KIUNGO mkongwe wa Simba na Yanga, Hassan Dilunga ameweka siri inayomfanya kusalia ndani ya kikosi cha JKT Tanzania kwa muda mrefu, huku akimtaja kocha Hamad Ally.
Mkongwe huyo huu ni msimu wa tatu ndani ya JKT, tangu alipoagana na Simba aliyoitumikia kwa miaka mitatu mfululizo baada ya kutoka Yanga.
Dilunga alisema, licha ya kwamba anapokea ofa mbali mbali, lakini bado ameamua kusalia JKT kwa sababu kwake yeye ile sio timu tu bali ni familia.
“Kwanza mimi ndio wamenilea kwa sababu nilivyotoka tu mtaani nikatua zangu, Ruvu Shooting ambapo ni kurwa na dotto na hii JKT, kwa hiyo kusalia hapa misimu mitatu najihisi kama niko nyumbani.
Aidha, alisema kocha Hamad anayekinoa kikosi hicho kwa sasa amemsaidia sana, yeye kama mchezaji kutoka kwenye uchezaji wa zamani mpaka wa kisasa.
“Ni kocha ambaye anafundisha soka la kisasa, siwasemi wengine ila yeye ana mambo mengi sio uwanjani tu hadi darasani, ndio maana unaona JKT ina mpira f’lani hivi wa tofauti.
“Hii inatusaidia sisi wachezaji kufanya majukumu yetu, kuna muda uwanjani unacheza kila eneo mengine sio yako, ila kupitia yeye kuna kitu kimeongezeka, ubora wake umeonekana mpaka ameitwa timu ya Taifa.”
Dilunga katika mechi tisa ilizocheza JKT Tanzania, amecheza saba na moja dhidi ya Fountain Gate akianzia benchini na nyingine moja hakuwapo kabisa, hivyo amefikisha jumla ya dakika 433 za uwanjani.
JKT Tanzania kwa sasa ndio vinara wa ligi, ikiwa imecheza mechi tisa, ikishinda nne, sare nne na kupoteza mchezo mmoja na kufikisha pointi 16.