Dar es Salaam. Mfanyabiashara wa vipodozi, Jenifer Jovin, maarufu Niffer, aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya uhaini, ameachiwa huru baada ya kusota mahabusu kwa siku 38 akieleza aliyoyaona gerezani, hajihusishi na siasa na hana chama.
Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuachiwa huru amesema:
“Kwanza namshukuru Mungu kwa siku ya leo, ni siku nzuri nimerudi kuungana na familia yangu tena. Haikuwa safari rahisi, lakini namshukuru kwa kila kitu, kikubwa tu mimi sina chama chochote cha siasa, na wala sijihusishi na siasa kwa namna yoyote ile, ni mwananchi tu wa Tanzania.”
“Kwa hiyo, hata wakati nafanya baadhi ya vitu vilivyopelekea mambo yote yameweza kutokea, baadhi ya vitu ni kutokuelewana tu. Lakini sipo kabisa katika siasa, namshukuru Mungu kwamba uchunguzi umefanyika na msamaha wa Rais umeweza kupita. Vitu vimeweza kuwa vyepesi na leo niko nyumbani,” amesema.
Amewashukuru waliosimama naye kipindi chote cha matatizo na kueleza:
“Zaidi ya yote nishukuru mamlaka zote na nimshukuru mama yangu kipenzi. Nilipata taarifa nikiwa ndani bado sijapata kuona vyote, ni vingi maana akili yangu mwenyewe kwa sasa sipo katika mood ya kuzungumza sana.”
“Mama yangu kwa namna alivyonipigania kama mzazi, familia yangu, marafiki zangu pamoja na Rais. Zaidi ya yote niwashukuru Watanzania ambao waliweza kufika magereza na walionisapoti kwa chochote, nawashukuru kwa upendo wenu,” amesema.
Amesema ni vyema jamii kukumbuka wafungwa kwa kupeleka misaada gerezani.
“Nililoona ni kuwa mnaweza kupeleka misaada kwa watoto yatima, lakini misaada inaweza kupelekwa hata magereza. Kwa hiyo kwa watu mtakaopata nafasi pelekeni misaada magereza pampasi za watoto, pedi za kina mama, maziwa kuna watoto wachanga kule, ndala, nguo pelekeni kule misaada, hilo ndilo la muhimu nililoliona kwanza,” amesema.
“Nimejifunza kushukuru. Kuna vitu unavifanya unakuwa huru kama hivi unaona tu ni kitu cha kawaida lakini thamani ya uhuru ni kubwa. Thamani ya amani ni kubwa sana unapokuwa huwezi kugusa hata simu, unapokuwa huwezi kwenda chooni peke yako mpaka mtu akutizame unafanya nini si maisha mazuri.”
Mwanaisha Isack, mama wa Niffer ameonesha furaha ya kumpokea binti yake uraiani akisema:
Mama mzazi wa Jennifer Jovin (26) maarufu kama Niffer akimkumbatia mwanae baada ya kufutiwa kesi ya Uhaini katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo. Picha na Michael Matemanga
“Kwanza namshukuru Mungu lakini pia narejea kwa magoti kwa kumuombea binti yangu msamaha. Nimefurahi mama nilikuja mbele yako nikiwa na hali mbaya siku hiyo nilikuwa naumwa lakini nikaona njia pekee ya kumsaidia binti yangu ni kuja mbele yako. Na leo narudi mbele yako Rais Samia Suluhu Hassan nakushukuru kwa msamaha wako.”
“Hatimaye leo niko na binti yangu. Kama nilivyoelezea mengi kuhusu mwanangu ndivyo ninavyojisikia furaha ninavyomuona mwanangu. Familia yote imenituma tena leo nije nikushukuru maana bila ya kauli yako sidhani kama ningekaa hapa na mwanangu,” amesema.
Amesema kipindi chote alichokamatwa Niffer kimemuathiri kwani amekuwa akilazwa kwa matibabu.
“Ninaimani hivi sasa nitakaa sawa. Ninawaomba wanangu kama alivyokuwa Niffer kabla hajafanya chochote kumbuka nyumbani, kumbuka ulipotoka. Mimi nimetoka Bukoba haraka baada ya kusikia shida za binti yangu. Mnafanya vitu kwa upande wenu lakini hamjui mnatuumiza na kutuathiri wazazi,” amesema:
“Nina shida maradhi yangu yamepanda kuliko yalivyokuwa, nawaomba mtafakari kabla hamjafanya mambo, yaani msifanye mambo kwa kukurupuka, mtuhurumie sisi mtatuua.”
Niffer na mwenzake, Mika Chavala, waliotetewa na wakili Peter Kibatala, wameachiwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, leo Jumatano, Desemba 3, 2025, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuwafutia mashtaka.
Uamuzi huo baada ya kutolewa ulipokewa kwa furaha na washtakiwa, ndugu, jamaa na marafiki waliofika mahakamani kufuatilia mwenendo wa kesi iliyopangwa kwa ajili kutajwa.
Niffer aliyevaa baibui nyeusi, mtandio mweusi kichwani, viatu vya mikanda vyenye rangi nyeupe, mkononi akiwa na tasbihi nyeupe pamoja na wenzake walifikishwa mahakamani saa 3:45 asubuhi na kupelekwa mahabusu ya Mahakama.
Baadaye shauri liliitwa chemba ambako waliachiwa huru, kisha wakarejeshwa mahabusu ya Mahakama kusubiri taratibu nyingine kabla ya kuachiwa huru.
Akiwa na mkoba mweusi alipotoka mahabusu akiwa huru, Niffer amepokewa na mama yake aliyemkumbatia kwa sekunde kadhaa huku akilia, kisha alisalimiana na ndugu, jamaa na marafiki.
“Thank you, God bless you, thank you so much, God bless you (asanteni, Mungu awakubarikini, asanteni sana, Mungu awabariki),” amesema Niffer, huku akiingia kwenye gari na kuondoka.
Kwa upande wake, Chavala ametoka mahabusu akisindikizwa na maofisa wa polisi hadi kwenye gari binafsi. Kabla ya kuondoka ametoa shukrani kwa Mungu na Watanzania.
“Mungu ni mwema. Namshukru lakini bado akili inafikiria mengi. Asante sana kwa Watanzania, asante kwa kila mmoja ambaye alikuwa anatuombea na kutupigania, Mungu awabariki sana,” amesema.
Baada ya kauli hiyo ameondoka mahakamani akiongozana na askari polisi.
Mpaka anaachiliwa huru leo, Niffer alikuwa ameshakaa mahabusu siku 38, kati ya hizo, 10 akiwa mahabusu ya polisi na 28 katika Gereza la Segerea baada ya kupandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka yaliyokuwa yakimkabili.
Awali, Niffer alikamatwa na polisi Oktoba 27, akapandishwa kizimbani Novemba 7, 2025 pamoja na wenzake 21, wakihusishwa na kuhamasisha na kushiriki maandamano ya siku ya uchaguzi, Oktoba 29, 2025, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya.
Katika kesi hiyo uchunguzi wa awali (PI) namba 26388 ya mwaka 2025, yenye mashtaka matatu, Niffer alikabiliwa na jumla ya mashtaka mawali, moja la kula njama kutenda kosa la uhaini linalomhusisha yeye na wenzake 21 na lingine la uhaini linalomhusu yeye peke yake.
Katika shtaka la kwanza, mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Clemence Kato alidai washtakiwa wote (Niffer na wenzake) kwa nyakati tofauti kati ya Aprili Mosi na Oktoba 29, 2025 walikula njama za kutenda kosa la uhaini.
Katika shtaka la pili, alidai washtakiwa 21 wenzake na Niffer, Oktoba 29, 2025 katika maeneo mbalimbali wilayani Ubungo, Dar es Salaam wakiwa chini ya utii wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walitengeza nia ya kuzuia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Kato alidai walitengeneza nia hiyo kwa lengo la kuitisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuithibitisha kwa kusababisha hasara kubwa kwa mali za Serikali zilizokusudiwa kutoa huduma muhimu.
Shtaka la tatu ambalo ni la uhaini lilimhusu Niffer pekee aliyedaiwa kati ya Agosti mosi na Oktoba 24, 2025 katika maeneo mbalimbali ya jijini Dar es Salaam, akiwa chini ya utii wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitengeneza nia kwa kuushawishi umma kuzuia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa kusudi la kuitisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alidaiwa alithibitisha nia hiyo kwa kuuhamasisha umma kununua barakoa za kujikinga na mabomu ya machozi kutoka dukani kwake kwa lengo la kujikinga na mabomu ya machozi ya polisi wakati wa maandamano yasiyo halali yaliyolenga kuzuia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya aina hiyo, isipokuwa katika hatua ya uchunguzi wa awali kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu baada ya upelelezi kukamilika, ambayo ndiyo ina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Kwa kuwa shtaka la uhaini halina dhamana, walipelekwa mahabusu, kusubiri kukamilika kwa taratibu nyingine kabla ya kesi yao kuhamishiwa Mahakama Kuu.
Novemba 25, 2025 washtakiwa 20 kati yao waliachiwa huru baada ya DPP kuwafutia mashtaka kwa mamlaka aliyonayo chini ya kifungu cha 92 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA), Marejeo ya mwaka 2023.
Mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Titus Aron, aliieleza Mahakama kuwa kesi ilikuja kwa ajili ya uamuzi kuhusu dosari za hati ya mashtaka lakini DPP hana nia ya kuendelea na kesi dhidi ya washtakiwa 20.
Hivyo walibakia wawili pekee, Niffer na Chavala ambao kesi dhidi yao ilipangwa kutajwa leo Desemba 3, 2025, ambayo ilipoitwa wakili Aron alieleza DPP hana nia ya kuendelea na mashtaka dhidi yao, kisha Hakimu Lyamuya akaamuru waachiliwe huru.
“Mahakama inakubaliana na ombi la upande wa Jamhuri kama lilivyowasilishwa, hivyo inawaachia huru washtakiwa hawa wawili, ” alisema.
Mbali ya Niffer na Chavala, washtakiwa wengine 51 waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka hayo wameachiwa huru baada ya DPP kuwasilisha mahakamani hapo hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi dhidi yao.
Washtakiwa hao wamefutiwa mashtaka na Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga kesi ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Wakati huohuo, washtakiwa 18 wa makosa ya uhaini jijini Dodoma wameachiwa huru wakiwa ni miongoni mwa 83 waliokamatwa na kuwekwa mahabusu kwa kuandamana na kufanya vurugu Oktoba 29, 2025.
Washtakiwa wengine 65 watafikishwa mahakamani kesho Desemba 4, kujua hatima yao.
Walioachiwa huru wameamriwa na Mahakama kuripoti kwa mpelelezi wa makosa ya jinai Wilaya ya Dodoma Mjini (OC-CID) mara moja kwa wiki, siku ya Jumatatu saa 2:30 asubuhi na atakayeshindwa kutimiza sharti hilo atakuwa amefanya kosa la kudharau amri kamili ya Mahakama, hivyo atachukuliwa hatua za kisheria.
Awali, mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali, Rachel Tulli, aliwasilisha taarifa kuwa DPP hana nia ya kuendelea na shauri hilo.
“Kwa kuwa washtakiwa wana rekodi za uhalifu OC-CID ameomba wawekwe chini ya uangalizi kwa muda wa miezi sita, watakuwa wanaripoti kwa wiki mara moja, lengo likiwa ni kuweka Jiji katika hali ya usalama na kuangalia mienendo yao kama wamejirekebisha,” amesema.
Hoja hiyo ilipingwa na wakili wa washtakiwa hao, Anselm Mwampoma, aliyesema dhana hiyo ni ya kufikirika kwa kuwa haina ushahidi kuwa washtakiwa hao huwa wanajihusisha na vitendo vya uhalifu. Ameiomba Mahakama wawe wanaripoti mara moja kwa mwezi na kama ikiwa wanaripoti kwa wiki mara moja basi muda upunguzwe hadi miezi mitatu badala ya miezi sita.
“Kuripoti kila wiki kwa kipindi cha miezi sita ni kuwapunguzia muda wa kufanya shughuli zao za uchumi, nashauri wawe wanaripoti mara moja kwa mwezi na kama ikiwa ni lazima waripoti kila wiki mara moja basi muda upungue kutoka miezi sita hadi mitatu, kwa sababu miezi sita ni mingi sana,” amesema.
Akitoa uamuzi, Hakimu Mkazi Mkuu, Denis Mpelembwa amesema kulingana na kiapo kilichowasilishwa mahakamani na OC-CID wa Wilaya ya Dodoma Mjini washtakiwa wote 18 wameonekana kuwa wamekuwa wakitenda makosa ya uhalifu wa kujirudia ikiwamo wizi, unyang’anyi wa kutumia nguvu na kuvunja nyumba za watu hivyo wanatakiwa kuwa chini ya uangalizi kwa kipindi cha miezi sita.
Mpelembwa amesema kutokana na kiapo hicho amewataka washtakiwa hao kuonesha tabia njema wanapokuwa nje kwa kutokutenda makosa na pia kuripoti kila Jumatatu saa 2:30 asubuhi kwa OC-CID kwa kipindi cha miezi sita kuanzia leo (Desemba 3) na atakayevunja sharti hilo atakuwa amekwenda kinyume cha amri halali ya Mahakama hivyo atashtakiwa kwa kuidharau mahakama.
Imeandikwa na Hadija Jumanne, James Magai, Aisha Lungato (Dar) na Rachel Chibwete (Dodoma)
