Dk Kijaji ataka tafiti za kisayansi kutatua changamoto uhifadhi

Arusha. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji, amesisitiza umuhimu wa tafiti za kisayansi kuwa chanzo cha sera, elimu kwa jamii, ubunifu kwa uhifadhi na suluhisho la changamoto zinazokabili maeneo yaliyohifadhiwa.

Ametaja baadhi ya changamoto kuwa ni migogoro kati ya wanyama na binadamu, mimea vamizi, ongezeko la watu na magonjwa mapya.

Amesema Serikali kwa kutambua kwa kina umuhimu wa uhifadhi kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya  2050 miongoni mwa nguzo muhimu itakayoangalia kwenye sayansi ni pamoja na uhimilivu wa mazingira dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Hayo yamesemwa leo Desemba 3, 2025 na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya  Maliasili na Utalii anayeshughulikia masuala ya utalii, Nkoba Mabula  kwa niaba ya Dk Kijaji katika kongamano la 15 la Kimataifa la Kisayansi lililoandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzana (Tawiri).

Amesema ni muhimu mamlaka za uhifadhi na wadau mbalimbali kutumia matokeo ya tafiti kuboresha uhifadhi, kuongeza ufanisi wa utalii na kunufaisha jamii na Taifa kwa ujumla.

Amesema Tanzania imetenga eneo lake zaidi ya asilimia 32.5 kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori na asilimia 80 ya utalii nchini unategemea wanyamapori, sekta ambayo inachangia pato ya Taifa kwa asilimia 21.

Amesisitiza uhifadhi wa wanyamapori ni suala lisilopaswa kupuuzwa na badala yake kupewa kipaumbele na kuwa bunifu na teknolojia zitakazotokana na tafiti mbalimbali zitakazosaidia kulinda mustakabali wa uhifadhi na utalii kwa ujumla.

“Mkutano huu ni jukwaa muhimu kwa kuwasilisha matokeo ya tafiti, kubadilishana uzoefu, na kuwaunganisha watafiti na watunga sera. Naomba tafiti zenu ziwe chanzo cha sera, elimu kwa jamii, ubunifu kwa uhifadhi, na suluhisho la changamoto zinazotukabili,”amesema na kuongeza.

“Ninaziomba mamlaka za uhifadhi na wadau wote kutumia matokeo ya tafiti kuboresha uhifadhi, kuongeza ufanisi wa utalii na kunufaisha jamii, hasa katika kipindi hiki ambacho tunakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ongezeko la watu, migongano kati ya binadamu na wanyamapori, mabadiliko ya tabianchi na mimea vamizi,”amesema.

Mkurugenzi Mkuu wa Tawiri, Dk Eblate Mjingo amesema kuwa kongamano hilo la siku tatu limekutanisha wanasayansi zaidi ya 500 kutoka nchi mbalimbali.

Amesema kongamano hilo linaongozwa na kauli mbiu isemayo ‘ubunifu katika uhifadhi wa wanyamapori na utalii endelevu’, ambapo kutawasilishwa matokeo ya tafiti zilizofanywa na Tawiri na wadau wengine.

“Ninawasihi washiriki wenzangu  kutumia kongamano hili kama kichocheo cha mikakati mipya na bunifu zitakazosaidia kulinda urithi wa maliasili ya Tanzania kwa vizazi vijavyo.”

“Kongamano mwaka huu ni tofauti kwani linaangalia ubunifu na matumizi ya teknolojia, tumekuwa tukifanya uhifadhi kwa kutumia njia zilizokuwepo ila sasa hivi changamoto ni kubwa na zinakuja zikiwa na mambo mengi pamoja kwani tusipofanya hivyo sasa tutachelewa,”amesema.

Mmoja wa wadau hao, Profesa Noah Sitati ambaye ni msimamizi wa miradi ya Shirika la World Wildlife Fund (WWF) katika nchi za Kenya na Tanzania (Southern Kenya,Northern Tanzania), amesema kuwa tafiti ni muhimu katika kukuza sekta ya utalii nchini.