Video: Rais Samia Atoa Onyo Kali Dhidi ya Wachochezi wa Amani ya Taifa



Akizungumza katika Mkutano na Wazee wa Dar es Salaam, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amelaani vikali vurugu zilizotokea Oktoba 29 na 30, akisisitiza kuwa matukio hayo hayalingani na misingi, utu, wala utamaduni wa Watanzania.

Dkt. Samia amesema kuwa kila aliyeathirika katika vurugu hizo iwe ni kuumia au kupoteza maisha ni Mtanzania ambaye ana haki na thamani sawa na mwingine yeyote.

“Kila aliyeumia au kupoteza maisha ni Mtanzania mwenzetu, mwenye haki sawa na mwingine. Hakuna mtu aliye juu ya mwingine. Haki ya kuishi na haki ya kuwa huru ni tunu zetu wote Watanzania, kwa hiyo hakuna sababu ya kuumizana au kunyimana uhuru,” amesema Rais Samia.

Ameeleza kuwa ni jambo la kusikitisha kuona baadhi ya watu wakipanga na kuratibu fujo kwa maslahi yao binafsi ya kisiasa, huku wakijaribu kuwafanya Watanzania wenzao kuwa kafara.

Dkt. Samia ametoa wito kwa wananchi kuendelea kulinda amani, utulivu na mshikamano ambao umekuwa nguzo muhimu ya taifa, akiongeza kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua dhidi ya wote watakaohatarisha usalama wa nchi.