Baada ya kula kiapo, madiwani wa Halmashauri ya Mtama wamemchagua Diwani wa Kata ya Nyengedi, Yusuph Tipu, kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, huku Diwani wa Kata ya Mtama akichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti.
Tipu ameshinda kwa kupata kura zote 28 kutoka kwa madiwani waliohudhuria, akichaguliwa kwa mara ya pili kuongoza halmashauri hiyo.
Baada ya kupitishwa leo Jumanne, Desemba 2, 2025, katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Mtama na Tipu amewataka madiwani kushirikiana na viongozi wa idara ili kuendeleza maendeleo.
Amesema kuwa uongozi wake wa awali uliiweza kuifikisha Halmashauri hatua nzuri, na katika kipindi hiki kingine cha miaka mitano ataendelea kutoka pale alipoishia ili kufanikisha maendeleo zaidi.
Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye, amewataka madiwani na watendaji kuwa wazalendo, kuhakikisha utoaji wa huduma bora, na kutumia lugha nzuri wanapohudumia wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Lindi Victoria Mwanziva akizungumza na madiwani mara baada ya kumaliza mchakato wa kumpigia kura Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mtama.
Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Victoria Mwanziva, amesisitiza umuhimu wa usimamizi wa miradi ya maendeleo, mapato ya halmashauri na kuepuka migogoro isiyo na tija.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mtama, Anderson Msumba amesema halmashauri imetenga Sh500 milioni kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa maduka, vibanda vya mama lishe katika stendi ya mabasi, utoaji wa mbegu kwa wakulima, pamoja na kuwapatia vijana wa bodaboda leseni ili kuwawezesha kufanya kazi zao kisheria.
