‘Risasi zitakapopigwa, hazitachagua huyu ni wa dini gani’

Dar es Salaam. Ujumbe wa Umoja wa Wahadhiri wa Kiislam Tanzania (Uwakta), umesema utaendelea kuhubiri amani ya nchi kwa kuwa pindi risasi zitakapopigwa hazitachagua huyu ni wa dini gani.

Wahadhiri hao wameyasema hayo leo Jumanne Desemba 2, 2025, kwenye mkutano na vyombo vya habari uliofanyika Msikiti wa Kindande Mtoni kwa Azizi Ally, jijini Dar es Salaam.

Lengo la mkutano huo ni kuhusu umuhimu wa kuendelea kulinda amani nchini.

Wakiongozwa na Sheikh Said Kinyogolo amesema wana uchungu na uhuru wa nchi hii kwa kuwa waliupigania hivyo wanaposikia watu wanataka kuuharibu wanaumia.

“Licha ya baadhi ya watu kutudhihaki tunapoyasema haya na wengine kufikia hatua ya kutuita ‘masheikh ubwabwa’, katu hatutaacha kuendelea kuihubiri amani na tuna imani Mungu atatuvusha salama kwa kuwa pia Watanzania walio wengi wanataka amani na nchi yao,” amesema Kinyogolo.

Kwa upande wake, Sheikh Ibrahim Mohammed amesema, “Katika hili tunaomba Mwenyezi Mungu ailinde amani ya nchi hii na hawa wanaotaka kulichoma taifa hili na kutuchonganisha awatafutie kazi zingine za kufanya, kwa kuwa katika makuzi kwenye miaka yote hiyo hatujalelewa hivyo,” amesema Sheikh Mohammed.

Sheikh Ibrahim Lubango amesema kwa muda sasa kumekuwa na mjadala mpana wa maneno ya haki na amani ambapo wapo wanaosema haki kwanza halafu amani.

“Kuna wanaosema haki bila amani haki haiwezi kuwepo lakini ukweli kikanuni neno linalotangulia ni amani.”

“Mfano juzi tu hapa tuliona wenzetu Taifa la Palestina watoto walikuwa wanapigwa ni wapi mtu angeweza kwenda kushtaki Polisi kuwa anapigwa wakati hakuna amani,” amesema Sheikh huyo na kuongeza.

“Hata hivyo hatumaanishi haki sio jambo la msingi bali kuna haja ya kutengenezea njia nzuri ya kuweza kuipata na pia isiwe sababu ya kuharibika kwa Taifa letu,” amesema Sheikh Lubango.