Sababu Chuo Kikuu cha Mwanza kufungiwa kudahili shahada ya udaktari

Mwanza. Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imekifungia Chuo Kikuu Mwanza (MzU) kudahili wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Shahada ya Udaktari wa Binadamu kwa mwaka wa masomo 2025/26, huku ikiwaruhusu wanafunzi waliodahiliwa kutafuta na kuomba kuhamia vyuo vingine baada ya chuo hicho kubainika kudahili wanafunzi mara kumi zaidi ya idadi iliyoruhusiwa kisheria.

Akizungumza na waandishi wa habari chuoni hapo leo Jumanne, Desemba 2, 2025, Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa amesema hatua hiyo imelenga kulinda ubora wa elimu na kuhakikisha kuwa vyuo vikuu vinazingatia kikamilifu sheria, kanuni na viwango vilivyowekwa katika uendeshaji wa programu za elimu ya juu nchini.

Amesema maamuzi hayo yalifanywa kwenye kikao maalumu cha 127 cha tume hiyo kilichofanyika Novemba 28, 2025 baada ya ukaguzi kubaini chuo hicho kilikiuka kwa kiwango kikubwa taratibu na miongozo ya udahili kwa kudahili idadi ya wanafunzi iliyozidi uwezo wake wa miundombinu na rasilimali watu, ikiwemo uhaba wa walimu wa kutosha kwa programu hiyo.

Profesa Kihampa amesema kuanzia Julai 15 hadi Oktoba 20, 2025, udahili wa wanafunzi wa Shahada ya kwanza uliendeshwa nchi nzima, ambapo kila chuo kilitakiwa kufuata vigezo na idadi iliyoainishwa katika mwongozo wa udahili kwa mwaka wa masomo 2025/26.

Hata hivyo, Chuo Kikuu Mwanza kilikaidi maelekezo hayo kwa kudahili idadi ya wanafunzi mara kumi zaidi ya kiwango kilichoidhinishwa.

Kutokana na hali hiyo, Tume imeamuru chuo hicho kusitisha mara moja udahili na usajili wa wanafunzi wote wa mwaka wa kwanza wa Shahada ya Udaktari wa Binadamu kwa mwaka wa masomo 2025/26, licha ya chuo hicho kupewa maelekezo ya kurekebisha idadi hiyo bila kufanikiwa kufanya hivyo.

Pamoja na hatua hiyo, Tume imetoa kibali kwa wanafunzi wote waliokwisha kudahiliwa na kuripoti chuoni hapo kuomba kuhamia katika vyuo vingine vilivyoidhinishwa kutoa programu ya Udaktari wa Binadamu au kozi nyingine wanazozipendelea kuanzia mwaka wa masomo 2025/26 au miaka itakayofuata, kulingana na nafasi zitakazokuwa zinapatikana.

Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Profesa Charles Kihampa akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Chuo Kikuu Cha Mwanza mkoani humo. Picha na PraiseGod Mgumba

Chuo hicho kimeelekezwa kuwataarifu rasmi wanafunzi walioathirika kuhusu uamuzi huo na kuwasaidia kukamilisha taratibu zote zinazohusu uhamisho wao kwenda vyuo vingine vitakavyowapokea.

“Tume inawaasa wanafunzi walioathirika na mabadiliko haya kuwa watulivu kwa kuwa suala hili linashughulikiwa kwa kuzingatia maslahi mapana ya wanafunzi na jamii kwa ujumla. Tume kwa kushirikiana na Chuo Kikuu Mwanza, pamoja na vyuo vitakavyowapokea wanafunzi husika, itahakikisha kuwa mchakato wa uhamisho unatekelezwa kwa haraka na ufanisi,”amesema Profesa Kihampa.

Wakati huohuo, Tume imeunda timu maalum ya wataalamu kuchunguza mwenendo wa masuala ya kitaaluma katika chuo hicho ili kubaini chanzo cha ukiukwaji huo na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kurekebisha hali na kuhakikisha chuo kinarejea katika uzingatiaji wa sheria, kanuni na taratibu za elimu ya juu.