Dar es Salaam. Licha ya Desemba kuwa na historia ya changamoto ya usafiri kutoka Dar es Salaam kwenda mikoani, mwaka huu imekuwa zaidi ya kawaida, kwani idadi kubwa ya abiria imeshuhudiwa, huku baadhi wakikwama kusafiri.
Kwa mujibu wa watoa huduma za usafiri wa mikoani, idadi ya abiria wanaosafiri sasa kutoka Dar es Salaam kwenda mikoani ni zaidi ya kawaida. Hali kama hiyo mara nyingi hushuhudiwa kuanzia Desemba 20.
Wakizungumza na Mwananchi leo Jumatano, Desemba 3, 2025, watoa huduma hao wamesema mwaka huu, mafuriko ya abiria yameanza mwishoni mwa Novemba na mwanzoni mwa Desemba, hali inayozua swali, kwanini mapema zaidi ya kawaida?
Wapo wanaohusisha hali hiyo na tishio la kiusalama katika Jiji la Dar es Salaam, eneo lililopangwa kuwa kitovu cha maandamano ya Desemba 9, kwa mujibu wa taarifa katika mitandao ya kijamii.
Hofu hiyo inajengwa na kumbukumbu za maisha magumu waliyopitia wakazi wa Dar es Salaam wakati wa maandamano yaliyozaa vurugu ya Oktoba 29, yaliyosababisha vifo, majeruhi, na uharibifu wa mali za umma na binafsi.
Katika vurugu hizo, Jeshi la Polisi lilitoa amri ya wananchi kutotoka nje kuanzia saa 12 jioni, iliyodumu kwa takriban siku tano. Baadhi yao walitaabika kwa kukosa chakula na huduma nyingine muhimu.
Hata hivyo, Desemba 2, Rais Samia Suluhu Hassan alitangaza hakikisho la usalama katika jiji hilo na maeneo mengine, akisema Serikali imejipanga kudhibiti matukio hayo wakati wowote.
Mmoja wa wasafiri, Daniel Michael, aliyekuwa anatokea Tanga kuelekea Moshi mjini, amesema ameshuhudia magari mengi binafsi yakiingia mkoani Kilimanjaro, jambo ambalo si la kawaida kwa tarehe hizo.
“Tunajua Desemba hii wakazi wengi wa Kilimanjaro, hususan Wachaga, hurudi kwao kwa ajili ya sikukuu za mwisho wa mwaka, lakini si kwa tarehe hizi, ni kuanzia katikati ya Desemba. Sijui kwa nini safari hii wanawahi hivi,” amesema.
Katika Njiapanda ya Himo kuanzia saa 10 alasiri, kumeonekana magari yenye namba mpya (E), yaliyotokea Tanga au Dar es Salaam, yakielekea maeneo ya Mwika, Marangu, Kilema, Wilaya ya Moshi, na Rombo.
Mbali na Njiapanda ya Himo, katikati ya Mji wa Moshi kumeanza kuonekana magari mageni ambayo kwa kawaida huonekana kuanzia katikati ya Desemba hadi Januari 3, na baadhi ni wageni wa barabara.
Maria Mageni alitarajia kusafiri na familia yake kuanzia Desemba 15 kwenda Magu, mkoani Mwanza, lakini mumewe amelazimika kubaki Dar es Salaam baada ya kukosa tiketi, ikidaiwa zimeisha.
Safari yake inasababishwa na kile alichoeleza kuwa amejifunza kwa matukio ya Oktoba 29, hivyo anaondoka mapema ili kuepuka hali zinazotarajiwa kuanza Desemba 9.
“Nilipanga kuondoka Desemba 15, lakini kutokana na funzo nililolipata Oktoba 29, nilijifungia muda wote. Kinachosemekana kinaenda kutokea kimeniambia niwahi kijijini,” amesema.
Maisha yake wakati wa vurugu hizo, amesema yalikuwa magumu kwa kuwa alikosa hata chakula na kulazimika kusaidiwa na wapangaji.
“Mazingira ya Dar es Salaam na kinachosemekana kinapangwa kutokea hayawezekani. Ni bora niwahi kijijini kwa ndugu zangu na familia,” amesema Maria.
Kama ilivyo kwa Maria, Shadrack Mwakareli naye amefungasha virago kulikimbia Jiji la Dar es Salaam kwenda kijijini Tukuyu, mkoani Mbeya, akisema ni salama zaidi.
“Kupata chakula Dar es Salaam si rahisi. Hadi mazingira yakichafuka unaweza kufia ndani. Maandamano haya yanayosemekana kuanza Desemba 9 hayana ukomo. Ni bora nijilinde mapema,” amesema Mwakareli.
Hadi anapoamua kusafiri, amesema ameshapigiwa simu kadhaa na ndugu zake kutoka kijijini, wakimtaka aende kwa maslahi ya usalama wake.
Hata hivyo, malengo ya Mwakareli yanakumbwa na kikwazo, baada ya kukuta mabasi yamejaa na yaliyopo wamepandisha bei kupitiliza.
“Nimefika hapa alfajiri lakini bado sijapata usafiri. Changamoto ni bei za tiketi kupanda sana, lakini hakuna namna, uhai ni muhimu zaidi,” amesema.
Shida ya usafiri imemkabili pia Neema Konzo, aliyesema alikwenda Kituo cha Mabasi cha Magufuli, Dar es Salaam, Jumatatu, akakosa tiketi na kulazimika kukata ya kusafiri Alhamisi.
“Nimenunua tiketi Jumatatu, Desemba mosi. Nilifika Mbezi asubuhi kwa lengo la kusafiri lakini sikupata tiketi, ilinibidi nikate kwanza nikapata ya siku ya Alhamisi, hivyo nilirudi nyumbani kusubiri tarehe ya safari,” amesema Neema, aliyekuwa akisafiri kwenda Njombe.
Joseph Rukamba, anayesafiri kwenda Bukoba, amesema: “Nimefika hapa tangu alfajiri lakini tiketi zimeisha. Nimeambiwa zimejaa hadi Desemba 8. Sitaweza kubaki Dar es Salaam, nitatafuta hata usafiri wa kuunga.”
Amesema matarajio yake ni kufika nyumbani kabla ya Desemba 8, hivyo hataweza kusubiri kwani wazazi na ndugu zake wanampigia simu mara nyingi kumwomba arudi kijijini.
Katika hatua nyingine, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, amewataka wananchi watakaosafiri msimu wa sikukuu kuhakikisha wanaacha waangalizi au walinzi wa maisha na mali zao.
“Vilevile wazingatie sheria za usalama barabarani na kufuata ishara zilizopo ili kuepuka ajali,” amesema.
Mwananchi imeshuhudia idadi kubwa ya watu katika Kituo cha Mabasi cha Magufuli wakizunguka kutafuta tiketi za kusafiri. Waliokuwa wamekalia na wengine kulala mabegi yao, huku watoto wakiwa chini, baadhi wakisubiri hatima ya kusafiri.
Mbali na hilo, Desemba 3, saa 10:00 jioni, Mwananchi imeingia katika tovuti za ukatishaji tiketi za kampuni kadhaa za mabasi zinazofanya safari za mikoani na kushuhudia yakiwa yamejaa.
Katika kampuni ya mabasi ya BM Coach kwa safari ya mkoani Arusha, Desemba 4, mabasi matano kati ya 10 yalijaa, mawili yakiwa na nafasi chache, na lingine la abiria wa hadhi maalumu viti 38.
Kwa kampuni ya mabasi ya Ally’s Star kwa safari ya mkoani Mwanza, Desemba 4, kati ya mabasi manne, mawili yalijaa na moja lilibaki na viti vinne, lingine la hadhi maalumu viti 38.
Kampuni ya mabasi ya Abood kwa safari ya mkoani Morogoro Desemba 4, mfumo wake umeonyesha ‘busy’, ukimaanisha unatumika kwa wengi.
Mmoja wa wakatisha tiketi wa kampuni moja ya mabasi (jia limehifadhiwa) amekiri kuwepo kwa ongezeko la wasafiri na hivyo kusababisha ugumu wa usafiri.
“Sababu mojawapo ni tishio la maandamano ya Gen Z Desemba 9. Baadhi wameona ni bora waondoke Dar es Salaam mapema kurudi Kilimanjaro, hasa ikizingatiwa mkoa wetu haina historia ya vurugu. Huwa ni tulivu,” amesema.
Kutokana na wingi wa abiria, amesema kampuni yao ina mabasi sita yanayofanya safari za mikoani, yote yamejaa, na wameongeza moja la ziada.
Mmiliki wa kampuni ya mabasi ya Kapricon, George Mberesero, amesema mbali na hofu ya maandamano, ugumu wa usafiri unasababishwa pia na wanafunzi wanaohitaji kurudi nyumbani baada ya kufunga shule.
Mwenyekiti wa Umoja wa Mabalozi wa Usalama Barabarani Tanzania (RSA), Mkoa wa Kilimanjaro, Khalid Shekoloa, amekiri ongezeko la abiria wanaotoka Dar es Salaam kwenda Kilimanjaro, akisema baadhi yao ni kwa hofu ya Desemba 9.
“Ni kweli kuna hofu fulani ya kile kilichotokea Oktoba 29 Dar es Salaam. Sasa baadhi wanarudi mapema kabla ya Desemba 7, japo Rais ametoa hakikisho la usalama, bado kuna hofu,” amesema.
Pamoja na hofu, Shekoloa amesema ongezeko la abiria limechangiwa pia na wanafunzi wanaorudi makwao, akisisitiza kuwa baadhi ya wenyeji wa Kilimanjaro wanarudi mapema kwani mkoa wao ni salama.
“Kule (Dar) wana kumbukumbu ya Oktoba 29, watu walifungiwa ndani, maduka yakafungwa kwa siku takriban tano. Mkoa Kilimanjaro ni shwari, hapakuwa na vurugu hizo, ni vijana wachache walijaribu Polisi ikawadhibiti,” amesema.
Msemaji wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Mustapha Mwalongo, amesema kuanzia Desemba mosi, idadi ya abiria wanaohitaji kusafiri kutoka Dar es Salaam imeongezeka kwa kasi.
Kuhusu ukaguzi wa tiketi, Mwalongo amewataka abiria kununua tiketi katika vituo rasmi au kwa mawakala waliotambulika ili kuepuka vitendo vya utapeli kutokana na msongamano.
“Nawasihi abiria kuhakikisha wanakata tiketi katika vituo rasmi au kupitia mawakala wanaotambulika, ili kuepuka usumbufu na hasara,” amesema
Amesema wamiliki wa mabasi kuongeza safari ili wajitahidi kusafirisha abiria wote, lakini ikiwa idadi itazidi, wataomba vibali vya kuongeza mabasi kutoka Mamlaka ya Usafiri Ardhini (Latra).