Elimu si uvumbuzi, bali uvumbuzi ni elimu

Leo namkumbuka mwamba wa kuitwa Abunuwasi. Kwa taarifa tulizonazo jamaa alikimbia umande, lakini alikuwa na akili zaidi ya mchwa. Alichemsha vichwa vya wanazuoni na wanasheria kwa mawazo yake mapya wakati wa mijadala na hukumu za mashauri mbalimbali. Katika moja ya vituko vyake, alitumia hesabu ndefu katika mchanganuo wa kutekeleza hukumu dhidi ya baba mkwe wake, Mfalme wa Baghdad.

Kisa kilianza kwa baba mkwe huyu kuota mali zikiwa chini ya nyumba ya Abunuwasi. Kwa mamlaka aliyokuwa nayo, alisimamia kundi la watu kufukua misingi ya nyumba ili kuzitoa mali zile. Lakini hawakupata chochote, hata hivyo waliiacha nyumba ikipoteza ubora na unadhifu wake. Kitendo hiki kilimuudhi sana Abunuwasi, akaapa kulipiza kisasi.

Abunuwasi alianza mpango wa kulipa kisasi kwa kupika chakula kitamu, akakifunika na kuyaacha masufuria chini ya meza. Akafunga mlango na kuuweka ufunguo chini ya zulia la mlangoni. Akaenda kwenye kijiwe cha wacheza bao na zumna kutoa onyo: “Msiende kuchukua ufunguo chini ya zulia, mkala chakula changu chini ya meza, halafu mkayaacha masufuria bila kuyafunika”.

Mara alipoondoka wale watu wakajiuliza sababu iliyomfanya atoe angalizo lile. Ilikuwa kama aliyewatuma, hivyo baada ya kujadiliana kwa muda wakaona bora kujaribu bahati yao. Wakaenda kuchukua ufunguo, wakaingia na kukuta kweli kuna biriyani chini ya meza. Wakalila hadi wakasaza, mwisho wakayaacha masufuria pasi na kuyafunika. Hapo hatua ya kwanza ikawa imekamilika.

Mwamba aliporudi akakuta yametimia. Chakula kimeliwa na sufuria zimeachwa wazi. Kitu alichofanikiwa ni kukuta nzi wakisherehekea makombo. Basi akawanasa kwa kufunika masufuria, na akawapeleka kuwastaki kwa baba mkwe (Mfalme). Mfalme hakuwa na hukumu zaidi ya kumpa Abunuwasi kibali cha kuwasaka na kuwateketeza wevi wake. Hatua ya pili ikawa imetiki.

Haraka mwamba akaenda kwa fundi kuchonga rungu. Kutoka siku hiyo alishinda akicheza bao kwa Mfalme hadi lengo lilipotimia. Nzi alitua juu ya ualaza wa Mfalme, Abunuwasi akajikunja kama mkizi na kumtwisha rungu zito. Mfalme alipiga yowe la maumivu, na Abunuwasi akakamatwa wakati akisherehekea kumuua nzi. Lakini aliachiwa huru baada ya kuonyesha kile kibali chenye saini ya Mfalme mwenyewe.

Vituko vya Abunuwasi vilifundishwa kwenye vyuo vya elimu ya juu. Hadithi zake hazitofautiani na za wavumbuzi maarufu waliowahi kufanya makubwa hapa duniani. Kwa hali ya kawaida, ilikuwa ngumu sana kuelewa falsafa za Abunuwasi kama zilivyokuwa falsafa za Galileo. Huyu alisema jua lilikuwa katikati ya sayari zote. Alijikuta akiadhibiwa kwa kifungo cha nyumbani kwa kosa la upotoshaji.

Mwanafalsafa ni nani? Hata wanafalsafa wenyewe hawajui jibu la swali hilo. Lakini wanatajwa kuwa na uwezo wa kufikiria nje ya boksi. Ni watu wanaoweza kufundisha mambo yaliyo tofauti kabisa na maisha ya kila siku. Walimu, wanazuoni na viongozi wa umma hawakuweza kukubaliana nao, kwa sababu walikwenda tofauti kabisa na mafundisho ya kiulimwengu.

Kwa mfano ile dhana ya “dunia duara” ilichanganya wengi sana. Umma ulifundishwa kuwa dunia ipo bapa kama meza, lakini Giordano akaja kitofauti. Huyu jamaa alichomwa moto kwa mafundisho yake mengine yaliyotafsirika kuwa kufuru. Katika wakati wao, viongozi wa dini ndio walioziongoza mamlaka, hivyo ilikuwa rahisi kumchukulia hatua kali mvumbuzi aliyekwenda tofauti na imani zao.

Itakumbukwa wasanii wa kale walizuiwa kufanya kazi zao binafsi. Walilazimishwa na wafalme kuchonga, kufinyanga na na kuchora miungu iliyoabudiwa na watu kwa hiyari au lazima. Wachongaji wakahofiwa kuwa wangeachwa kutumia akili zao wenyewe, aidha wangepeleka mawazo mapya kwenye jamii, au wapinzani wa utawala wangewatumia vibaya kwa kuanzisha mawazo kinzani.

Kwa muda mrefu vijana wa Kitanzania wameishi na bunifu zao vichwani mwao. Hawakuwa na jukwaa la kuzionesha kwa umma. Tatizo kubwa lilikuwa ni ithibati, kwamba mawazo yao hayakuthibitishwa kupitia mitaala yetu. Kuna vijana walikuwa mahiri kwa ubunifu wa vituo vya redio, lakini hawakuthibitishwa na TCRA ya enzi zao. Wengine walitengeneza bunduki zilizokosa ithibati ya vyombo vya usalama.

Haya pia yaliwakuta wazee wetu wa Iringa au Morogoro walioweza kufua umeme kwenye maporomoko ya maji asilia. Pia, nilipata kusikia ati kwenye maonesho ya ufundi na teknolojia Mkoani Mbeya, vijana wawili walipeleka ubunifu wao wa kutengeneza mvua. Inasemekana waliihifadhi mvua kwenye mfuko, walipoufunua mvua ikanya! Lakini nao walikwamishwa na ithibati.   

Umefika wakati wa kuyasikiliza mawazo yaliyo nje ya uzio. Mbona Wachina walikuja na mvua ya kutengenezwa kwa kukusanya mawingu na wakasikilizwa? Au baada ya kuipinga tiba asilia kwa muda mrefu, mbona sasa inakubalika kwenye Hospitali za Serikali? Wasikilizwe bunifu zao hata kama hazitaeleweka kwa urahisi. Kwani akina Isaack Newton walieleweka?

Tukumbuke kuwa wavumbuzi wengi hawakuhitimu popote, bali vumbuzi zao ndizo zilizopelekwa madarasani. Kwa mfano huyu aliyekuwa akipunga upepo ufukweni mwa bahari. Alitazama kwa upeo wa macho yake, pale bahari ilipoonekana kukutana na anga, akaanza kuona moshi, kisha bendera, halafu milingoti na hatimaye meli. Hilo likamtambulisha kuwa dunia ilifanana na mpira.

Hashtagi kwa Waziri wa Maendeleo ya Vijana, Joel Nnauka.