Dodoma. Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dodoma, imewaachia huru washtakiwa sita, wakiwamo waganga wa jadi, walioshtakiwa kwa mauaji na kuchukua sehemu ya viungo ili kutengeneza dawa ya utajiri.
Miongoni mwa walioshtakiwa ni mshtakiwa wa sita, Oscar Labani, ambaye upande wa Jamhuri ulidai ndiye mteja wa dawa ya kumfanya awe tajiri, ambayo mchanganyiko wake ulihitaji viungo vya binadamu.
Mwili wa mwanamume ambaye hakutambulika ulipatikana Machi 3, 2023 kwenye njia ya reli katika Mtaa wa Mlewa wilayani Manyoni, mkoani Singida. Kichwa na mguu wa kushoto vilitenganishwa na kiwiliwili na haukuwa na uume.
Walioachiwa huru katika hukumu iliyotolewa Novemba 28, 2025 na Jaji Evaristo Longopa na nakala kupakiwa kwenye tovuti ya mahakama leo Desemba 2, 2025 ni Othman Kalinga, ambaye ni mganga wa jadi aliyekuwa mshtakiwa wa kwanza.
Wengine ni Shaban Rajabu (dereva wa bodaboda), Omary Jumanne (mganga wa jadi), Hamim Athman (mwanafunzi wa uganga), Salum Zacharia (mpigapicha na msaidizi wa mganga) na Oscar Labani.
Jaji Longopa katika hukumu amesema hakuna ubishi kuwa kulitokea kifo cha mtu asiyefahamika, lakini ushahidi wa Jamhuri hauonyeshi kuunga mkono nadharia ya mauaji na huenda kifo chake kilitokana na kugongwa na treni.
“Hakuna shahidi hata mmoja wa Jamhuri aliyeweza kujenga ushahidi kuwa alimuona mshtakiwa yeyote akimuua mtu huyo. Ushahidi unaonyesha mwili ulikutwa katika njia ya reli ukiwa umetenganishwa kichwa na mguu,” amesema.
Jaji amesema: “Jamhuri ilijaribu kuonyesha kama vile kuna kitu butu kizito kilitumika, lakini hakuna kitu hicho kilitolewa mahakamani kama kielelezo. Ushahidi wa Jamhuri umeacha mashaka kuwa pengine hakuuawa bali aligongwa na treni.”
“Shahidi namba 1, 2, 4 na 5 walikuwa na jambo linalofanana. Hawa mashahidi wanne kuna wakati walikuwa wanauelezea mwili wa marehemu kama wa mtu aliyegongwa na treni. Ushahidi huu unaacha mashaka mengi,” amesema.
Jaji Longopa amesema: “Kukosekana kwa ushahidi unaothibitisha kuwa kuna kitu butu kizito kilitumika kusababisha kifo na mazingira ya namna mwili ulivyokutwa, unafanya kusiwe na sababu yoyote ya kutoamini kwamba huenda aligongwa na treni.”
Amesema amepitia ushahidi wote na unakosa nguvu kuonyesha kuwa washtakiwa kuna muda walikutana, kupanga na kuwa na dhamira moja ya kusababisha kifo cha mtu huyo ambaye jina wala makazi yake hayakufahamika.
“Hakuna ushahidi kuwa washtakiwa hawa sita ama walihusika moja kwa moja au katika njia moja au nyingine na kusababisha kifo hicho. Hisia peke yake haiwezi kuwatia hatiani kwa kosa kubwa kama hilo,” amesema.
Amesema inachokiona mahakama ni kuwa, upande wa mashtaka uliegemea zaidi katika maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa kwanza, ambayo hata hivyo hayakupokewa mahakamani kama kielelezo kwa sababu ya dosari za kisheria.
Jaji Longopa amesema kesi hiyo ni moja kati ya ambazo uchunguzi wa kisayansi wa vinasaba (DNA) ungesaidia kutegua kitendawili, lakini hata nguo na vifaa vingine vilivyokamatwa kwa washtakiwa havikufanyiwa DNA.
“Kupuuza kwa upande wa mashtaka kutumia uchunguzi wa kisayansi kuthibitisha ugumu wa kosa hili na badala yake kubakia na ushahidi wa hisia peke yake hauwezi kuthibitisha shtaka zito kama la mauaji,” amesema.
Jaji amesema: “Kushindwa kutumia utaalamu wa kisayansi kubainisha uhusiano kati ya kifo na washtakiwa kuna madhara makubwa kwa upande wa mashtaka ambayo ni kushindwa kuthibitisha kesi kwa kiwango kinachotakiwa.”
“Ushahidi uliopo katika kumbukumbu umeshindwa kuwaunganisha washtakiwa na kifo hicho. Hakuna chochote kinachoonyesha washtakiwa ndio ambao walishiriki kusababisha kifo hicho na walikuwa na dhamira ovu,” amesema.
Katika mazingira hayo, Jaji Longopa amesema upande wa mashtaka umeshindwa vibaya kuwaunganisha washtakiwa na kifo hicho na hakuna ushahidi wowote wa kuwaunganisha washtakiwa ambao ni raia wa kawaida na kifo hicho.
Shahidi muhimu alikuwa mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai wilaya (OC-CID), Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Peter Makala, aliyeeleza kuwa Machi 3, 2023 saa 12:00 asubuhi, alipata taarifa ya uwepo wa mwili wa mwanamume asiyefahamika.
Alifika eneo la tukio akaona kichwa na mguu wa kushoto vikiwa vimetenganishwa na kiwiliwili, vikiwa pande mbili tofauti za njia ya reli.
Aliona michirizi ya damu kama vile mwili uliburuzwa kutoka kibanda cha mamalishe.
Shahidi huyo alieleza ingawa ilionekana kama amegongwa na treni, lakini alishuku ni mauaji ya kukusudia kutokana na kuwapo matone ya damu na mazingira kuwa mwili uliburuzwa hadi eneo hilo.
Katika kuuchunguza mwili huo, ilionekana kama umekatwa na wauaji kuondokana nao. Mwili ulipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Manyoni na kubaini kifo chake kilitokana na kupigwa na kitu kizito ambacho ni butu.
Katika ushahidi, Machi 23, 2023, alidai alipata taarifa kuwa waliofanya mauaji hayo ni waganga wa jadi aliodai ni Othman Kalinga akishirikiana na Hamim Athman na Shaban Rajabu, wakazi wa Tambukareli.
Alidai siku hiyo waliwakamata Hamimu na Shaban, lakini mshtakiwa wa kwanza, Othman Kalinga hakuwapo nyumbani, huku nyumba yake ikiwa imefungwa. Wawili hao waliwajulisha polisi kuwa Kalinga amesafiri kwenda Sikonge.
Polisi walikwenda Sikonge mkoani Tabora ambako walimkamata Kalinga na kumrudisha Kituo cha Polisi Manyoni.
Siku iliyofuata walikwenda kufanya upekuzi nyumbani kwa Kalinga na kupata vifaa anavyovitumia kwa tiba asilia.
Makala alidai ofisa mwenye cheo cha Sajini aitwaye Emmanuel alimuhoji Kalinga akakiri kushiriki katika kosa hilo, akawataja washirika wenzake, akiwamo pia mteja wake.
Kwa mujibu wa kachero huyo, mteja wa mganga alihitaji matambiko kwa ajili ya kupata utajiri, hivyo matumizi ya viungo vya mwili wa binadamu yalihitajika. Alidai washirika wa mganga walikiri kushiriki kuandaa dawa hiyo.
Shahidi wa pili, Mary Kanani ambaye ni mjasiriamali, alidai siku ya tukio alikwenda kuokota kuni jirani na kibanda chake cha biashara ambako aliona matone ya damu na aliwajulisha polisi waliofika eneo hilo.
Shahidi wa tatu, Kassim Makingo alieleza namna alivyoshuhudia upekuzi nyumbani kwa mshtakiwa wa kwanza, huku shahidi wa nne, Charles Fabian alitoa ushahidi wa namna alivyoufanyia uchunguzi mwili wa marehemu.
Shahidi wa tano, Sajini Emmanuel alieleza namna alivyoshiriki ukamataji wa baadhi ya washitakiwa, akiwamo Kalinga. Alieleza yeye ndiye aliandika maelezo yake na washtakiwa wengine, ambao wao walikana kuhusika na mauaji hayo.
Katika utetezi wao, Kalinga alikiri kuwa mganga wa jadi mwenye ofisi Itigi, Sikonge na Dar es Salaam. Alieleza anamfahamu Hamimu kama msaidizi wake na Shaban Mussa kama bodaboda ambaye amekuwa akimbeba.
Alieleza namna alivyokamatwa na Polisi na kurejeshwa Itigi na nyumba yake ilivyofanyiwa upekuzi. Alikana kuandika maelezo ya onyo polisi na kuhusika na mauaji. Akaomba mahakama imwachie huru.
Washtakiwa wengine wote walikana kuhusika na mauaji, huku wa sita, Labani akisema mashtaka ya mauaji dhidi yake hayana msingi na wala hamfahamu Kalinga wala washtakiwa wengine ambao alishtakiwa nao.
