzania ni lango la kuingia Afrika, tatizo ni siasa tuliyonayo ya kutofungamana na upande wowote,” amesema.
Rais Samia amesema pia kuna mali yakiwamo madini, bahari, maziwa, ardhi yenye rutuba, madini adimu, hivyo nchi inapigwa kwa vile ilivyoumbwa.
“Maumbile yetu na utajiri wetu isiwe laana tukauwana sisi kwa sisi,” amesema.
Pia, amesema Tanzania haikuwa inapigwa mawe kwa kuwa ilihesabika kuwa masikini, lakini ulipofunguliwa utajiri, kuna watu wanaumia.
Katika kudhihirisha msimamo huo, Rais Samia amesema amewasikia wanaodai hawatakubali kukaa na Serikali iwapo mambo kadhaa yatafanywa, akieleza Serikali yake sio ya kuamrishwa wala kupewa maelekezo.
“Serikali haipewi masharti hayo, labda Serikali ya wanafunzi kwa walimu wao. Lakini nchi huru inayojielewa na kuendesha mambo yake mmh… mmh…kama ni Watanzania wa kweli walishasema, walishatoa uamuzi wameipa CCM (Chama cha Mapinduzi) asilimia 97 hayo ndio maamuzi ya wananchi, wananchi wanaowasemea wao ni wepi,” amesema.
Katika hotuba yake hiyo iliyoanza saa 6:25 hadi 7:25 mchana, amesema nguvu iliyotumika na vyombo vya dola kudhibiti vurugu hizo, iliendana na ukubwa wa tukio lenyewe na kwamba ameapa kuilinda nchi, mipaka yake na usalama wa raia wake.
“Sasa tunapoambiwa kwamba tulitumia nguvu kubwa sana kwenye tukio lile, nguvu ndogo ilikuwa ni ipi? Ilikuwa tuwaangalie waandamanaji waliojiandaa kufanya mapinduzi mpaka wafanikiwe? Hapo patakuwa pana dola kweli, dola haipo hivyo,” amesema.
Rais Samia amesema jambo kama hilo, limeshuhudiwa pia katika maeneo mengi, panapotokea vurugu kama hizo, Serikali hutumia nguvu kubwa kudhibiti.
“Sasa wanapokuja kutulaumu mlitumia nguvu kubwa, wao walitaka nini, tujiulize wao ndio wafadhili wa kile kilichofanyika? Walitaka tuangalie ile ‘mob’ hadi ifanikiwe kile walichowapa fedha walichowatuma? Hapana tuliapa kuilinda nchi na mipaka yake,” amesema.
Katika kufanya shughuli za ulinzi wa nchi na usalama wa raia wake, amesema Serikali itafanya kila inavyowezekana kuhakikisha inatimiza wajibu wake.
Lilikuwa jambo la kupangwa
Katika hotuba hiyo, amesema kilichotokea ni jambo lililopangwa na walioliandaa walidhamiria kuangusha dola ya nchi na vijana walifanywa makasuku na kuyumbishwa.
“Lile lilikuwa ni jambo la kupangwa na vurugu zile zilidhamiria makubwa. Vurugu zile ni mradi wenye nia ovu wenye wafadhili, washtiri na watekelezaji.
“Wapo walioingia kwa kufuata mkumbo tu pengine kwa ahadi ya maisha mazuri baadaye,” amesema.
Kinachothibitisha hilo ni tukio lililopangwa, amesema miundombinu na majengo mbalimbali ya umma na watu binafsi yaliunguzwa.
Rais Samia amesema hilo linafanya tukio hilo ligeuke kutoka kuwa na sura ya maandamano hadi vurugu zilizoandaliwa kwa dhumuni maalumu.
Hata hivyo, amehoji kwanini imefanyika siku ya uchaguzi, akisema walishajua ushindi mkubwa wa CCM, kutokana na kazi iliyofanywa kabla.
Amesema hata wapinzani walikataa wenyewe kuingia kwenye uchaguzi kwa sababu walishajua wasingefanikiwa na aibu ingewapata.
Katika hilo, amesema kuna waratibu wanaoishi nje ya nchi, wengine wanajulikana na wengine hawajulikana, Serikali inawatafuta ili kuwajua.
“Hili jambo lina waratibu kutoka nje, lakini kwanini waratibu kutoka nje? Wale waratibu kutoka Tanzania tunawajua, ni shida za maisha, akisukuma maandamano, umbea… Watanzania wale wale vijana wanatumia fedha zao kununua bando kuwasoma, ukisoma yeye anapata fedha,” amesema.
Pia, amesema wapo ambao hawana shida ya maisha wako pazuri, wanalipwa na hao wanaotaka hayo yatokee, lakini wamekosa uzalendo na ukiwatazama vizuri sio Watanzania kamili.
Rais Samia amesema wakati anaingia madarakani alinyoosha kile alichokiita mkono wa rehema kwa wapinzani kwa kuzungumza nao na kuwataka warudi.
Amesema kuna wakati, alilazimika kutumia hata posho zake za safari kuwawezesha kwa kuwa hawakuwa na kitu, lakini baada ya yote wamepata nafasi ya kurudi nchini na kuanza kumtusi.
“Nikidhani nawanyooshea watu wa nchi. Ni hawahawa walioniambia sawa, tutarudi lakini tuna kesi, nikawaambia nitazifuta njooni tutazifuta mje tujenge nchi,” amesema.
Amesema walitaka kufanya maandamano wakasindikizwa hadi walipofika na wakatawanyika na kwamba yale ndio maandamano.
Licha ya Rais Samia kutowataja kwa majina lakini miongoni mwa viongozi wa kisiasa waliokuwa wakiishi ughaibuni ni Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, mbunge wa zamani wa Arusha Mjini, Godbless Lema na aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Viktoria, Ezekiel Wenje ambaye hata Oktoba 13, 2025 alitimkia CCM.
Rais Samia amesema baadhi walisema hawana fedha, lakini aliamua kutoa posho zake kuwapa wapate za kutumia waliporejea nchini, lakini wanachokifanya sasa hakikubaliki.
Bila kuwataja majina, amesema viongozi hao walidai kuwapo na kesi za viongozi akiwamo Lissu na wanachama wao, jambo alilosema kesi nyingi zilifutwa lengo ni kurudisha umoja.
Kuhusu vijana, amesema wengi wameingizwa njiani wakaimbishwa wimbo wasioujua wa kudai haki, lakini kiuhalisia hakuna anayejua.
Ameonesha kushangazwa na wale wanaodai wameandamana kwa sababu ya maisha magumu, akidokeza hali ya Tanzania ni bora zaidi ya nchi nyingine nyingi za Afrika Mashariki.
“Ningekuwa na uwezo ningebeba vijana wa Tanzania nikawatupa kwenye nchi tofauti tu wakaone ugumu wa maisha uliokuwepo,” amesema.
Hata hivyo, amesema yote yanatokea kwa sababu vijana wameachwa bila mwelekeo na wamekosa watu wa kuwaongoza.
“Vijana wazalendo hasa kutoka vyama vya upinzani walikuja kutwambia, jamani kaeni vizuri kuna hili. Na hilo tumejifunza tunakwenda kulifanyia kazi,” amesema.
Katika hotuba yake hiyo, amewataka viongozi wa dini kuacha kujivika majoho ya kuendesha nchi kwa utashi wao binafsi, akisisitiza Tanzania itaongozwa na Katiba.
Amesisitiza Tanzania haitaendeshwa kwa madhehebu ya dini bali kwa mujibu wa Katiba yake na kwamba hakuna kiongozi wa dini mwenye dhamana ya kutoa matamko ya namna ya uendeshaji wa nchi.
“Ubora wa dini upo mioyoni mwetu, hakuna overriding hapa…Kwamba mimi dini yangu, nitaoveriding Tanzania, nikilitoa ndio hilohilo.
“Toka nimekaa (ameingia madarakani Machi 19, 2021) matamko nane yametolewa na TEC, lakini ukienda chini wenyewe kwa wenyewe wanapingana, matamko hayafanyi kazi vizuri,” amesema.
Amesema Tanzania ni nchi ya umoja, mshikamano, akiwataka Watanzania kutokubali kuvurugana kwa misingi ya dini na kisiasa, hata kama aliyeopo madarakani hawampendi.
Amesema dini zote zinasema kila mamlaka imeletwa na Mungu bila kujali ni mwanamke au mwanamume na hakuna anayejua sababu ya kuletwa kwa mamlaka hiyo.
“Niwaombe sana viongozi wa dini tuvae majoho ya kuonesha sura halisi, hakuna kitabu chochote kilichosema tutazitumia dini zetu kuvuruga nchi zetu,” amesema.
Amewasisitiza viongozi wa dini wasiivuruge nchi na kama kuna lolote njia sahihi za mazungumzo zipo na kukaa kujadiliana, hakuna sababu ya kufika tulipofika.
Miongoni mwa matamko ambayo TEC imeyatoa ni la Novemba 15, 2025 ililaani matukio ya Oktoba 29, 2025 ikitaka wote waliokamatwa kabla, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi kuachiwa huru huku ikikumbushia mchakato wa Katiba mpya.
Maaskofu hao walitoa tamko hilo baada ya tafakari na sala walizozifanya kwa siku nne Novemba 11-14, makao makuu ya TEC, Kurasini jijini Dar es Salaam.
Pia, walitaka viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama kuwajibika kwa kujiuzulu kutokana na yaliyotokea Oktoba 29.
Maaskofu hao walitaka kufanya uchunguzi huru na wa haki kuhusu wadau wa ndani na kimataifa.
Kuhusu suala la mchakato wa Katiba, Rais Samia amesema suala hilo kwa sasa haliwezi kufanyika kwa sababu nchi imeingia kwenye mgawanyiko, hivyo maridhiano yakifanyika mchakato huo utaendelea tena kwa kuwa, hakuna anayebisha juu ya umuhimu wa Katiba mpya.
Rais Samia amesema safari ya kusaka madaraka mwaka 2030 isiende kuivuruga nchi na anamwangalia mmoja mmoja kati ya wateule wake, atakayemwona ana nia na hilo atamuondoa.
“Ile safari ya 2030 isiende kutuharibia nchi. Ndugu zangu mengine yaliyosemwa na wazee hapa nimeyapokea, waziri wao yupo ambaye atashughulikia shida zao,” amesema.
Pia, amesema Mungu ndiye anayejua kuhusu nani atakayekuwa kiongozi wa Tanzania, mwaka 2030 hivyo hata ujiandae vipi hakuna mwenye uhakika na nafasi hiyo.
Katika hotuba hiyo, amesema huu sio wakati wa kukaa na kunyoosheana vidole bali kushikana na kukubaliana kwamba, kila kilichomo ndani kiwanufaishe Watanzania.
“Lililopita limepita, kwa maneno tunasikia lipo lingine linapangwa lakini Inshallah Mola hatasimama nao litapeperuka,” amesema.
Kuhusu madai ya maandalizi ya maandamano yajayo Desemba 9, amesema wakati wowote yatakapofanywa, Serikali imejipanga kuyakabili wakati wowote.
“Kama wanadamu hukosana wakaelewana, hatusemi Serikali labda tuko sawa hatuna makosa inawezekana kabisa tuna upungufu na hakuna Serikali duniani isiyo na mapungufu. Lakini wanakaa wanazungumza na kuondoa mapungufu yaliyopo,” amesema.
Aidha, Rais Samia amesema kwa vyovyote vile Tanzania haikupaswa kuvuruga amani wala kusababisha vifo vya raia kwa sababu kifo cha mmoja kinawagusa wote.
“Natoa pole kwa wale wote walioondokewa na ndugu na jamaa zao, kwani hawa ni ndugu zetu sote. Damu ya Mtanzania mmoja ni damu yetu sote,” amesema.
Awali, akitoa salamu mbele ya Rais Samia, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Dar es Salaam Salum Matimbwa amesema kundi hilo limefadhaishwa na matukio ya vurugu Oktoba 29, mwaka huu, huku wakiahidi kuendelea kuwashauri vijana watambue safari ya maendeleo yao inahitaji amani.
Ametumia jukwaa hilo kurejea historia ya kuwepo kwa kodi ya kichwa nchini, iliyochukiwa na wengi enzi hizo, akisema hakuna aliyeingia barabarani kuandamana, badala yake Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliongoza mazungumzo hadi mambo yakabadilika.
Amesema vurugu zilizotokea zimewashtua na kuwafadhaisha kwa sababu zimeambatana na vifo, mali za watu zimeharibiwa na miundombinu inayosaidia watu imeathiriwa.
“Kwa kweli imetufadhaisha. Wazee tumesikitishwa na vifo vilivyotokea na uharibifu huo na tunamuomba Mungu awahifadhi wale waliotangulia na awaweke mahali pema wanapostahili,” amesema.
Hata hivyo, ameeleza kufurahishwa na hatua ya Rais Samia kuonesha kuchukizwa na matukio hayo na kauli yake ya kurudisha amani.
Amesema wakati nchi inatawaliwa na wakoloni, kulikuwa na kodi ya kichwa na isingewezekana kutoka eneo moja kwenda lingine kama haujalipa.
Pamoja na yote hayo, amesema hakuna aliyeingia barabarani, bali Mwalimu Nyerere aliongoza mazungumzo na hatimaye yote yamekwisha, ndio maana kwa sasa wanashangaa yaliyotokea imekuaje.
