Mwanza. Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, limemthibitisha Diwani wa Kata ya Mhandu, Sima Constantine kuwa Mstahiki Meya wa jiji hilo kwa kipindi cha pili kuanzia mwaka 2025-2030.
Sima ambaye alikuwa Meya kwa kipindi kilichopita 2020-2025, amepitishwa leo Jumanne Desemba 2, 2025 katika kikao cha kwanza cha baraza hilo ambalo madiwani wake wote kutoka kata 18 ni wa Chama cha Mapinduzi (CCM), lililokaa katika ukumbi wa halmashauri hiyo.
Ambapo, kikao hicho kimehudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi, Mbunge wa Nyamagana, John Nzilanyingi, wakuu wa idara, watendaji wa mitaa na kata, na wananchi, huku madiwani wote wakila kiapo, ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma, na kukabidhiwa vifaa vya kazi.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi (kushoto), akimkabidhi vitendea kazi, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya jiji la Mwanza, Sima Constantine Sima (kulia) baada ya kuthibitishwa na baraza la madiwani. Picha na Damian Masyenene
Sima amethibitishwa rasmi baada ya kupigiwa kura zote 26 za ndiyo, ambapo jana kamati ya madiwani ya chama hicho ilimchagua kwa kura 15 kati ya 26 akimbwaga mpinzani wake, Happiness Ibasa aliyepata kura 11.
Naye, Anitha Rwezaula amepitishwa kwa kura zote 26 za ndiyo kuwa Naibu Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza, ambapo jana kamati ya chama chake ilimchagua kwa kumpigia kura 14 kati ya 26 akiwashinda, Joyce Nyakiha (6), na Mariam Shamte (6).
Akizungumza wakati akiomba kura kwa madiwani, Sima amesema kipaumbele chake ni kuboresha miundombinu ya jiji hilo, kuimarisha makusanyo ya mapato ya ndani, na mikopo kwa vijana.
”Natambua tuna kazi ya kuifanya Mwanza kuwa jiji kinara, nitakuwa kiungo kati ya Serikali na wananchi. Naahidi kuwa baraza hili litakuwa la mfano na nitasimama kama Meya tukaibadilishe Mwanza kuwa ya mfano,” amesema Sima.
Hata hivyo, baada ya ahadi hizo, baadhi ya madiwani waliuliza maswali ambayo yameonyesha kutoridhishwa na hali ya miundombinu ya barabara za jiji hilo, na kutokuwa na mpango madhubuti wa kukabiliana na majitaka mvua zinaponyesha.
Diwani wa Kata ya Mirongo, Nurdini Mbaji, amehoji jiji hilo licha ya kutajwa kuwa la pili kwa ukubwa nchini lakini shughuli nyingi zinafungwa mapema na kusababisha mzunguko wa kifedha kuwa mdogo, huku huduma muhimu zikishindwa kupatikana kwa saa 24.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi (kushoto), akimkabidhi vitendea kazi, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya jiji la Mwanza, Sima Constantine Sima (kulia) baada ya kuthibitishwa na baraza la madiwani. Picha na Damian Masyenene
Naye, Chanila Mwakyoma, Diwani Kata ya Lwanhima, amesema licha ya sifa kubwa lakini limekuwa na changamoto ya kutapakaa maji taka na barabara kutopitika mvua zinaponyesha na kusababisha shughuli muhimu kusimama.
”Jiji hili liko giza hakuna taa za barabarani licha ya kujinasibu ni jiji kubwa, umejipangaje sasa kubadilisha hili na kuleta hadhi ya jiji kubwa kama Mwanza. Pia miundombinu mingi haipitiki na shughuli zinasimama mvua zinaponyesha,” amesema Mwakyoma.
Akijibu hoja hizo, Sima amekiri jiji hilo kukabiliwa na changamoto hizo, huku akiwaomba madiwani, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, na watendaji wa Serikali kumpa ushirikiano na kumuunga mkono ili kwenda kubadilisha hali hiyo.
”Lazima tukiri ni kweli mvua inaleta tabu ndiyo maana tulifanya mapinduzi kwa kutengeneza barabara za mawe, lami, na kuboresha mitaro katika baadhi ya mitaa. Tumeshanunua greda, rola na mitambo mingine ili kuongeza tija na uwajibikaji katika kuboresha miundombinu,” amesema
Kwa upande wa Makilagi amewataka madiwani hao kutambua fursa zilizopo katika jiji hilo na kuzitumia ili halmashauri ipige hatua, huku akiwahimiza kuifahamu vyema halmashauri yao ili kujua maeneo ya kuyafanyia kazi.
