Mwanza. Wakati madiwani wa Manispaa ya Ilemela, Mkoa wa Mwanza wakimchagua Sara N’ghwani kuwa Meya na Kurthum Abdallah kuwa Naibu Meya, viongozi hao wamesisitiza umuhimu wa kuwa na amani wakisema mpaka sasa kuna watu wanaishi kwa wasiwasi.
Wilaya ya Ilemela ni miongoni mwa maeneo yaliyokumbwa na maandamano yaliyozaa vurugu wakati na baada ya uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025 ambapo ofisi na mali za umma na binafsi zilichomwa moto.
Meya N’ghwani amesisitiza amani mara mbili jana Jumanne Desemba 2, 2025 baada ya kushinda na wakati akifunga kikao cha kwanza cha baraza la madiwani katika manispaa hiyo.
“Tudumishe amani yetu ya Tanzania…bila amani tutakimbia miji yetu bila sababu za msingi, nina wasihi sana kila tutakapokwenda tuzungumze amani.
“Mpaka sasa hivi bado watu tunaishi kwa wasiwasi, lakini mimi naomba viongozi wa dini muendelee kutusaidia huko makanisani kuzungumza na wananchi na sisi tunapokutana na wananchi wetu tutoe huo wosia wa kudumisha amani,”amesema.
Amesema amani ndiyo msingi wa maendeleo na bila amani, huduma muhimu ambazo wananchi wanapaswa kuzipata haziwezi kufikishwa ipasavyo.
“Tukifanya hivyo tutatekeleza matakwa ambayo wananchi wetu wametuagiza kuja kuwasimamia. Nina waahidi kuwa mtumishi mwema wa halmashauri hii ya Ilemela.
“Naomba sana Mwenyezi Mungu atubariki sote lakini tudumishe amani yetu ya Tanzania maana ndiyo kila kitu. Amani ikikosekana hata hizi huduma muhimu wananchi wanapaswa kuzipata hawatozipata,” amesisitiza N’ghwani.
Kwa upande wake, Naibu Meya, Kurthum Abdallah amesema atamshauri Meya na kushirikiana na madiwani wenzake pamoja na Serikali kuhakikisha maendeleo yanapatikana huku amani ikiendelea kutawala.
“Kwa sababu amani ikipotea kila kitu hakiendi. Ndugu zangu tulinde amani ya nchi yetu. Mkijenga imani huzaa imani,” amesema Kurthum.
Katika uchaguzi huo, Sara alipigiwa kura za ndiyo 27 kati ya kura zote kutoka kwa madiwani wa Kata 19 za manispaa hiyo, huku Kurthum akipata kura 24 kati ya 27.
Awali, Mwenyekiti wa shughuli za uchaguzi huo ambaye ni Katibu Tawala wa Ilemela, Anna Mbao amewataka madiwani kutimiza wajibu wao kwa uadilifu na kuhakikisha wanawatumikia wananchi waliowachagua kwa kuwakilisha changamoto zao na kuzifanyia kazi.
Diwani wa a Pasiansi, Regina Rubala amewaomba wananchi wawasaidie kwa kuwapa viongozi wao ushirikiano ili kuwarahisishia kupeleka maendeleo.
Naye, Diwani wa Kitangiri, Donald Ndalo amesema atawatumikia wananchi wake kwa kuhakikisha anachukua changamoto zao, kuzileta kwenye baraza kisha kurejesha matokeo kwao.
Akisoma taarifa ya utendaji kazi wa halmashauri ya manispaa hiyo kwa kipindi cha Juni hadi Oktoba 30, 2025, Mchumi wa Manispaa hiyo, Herbert Bilia amesema bajeti ya mwaka huu wa fedha ya Ilemela ni Sh86.8 bilioni.
“Hadi kufikia Oktoba, tumepokea na kukusanya zaidi ya Sh30.02 bilioni kwa maana ya mapato ya ndani Sh4.9 bilioni, mishahara Sh21 bilioni pamoja na Sh3.3 bilioni ya miradi ya maendeleo na Sh591.8 yakiwa matumizi ya kawaida,” amesema.
