Simba, Yanga zarudi mzigoni Ligi Kuu Bara

VIGOGO wa soka nchini, Simba na Yanga waliokuwa katika majukumu ya mechi za kimataifa wakishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, wanatarajiwa kurejea tena mzigoni kwenye Ligi Kuu Bara baada ya kucheza mara ya mwisho mapema mwezi uliopita na kila moja kuvuna pointi tatu kwa ushindi.

Yanga iliyopo Kundi B imetoa kupata suluhu ugenini dhidi ya JS Kabylie ya Algeria na kuifanya ifikise pointi nne baada ya mechi mbili za kundi hilo, huku watani wao wakichapika katika mechi ya pili mfululizo mbele ya Stade Malien ya Mali baada ya awali kulala 1-0 nyumbani katika Kundi D.

Lakini kwa sasa vigogo hao wanabidi kusahau matokeo hayo ya mechi za CAF kwa kujiandaa kushuka uwanjani wiki hii kucheza mechi mbili za chapuchapu kabla ya Ligi Kuu kusimama hadi mwakani kupisha Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 zinazofanyikia Morocco.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Bodi ya Ligi Kuu, timu hizo kila moja itakuwa kwenye uwanja wa nyumbani kusaka pointi tatu muhimu, Yanga ikipewa Fountain Gate na Simba ikipangiwa kuvaana na Mbeya City iliyomtimua kocha Malale Hamsini baada ya kichapo cha Namungo.

MZIGONI 01

Awali, Yanga na Simba zilikuwa zisafiri kwenda katika miji ya Mbeya na Tabora kuvaana na Tanzania Prisons na TRA United, lakini Bodi ya Ligi ilifanya mabadiliko na kuzifuta mechi hizo za ugenini na kusema ingezipangia mechi za nyumbani kwenda sawa na ratiba.

Ndipo sasa wametakiwa kushuka uwanjani Alhamisi hii dhidi ya timu hizo wakiwa nyumbani, kisha kuendelea na ratiba za wikiendi hii, ambapo Yanga itakuwa mgeni wa Coastal Union iliyofungiwa uwanja wao wa nyumbani wa Mkwakwani, Tanga na Simba kuvaana na Azam FC.

MZIGONI 03 (1)

Mechi ya Yanga na Fountain itapigwa saa 10:00 jioni ya Alhamisi kwenye Uwanja wa KMC Mwenge, wakati Simba ikiialika Mbeya City kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo kuanzia saa 1:00 usiku.

Baada ya hapo ndipo zitafuata mechi za Desemba 7 zitakazokuwa za mwisho mwa mwaka huu kupigwa ili kupisha fainali za Afcon 2025 ambazo Tanzania itashiriki ikiwa ni mara ya nne tangu Uhuru wa nchi na michuano yenyewe itaanza Desemba 21 hadi Januari 18 mwakani.

Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi, Karim Boimanda amesema wamesogeza mechi mbele ili kutoa nafasi ya mapumziko kwa timu hizo ambazo zilikuwa ugenini katika mechi ya pili hatua ya makundi.

MZIGONI 03

“Ni kweli ratiba ya mechi imebadilishwa na tulitoa sababu kuwa kutakuwa na mabadiliko kutokana na ratiba ngumu kwa timu zetu zinazoiwakilisha Tanzania kimataifa,” amesema Boimanda na kuongeza;

“Yanga imewasili jana (juzi) ikitokea Algeria na Simba kesho (leo) ikitokea Mali, hivyo tumeamua kuzipa siku mbili za mapumziko kabla ya kuendelea kuchanga karata za Ligi Kuu.”

MZIGONI 02

Kabla ya mechi ya jana kati ya Mashujaa na Coastal Union, msimamo ulikuwa unaonyesha Yanga imecheza mechi nne ikikusanya pointi 10 baada ya kushinda tatu na kutoka sare moja ikiwa nafasi ya tano, wakati Simba ilikuwa nafasi ya saba ikivuna pointi tisa ikishuka uwanjani mara tatu na kushinda zote, huku JKT Tanzania ikiwa ndio kinara kwa kusanya pointi 16.