Mwanariadha wa kimataifa wa Tanzania kutoka Jeshi la Wananchi (JWTZ), Staff Sajenti Alphonce Simbu, amerejea nchini leo Desemba 2, 2025 akitokea jijini Monaco, Ufaransa, ambako alishiriki kuwania tuzo za mwanariadha bora wa mwaka 2025 katika kipengele cha mbio za nje ya uwanja.
Tuzo hizo zilifanyika Novemba 30, 2025, zilimshindanisha Simbu na Mkenya Sebastian Sawe, baada ya wote kuingia fainali kutokana na matokeo yao makubwa katika majukwaa ya kimataifa.
Simbu aliingia fainali kwenye orodha hiyo kutokana na mafanikio makubwa aliyopata mwaka huu 2025, ikiwemo kutwaa medali ya dhahabu ya mbio za marathoni za dunia yaliyofanyika Tokyo, Japan, mwezi Septemba na kuwa Mtanzania wa kwanza kushinda medali hiyo tangu nchi ilipoanza kushiriki mashindano hayo mwaka 1983. Ushindi huo uliibua matumaini na faraja kubwa kwa wadau wa riadha hapa nyumbani.
Hata hivyo, licha ya mafanikio hayo, tuzo hiyo haikwenda kwake, bali ilitwaliwa na Sawe kutoka Kenya, lakini pamoja na hilo, kurejea kwa Simbu kumepokelewa kwa heshima kubwa kutokana na hadhi aliyoipa nchi katika jukwaa la dunia, na namna aliyoendelea kuonesha ubora katika mbio ndefu za kimataifa.
Akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) akitokea Monaco, Simbu amewashukuru Watanzania kwa sapoti yao kubwa, hususan kura walizompigia na uungwaji mkono anaoupata kutoka serikali na taasisi mbalimbali.
“Nawashukuru Watanzania kwa sapoti yao, serikali, Baraza la Michezo la Taifa (BMT), kwa sababu katika hatua hii huwezi kusimama mwenye lazima utashikwa mkono.
“Naishukuru taasisi ninayoifanyia kazi Jeshi la Wananchi wa Tanzania kupitia Mkuu wa Majeshi kwa kuendelea kunipa sapoti katika kuiwakilisha nchi kimataifa,” amesema Simbu.
Ameongeza kwamba, anajivunia kuwa Mtanzania wa kwanza kufika hatua ya juu ya tuzo hizo zinazotolewa na Shirikisho la Riadha la Dunia (WA), na anaamini siku moja ataibuka mshindi kutokana na kiwango anachoedelea kuonyesha.
Kutokana na mafanikio hayo, wadau wa michezo na sekta binafsi wameendelea kumpongeza ambapo mkurugenzi wa hoteli za Makunduchi Village, Mohammed Haji maarufu kama Boss Mo, amesema Simbu ni hazina ya taifa na anatangaza nchi kimataifa kupitia michezo.
Kwa upande wake, Prisila Simfukwe, mkurugenzi wa kampuni ya Take Mwanzo, amesema wataendelea kumsapoti Simbu katika juhudi zake za kuipeleka Tanzania mbali kupitia riadha sambamba na kuunga mkono juhuzi za serikali zinazolenga kukuza michezo kitaifa.
Naye Moses Simon, mkurugenzi wa kampuni ya Ntua Communications Ltd inayosimamia chapa ya Simbu, amesema wanatamani kuona mwanariadha huyo akiipeperusha bendera ya Tanzania kimataifa si tu kwa michezo bali pia katika utalii.
