Dar es Salaam. Katika kuunga mkono jitihada za malezi na ustawi wa watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu, Benki ya Absa imekabidhi msaada wa mahitaji muhimu yatakayo wasaidia kujikimu kimaisha.
Taasisi hiyo imeunga juhudi hizo kwa kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali ikiwemo vyakula, sabuni, vinywaji na mashine nne za cherehani kwa kituo cha kulelea watoto yatima cha Raya Islamic Orphanage Centre kilichopo kijiji cha Lugono, wilayani Mvomero mkoani Morogoro.
Msaada huo ni sehemu ya programu endelevu ya benki hiyo na wafanyakazi wake ya kurudisha fadhila kwa jamii kwa kutembelea na kusaidia vituo vinavyolea watoto yatima na walio katika mazingira hatarishi.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo jana Jumatatu, Desemba 1, 2025 Meneja wa Tawi la Absa mkoani Morogoro, Godfrey Chilewa, amesema benki hiyo imejikita katika kupunguza changamoto zinazovikabili vituo vya malezi nchini.
“Watoto yatima wana uhitaji sawa wa malezi kama watoto wengine. Sisi Absa tunasema stori yako ina thamani, na tunatambua kuwa hadithi zao pia zina thamani. Tunaamini misaada kama hii inachangia kujenga mustakabali bora kwao,” amesema Chilewa.
Ameongeza ustawi wa watoto hao unahitaji nguvu ya pamoja kati ya Serikali, taasisi binafsi na jamii kwa ujumla, sambamba na dhima ya Absa ya kuiwezesha Afrika na Tanzania ya kesho, hatua moja baada ya nyingine.
Kwa upande wake, Saidi Hamis (27), mmoja wa vijana waliokulia kituoni hapo, amesema kituo hicho kinawalea watoto 113 wavulana 66 na wasichana 47ambao wengi wao wanatoka katika familia zenye changamoto za kijamii.
Amesema kuwa kituo kilianzishwa mwaka 2013 eneo la Mindu kabla ya kuhamia Lugono na kwa sasa kinakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa uzio.
“Kutokuwa na uzio kunatuweka hatarini kuvamiwa na wanyama, ikiwemo tembo kutoka Hifadhi ya Taifa ya Mikumi. Tunaomba jamii ituunge mkono kukamilisha ujenzi wa uzio ili watoto wawe salama,” amesema.
Naye Karamelo Kizilahabi (17), mmoja wa watoto wanaolelewa kituoni hapo, amesema mashine za cherehani walizopokea zitawasaidia kujifunza ufundi wa kushona ikiwa ni hatua muhimu ya kuwawezesha kujitegemea wanapokomaa.
“Cherehani hizi zitatujengea ujuzi na kutusaidia baadaye kujipatia kipato. Tunawashukuru kwa kutukumbuka na tunawaombea waendelee kuwa na moyo huu,” amesema.
Amesema msaada huo umetajwa kuwa mkombozi kwa kituo hicho na hatua muhimu katika kuboresha mazingira ya malezi na elimu kwa watoto wanaolelewa hapo.
