Joto kampeni za uchaguzi Uganda lapanda, Museveni akacha mdahalo

Kampeni za uchaguzi nchini Uganda zimezidi kupamba moto kuelekea uchaguzi mkuu wa Januari 15, 2025 ambapo Rais Yoweri Museveni anayetetea nafasi hiyo akishindana kwa karibu na wagombea wengine.

Museveni anagombea tena muhula wa saba akiwa ni Rais wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki, akiwa ameliongoza taifa hilo tangu mwaka 1986 alipoingia madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi akiongoza kikundi cha NRM ambacho sasa ni chama cha siasa.

Ukiwa umebakia mwezi mmoja na wiki mbili pekee kufanyika kwa uchaguzi huo, kampeni zimeshika kasi ambapo upinzani mkali upo baina na Museveni na mgombea wa chama cha NUP, Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine.

Chama cha NUP kimedai kuwa mamia ya wafuasi wa mgombea wake wa urais, Bobi Wine, wamekamatwa na vyombo vya usalama wakati wa mikutano ya kampeni iliyoendelea katika maeneo ya Kampala na Mukono.

Kwa mujibu wa msemaji wa NUP, ukamataji huo umetokea wakati Bobi Wine akiendelea na ziara zake katika ngome kuu za upinzani, hatua ambayo chama hicho kimeitaja kuwa ni “mkakati wa serikali kuwatisha wapigakura.”

Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini humo aliwatuhumu waandaaji wa kampeni hizo kuendesha “msafara haramu” na kudai kuwa askari waliingilia kati kurejesha utulivu na kuzuia uvunjifu wa amani.

Bobi Wine anajaribu tena kumng’oa madarakani Rais Museveni, ikiwa ni jaribio lake la pili baada ya kumaliza nafasi ya pili katika uchaguzi wa mwaka 2021.

Uganda inatarajiwa kufanya uchaguzi mkuu Januari mwakani, ambapo wapiga kura watachagua rais mpya pamoja na zaidi ya wabunge 500.

Rais Museveni na mpinzani wake mkuu, Bobi Wine, wameendelea kuvutana katika kampeni za kuelekea uchaguzi wa urais wa Januari 15, 2026, huku kila mmoja akijaribu kupenya kwenye ngome ya mwenzake na kupangua ujumbe wake wa kisiasa.

Museveni, ambaye ametumia siku tano katika eneo la Bugisu, amewataka wakazi wa Mbale kuwakataa “watalii wa siasa” wanaojitokeza wakati wa uchaguzi bila kuwa na uwezo wa kuleta maendeleo ya kweli.

Ametumia kampeni hizo kusisitiza mpango wa kuongeza utajiri wa kaya, kuchochea viwanda vinavyotokana na kilimo na kuimarisha miundombinu ili kutokomeza umaskini na udhaifu wa kiuchumi.

Amedai kuwa yeye pekee ndiye “anayeweza kuhakikisha maendeleo ya uhakika na mageuzi ya kiuchumi,” akisisitiza kuwa utegemezi mkubwa wa kilimo cha kujikimu—ambacho kinafanywa na zaidi ya asilimia 70 ya kaya nchini humo—utamalizwa kupitia Parish Development Model (PDM).

“Bugisu ina ardhi, mvua na mazao. Kinachokosekana ni nidhamu katika kuchagua shughuli za kiuchumi,” alisema akiwa Sironko. “Huwezi kutoka kwenye umaskini kwa kufanya kilimo kidogo kilichogawanyika.”

Alitaja mazao kama kahawa, ufugaji wa maziwa, uyoga na matunda kuwa ni nyenzo muhimu za kukuza utajiri. Hata hivyo, wakazi walimkumbusha changamoto ya upatikanaji wa masoko kutokana na ubovu wa miundombinu ya barabara.

Museveni aliahidi kukarabati barabara ya Mbale–Lwakhakha, inayowaunganisha wakulima na soko la Kenya.

Kwa kuwa Bugisu iko karibu na soko kubwa la Kenya, ina vivutio vya utalii katika Mlima Elgon na fursa za biashara za mipakani, ahadi ya Rais ya kuendeleza Kituo cha Viwanda na Biashara cha Mbale—ambacho kinatarajiwa kutoa ajira kwa zaidi ya vijana 20,000 katika miaka 10 ijayo—ilipokelewa kwa shangwe.

“Uanzishwaji wa viwanda utapunguza pengo la ajira. Ni viwanda pekee vitakavyoweza kuibeba nguvu kazi ya vijana na kuongeza thamani ya mazao yetu,” alisema.

Novemba 30, 2025, wagombea watano wa urais nchini Uganda waliketi pamoja, wakitenganishwa kwa umbali usiozidi mita moja, katika mdahalo adimu wa kitaifa uliodumu hadi usiku wa Jumapili na kuchomoza ndani ya miongo ya mvutano wa kisiasa, hofu ya kiuchumi na kutokuaminiana kwa wananchi kwa taasisi zao.

Mdahalo huo uliorushwa moja kwa moja na NTV Uganda na Spark TV, na pia kurudiwa hewani kupitia KFM na Dembe FM, ulikuwa wa kwanza wa midahalo ya urais kuelekea uchaguzi wa Januari 15, 2026 — na kwa mara ya kwanza nchini humo, ukijumuisha uhakiki wa taarifa papo hapo.

Ndani ya ukumbi huo uliosheheni utulivu, mwanga hafifu na usanifu uliopangwa kwa uangalifu, hali ilikuwa ya tahadhari kana kwamba taifa lilikuwa kwenye mduara wa sintofahamu huku wafuasi wa chama tawala cha NRM wakisusia tukio hilo, zikiwa zimesalia siku 46 kabla ya uchaguzi.

Rais Yoweri Museveni, aliyeiongoza Uganda tangu 1986, ndiye aliyekosekana usiku huo. Timu yake ya kampeni ilithibitisha kupokea mwaliko wa NMG takriban siku 10 kabla, lakini ikasema kwamba Rais alikuwa na “majukumu mengine ya kampeni.”

Badala yake, NRM ilisukuma tukio mbadala: kipindi kilichorekodiwa cha mtandaoni, “Gen Z Podcast,” kilichoonyeshwa na UBC saa 3 usiku, kikionekana kama maudhui mepesi ya kumtambulisha Rais kwa vijana.

Kutokuwepo kwake kulichochea mjadala mkali, ndani na nje ya ukumbi, hasa mitandaoni. Wagombea wengine wadogo, Robert Kasibante wa National Peasants Party na Mubarak Munyagwa Sserunga wa Common Man’s Party (CMP), nao pia hawakuhudhuria.

Katika mdahalo huo, Bobi Wine alianza kwa hatua ya kumshambulia, akisema: “Museveni hayupo hapa kwa sababu yeye ni wa jana, sisi tunazungumza kuhusu kesho.”

Kaulimbiu ya kwanza ilikuwa uchumi, ukuaji, na ajira za vijana — mada iliyovuruga meza mara moja.

Bobi Wine alitaja tatizo la uchumi kama linalosababishwa na “kutengwa kwa wananchi na hujuma za kimfumo.”

Aliahidi kuzalisha ajira milioni 10 kupitia sekta ya ubunifu, utalii, na kukuza biashara ndogo na za kati (SMEs).

Pia, aliahidi kupunguza gharama za kufanya biashara, kukarabati miundombinu ya usafiri, kupitia upya mikataba ya kimataifa, na — kauli iliyoshangiliwa — kutia saini Muswada wa Mishahara ya Kima cha Chini uliocheleweshwa kwa miaka.

“Haya si mambo ya kufikirika. Vijana wengi wameshindwa na mfumo huu. Tunapaswa kuwawezesha wajasiriamali wadogo,” alisema.

Frank Bulira Kabinga wa Revolutionary People’s Party (RPP) alisema matatizo ya uchumi nchini humo ni “dalili za maradhi ya kisiasa,” akimtaja Museveni na mfumo wake kama chanzo kikuu cha kudumaa kwa taifa.

Alipendekeza Uganda igawanywe katika majimbo 16 ya kijimbo (federal), akisema hatua hiyo itapunguza ufisadi na kufanya maamuzi ya kiuchumi kuwa ya karibu zaidi na wananchi.

Mgombea wa FDC, Nathan Nandala Mafabi, aliwakumbusha watazamaji kuwa zaidi ya asilimia 70 ya Wauganda wanategemea kilimo.

“Uganda tumezoea kuandika mapendekezo, si kutekeleza,” alisema, akiahidi kuwekeza kwenye mafunzo ya kilimo, Tehama, ujenzi na uchakataji mazao.