YANGA inafurahia sare ya ugenini iliyoipata kule Algeria Ijumaa iliyopita katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika Kundi B, lakini matokeo hayo yameitibua hali ya hewa JS Kabylie, huku kiungo wa zamani wa Simba, Babacar Sarr akifichua tatizo lilianzia kwa Djigui Diarra.
Kiungo huyo aliyejiunga na Simba dirisha dogo la usajili msimu wa 2023-2024 na kucheza kwa nusu msimu kisha akatimkia JS Kabylie, alicheza mechi hiyo dhidi ya Yanga kwa dakika 45 za kwanza na kumpisha Mostapha Rezkallah Bott.
Akizungumza na Mwanaspoti, Sarr amesema sare waliyoipata mbele ya Yanga imewaacha na maumivu makubwa na aliyesababisha hilo ni Diarra.
Sarr amesema kila mmoja katika timu hiyo alishtushwa na ubora wa Diarra, ambaye ameacha gumzo kutokana na namna alivyokuwa kikwazo katika kuruhusu mashambulizi yao kukamilika.
Kiungo huyo raia wa Senegal, alifichua baada ya mechi hiyo walikutana na makocha wao kuangalia namna walivyocheza na kugundua Diarra alikuwa bora, akiokoa mashambulizi sita.
“Ukweli, matokeo yale hatukuyatarajia kabisa. Tulijua baada ya kupoteza ugenini tunarudi nyumbani kushinda. Tulifanya kila lililowezekana lakini haikuwa siku yetu,” amesema Sarr.
“Nadhani Yanga wanatakiwa kumshukuru sana kipa wao (Diarra). Alikuwa na dakika 90 bora sana. Baada ya mimi kutoka, pale benchi kila wakati tulikuwa tunawakumbusha wenzetu namna ya kutulia ili watumie nafasi.
“Mechi ilipomalizika kesho yake tulifanya kikao cha kuangalia namna tulivyocheza ule mchezo, tulikosea wapi na tukaonyeshwa jinsi kipa wao alivyofanya kazi kubwa akiokoa mashambulizi sita.”
Aidha, Sarr aliongeza kuwa mbali na ubora wa Diarra, Yanga pia ilicheza kwa nidhamu kubwa na mpaka sasa mashabiki wao wanaendelea kulalamika kutokana na matokeo hayo.
“Yanga walicheza vizuri. Hatukudhani kama wangetupa mechi ngumu kama ile. Walikuwa na mpango mzuri. Tutakutana nao kwenye mechi ya mwisho ya makundi.
“Huku (Algeria) bado mashabiki wetu hawana raha kabisa. Kila unapopita wanalalamika kutokana na nafasi ile na mimi wanauliza kwa nini nilikosa ile nafasi ya kipindi cha kwanza ambayo nayo kipa wao aliicheza kwa umakini,” amesema Sarr.
Yanga imefikisha pointi nne katika Kundi B sawa na Al Ahly baada ya kila moja kucheza mechi mbili, JS Kabylie na AS FAR Rabat zina pointi moja.
