WAKATI Ligi ya Kikapu Taifa (NBL), ikiendelea mjini Dodoma kuna ushindani wa mastaa hasa wale wanaocheza Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL).
Nyota hao waliosajiliwa na timu za mikoa mbalimbali kutokana na zile wanazozichezea kukosa nafasi ya kushiriki NBL, wamekuwa wakionyesha ushindani kama ilivyo BDL kwenye Uwanja wa Chinangali.
Baadhi ya wachezaji hao ni Junior Louissi, Lerry Mve na Joseph Kamamba waliotokea Srelio ambao kule Dodoma wamesajiliwa na Kisasa Heroes ya mjini humo.
Vilevile wapo mastaa wa Stein Warriors ambao Evance Davies na Felix Luhamba wanaoichezea Planet ya Mwanza, Victor Michael wa Vijana (City Bulls) anayeichezea Dom Spurs ya Dodoma.
Wengine ni Jonas Mushi, Sisco Ngaiza, Tyrone Edward (Stein Warriors) na Solo Geofrey (Pazi) ambao wanaichezea UDSM Outsiders ya Dar; Josephati Petar anaitumikia Pazi ilhali katika NBL anaichezea JKT ya Dar pamoja na Swalehe Baruani (Dar City) anayekipiga katika kikosi cha Dom Spurs cha Dodoma.
Nyota wa timu za wanawake Dar nao wapo nyuma kwani kuna Anamary Cyprian na Witness Mapunda wanaoichezea Jeshi Stars pamoja na Dina Mussa wa Ukonga Queens ambao kwa pamoja wanakitumikia kikosi cha Fox Divas cha Mara, Noela Uwendameno wa Jeshi Stars anayeichezea JKT Stars (Dar), Jesca Lenga na Irene Gerwin wa DB Troncatti wanaichezea DB Lioness. Bingwa mtetezi wa NBL upande wa wanaume ni Dar City ya Dar es Salaam na kwa wanawake ni Fox Divas ya Mara.
DAR CITY YAONYESHA UKUBWA
Licha ya Dar City kumpumzisha nyota wake walioshiriki mashindano ya Road to BAL Elite 16, imedhihirisha ubora katika Ligi ya Kikapu Taifa (NBL).
Timu hiyo inayonolewa na kocha Mohamed Mbwana iliwapumzisha nyota wake ambao ni Nisre Zouzoua (Marekani), Solo Diabate (Ivory Coast), Deng Angok (Sudan ya Kusini) na Raphiael Putney (Marekani).
Wachezaji waliobaki Hasheem Thabeet, Ally Abdallah, Fotius Ngaiza na Haji Mbegu wanashirikiana na baadhi ya wachezaji wengine waliowasajili katika ligi hiyo akiwepo Clinton Best kutoka nchi ya Nigeria.
Akizungumza Mwanaspoti kwa simu kutoka Dodoma, meneja wa Dar City, Simon Joe amesema wamejipanga vizuri kutetea ubingwa.
“Sisi tuko vizuri na kadri ligi inavyoendelea tumekuwa tukibadilika. Licha ya timu zingine kutukamia ubora wa wachezaji ndiyo unaoleta majibu,” amesema Joe.
Katika mchezo wa kwanza Dar City iliishinda Dom Spurs kwa pointi 53-45, ikaifunga Pamoja BBC kutoka Arusha kwa pointi 104-47. Michezo mingine iliifumua Planet ya Mwanza kwa pointi 106-45, ikaifunga Kisasa Heroes (Dodoma) kwa pointi 74-62.
KIKAPU TAIFA YATOA UZOEFU
Kocha mkuu wa Bright Queen ya Dodoma, Zacharia Vitalis amesema ugeni NBL ndiyo uliwafanya wapoteze mechi.
Hata hivyo, amesema licha ya ugeni wachezaji wao wamepata uzoefu na lengo limetimia.
“Tumecheza na timu iliyosajili wachezaji wazoefu kutoka nje ya nchi. Kwa kweli tumejifunza vitu vingi kupitia kwa wachezaji hao,” amesema Vitalis.
Kwa mujibu wa Vitalis katika mashindano waliwakosa nyota wao baada ya kutopewa ruhusa na waajiri wao.
Katika mchezo wa kwanza wa timu hiyo ilifungwa na Fox Divas kwa pointi 116-22 na JKT Queens 76-43.
Ligi hiyo inashirikisha timu 20 kati ya hizo 12 zikiwa za wanaume na nane za wanawake, huku za wanaume zikiwa zimegawanywa katika makundi mawili.
Kundi A lina Dar City (DSM), Kisasa Heroes (Dodoma), BBC (Arusha), Young Warriors (Morogoro), Mbeya Flame (Mbeya) na Manyara. Kundi B kuna UDSM Outsiders (DSM), JKT BBC (DSM), Dodoma Spurs (Dodoma), Planet BBC (Mwanza), Home Boys (Rukwa) na Wavuja Jasho BBC (Kigoma).
Kwa upande wa wanawake ni Fox Divas (Mara), DB Lioness (DSM), JKT Queens (DSM), Vijana Queens (DSM), Mbeya Frame Queens (Mbeya), Bright Queens (Dodoma) na Orkeeswa (Arusha).
VIJANA QUEENS YAZINDUKIA DODOMA
Baada ya Vijana Queens kufanya vibaya katika mashindano mbalimbali ya mchezo huo, imeweza kuzinduka NBL.
Timu hiyo iliondokewa na nyota wake waliojiunga na Tausi Royals na Jeshi Stars na baada ya hapo iliwapandisha wale wa kikosi cha pili.
Hata hivyo, licha ya kuwapandisha wachezaji hao haikufanya vizuri katika NBL mwaka jana pamoja na Ligi ya Wanawak Mkoa wa Dar es Salaam (WBDL).
Katika michezo iliyocheza iliishinda DB Lioness (DSM) kwa pointi 59-31, JKT Stars (DSM) pointi 70-62, Orkeeswa (Arusha) pointi 48-27 na Bright Queens (Dodoma) kwa pointi 75-25.
TANO ZASHINDWA KUSHIRIKI NBL
Ukata umesababisha timu tano zishindwe kushiriki Ligi ya Taifa ya Kikapu, mwaka huu.
Timu hizo ni Kisasa (Shinyanga), Centre (Tabora), DB Troncatti (Dar), Deep Sea na Tanga United Queens za Tanga.
Kamishna wa Ufundi na Mashindano wa Ligi ya kikapu Mkoa wa Shinyanga, George Simba amesema licha Risasi kuahidiwa kupewa fedha na wadhamini waliowaomba, lakini walishindwa kutekelezewa ahadi hiyo.
Mmoja wa waratibu wa Ligi ya Kikapu Mkoa Tabora, Abrose Kitalika amesema Center ilishindwa kwenda Dodoma kutokana na kukosa fedha za maandalizi.
