Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imebatilisha uamuzi uliomteua Rosemary Ishengoma kusimamia mali, akaunti za benki na ustawi wa baba yake, Johnson Ishengoma (67), baada ya mtoto huyo kudai mzazi wake hana akili timamu, hivyo hana uwezo wa kusimamia masuala yake ya kifedha.
Uamuzi uliobatilishwa ulitolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Mwishoni mwa Novemba, 2025, Rosemary aliwasilisha maombi mahakamani hapo akaeleza baba yake, Ishengoma hana akili timamu, hivyo akaomba ateuliwe kusimamia akaunti ya benki, mali na ustawi wa baba yake.
Alieleza baba yake Ishengoma (67), ambaye ni mhadhiri katika Chuo Katoliki cha Mbeya, alizimia Septemba 6, 2025 akalazwa katika Hospitali ya Mbeya na baadaye Kairuki, Dar es Salaam.
Rosemary alieleza kuwa, baba yake alipata kiharusi kutokana na mshipa wa damu kwenye ubongo kupasuka, hali iliyosababisha asiwe na akili timamu.
Katika Mahakama hiyo ya chini, alieleza wakati baba yake akiwa amelezwa hospitalini, kuna ndugu yao alitoa Sh3 milioni kutoka akaunti yake kwa kutumia alama ya dole gumba bila ridhaa ya baba yake.
Vilevile, alieleza ndugu wengine walichukua Sh5 milioni kwa matumizi mbalimbali bila kumjulisha.
Rosemary aliieleza Mahakama kuwa baba yake hawezi tena kusimamia mali zake kwa sababu ya hali yake ya akili. Pia,alilalamika kuhusu matunzo duni pale wauguzi au walezi wanapokosekana.
Baada ya kusikiliza maombi hayo, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilimpa Rosemary mamlaka ya usimamia wa mali zote za baba yake, ikiwamo akaunti ya benki na ustawi wake hadi atakaporejesha utimamu wa akili.
Baada ya kupata taarifa za uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Ishengoma alifungua shauri la maombi ya marejeo akisema ana akili timamu.
Katika shauri la maombi ya marejeo lililofunguliwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, Ishengoma alieleza amri iliyotolewa Kisutu ilitokana na madai ya uongo.
Alidai Mahakama hiyo ya chini ilishindwa kufanya uchunguzi stahiki na kushindwa kumpa yeye au ndugu zake nafasi ya kusikilizwa.
Alidai Mahakama haikufuata taratibu sahihi na sasa hawezi kufikia mali zake kwa ajili ya mahitaji yake ya msingi.
Ishengoma alieleza usimamizi wa mjibu maombi (binti yake Rosemary) juu ya mali zake ni hatari kwa maisha yake.
Pande zote mbili katika shauri hilo zilipokutana Novemba 26, 2025. Mjibu maombi (Rosemary) aliagizwa kuwasilisha kiapo kinzani ndani ya siku mbili, usikilizwaji ulipangwa kufanyika 28 Novemba 28.
Siku hiyo, mjibu maombi alifika akiwa na wakili, Daniel Kalasha aliyeomba shauri kuahirisha kwa siku tano ili kuwasilisha kiapo kinzani pasipo kutoa sababu ya kushindwa kutekeleza amri ya awali. Ombi lake lilikataliwa. Aliruhusiwa kujibu kwa hoja za kisheria pekee.
Wakili wa mwombaji, Ludovick Nickson, alibainisha kuwa hakuna cheti cha kitabibu kilichowasilishwa kuthibitisha kuwa mwombaji (Ishengoma) alilazwa kutokana na ugonjwa wa akili.
Pia, alieleza siyo mwombaji au ndugu zake walioitwa kama inavyotakiwa chini ya kifungu cha 20(2) cha Sheria ya Afya ya Akili.
Alidai Mahakama haikujiridhisha chini ya kifungu cha 20(1) kwamba mwombaji alilazwa, wala hakuna cheti cha kitabibu kutoka kwa daktari mwenye sifa kama kinavyotakiwa na vifungu 23(1) na 19(3).
Wakili Nickson aliomba haki ya mwombaji irejeshwe na aruhusiwe kuendesha mali na akaunti zake, akidai yuko timamu kiakili. Wakili wa mjibu maombi hakuwa na cha kueleza.
Katika hukumu aliyoitoa Desemba mosi, 2025 Jaji Elizabeth Mkwizu, amesema amezingatia maombi, hoja za pande zote, rekodi za Mahakama za chini na sheria.
“Kwa jumla, usimamizi wa mali za watu wasio na akili timamu unasimamiwa na sehemu ya V ya Sheria ya Afya ya Akili, Sura 98. Kifungu cha 19 kinaorodhesha watu wanaoweza kuwasilisha maombi, wakati vifungu 20 na 21 vinahusu utoaji wa taarifa na mahudhurio. Kifungu cha 23 kinahusu uthibitisho wa uwezo wa akili,” amesema.
Jaji Mkwizu amesema: “Hakuna tatizo kuhusu ustahiki wa mjibu maombi kuwasilisha maombi kwani ni mtoto mzima wa mwombaji. Maombi pia yaliambatanishwa na kiapo chenye maelezo ya mali na undugu pamoja na taarifa ya kitabibu.”
Hata hivyo, amesema tatizo linaanzia kwenye utoaji wa taarifa za wito na uthibitisho wa ugonjwa wa akili.
Amesema kifungu cha 20 kinataka mtu anayelengwa na maombi apewe taarifa isipokuwa kama ni lazima kutofanya hivyo.
“Rekodi zinaonesha mwenendo ulikuwa wa upande mmoja. Novemba 10, 2025 mjibu maombi na wakili wake walifika mahakamani bila mwombaji. Wakili alieleza Mahakama kuhusu dharura, akisema Johnson Ishengoma ana matatizo ya kumbukumbu na hawezi kusimama au kutembea na kwamba fedha zinahitajika kwa matibabu na uangalizi,” amesema jaji.
Amesema hakimu bila kutaka taarifa kwa mwombaji au ndugu zake wala kutoa sababu za kutotoa taarifa, alitoa amri ya kukubali maombi.
“Hili ni kosa kubwa linalokiuka sheria na haki ya msingi ya kusikilizwa chini ya Ibara ya 13(6)(a) ya Katiba. Mahakama ya Rufaa imesisitiza mara nyingi kuwa kukosa kusikilizwa ni uvunjifu wa haki za kikatiba,” amesema akirejea uamuzi uliofanywa na mahakama katika shauri la Mbeya Rukwa Outposts and Transport Ltd dhidi ya Jestina Mwakyoma (2001) TLR 251.
Amesema licha ya kuwapo ripoti ya matibabu, hakimu hakuitathimini wala kusikiliza ushahidi wowote kuthibitisha hali ya akili ya mwombaji.
“Sheria inataka ushahidi wa kitabibu na Mahakama inaweza kumtaka mlengwa kufika au kuchunguzwa na daktari,” amesema akirejea vifungu 23 na 21.
Jaji amesema: “Kibali cha kuchukua mali za mtu hakiwezi kutolewa bila ushahidi madhubuti kwamba mtu ana ugonjwa wa akili. Bila kufanya hivyo, kuna hatari ya maombi kuwasilishwa kwa sababu za chuki, masilahi binafsi au madai ya kupikwa.”
Amesema katika shauri hilo, hakuna ushahidi wa uchunguzi wa akili uliofanywa na Mahakama ya chini na kwamba, nakala ya taarifa ya kitabibu inaonesha tu kulazwa Hospitali ya Kairuki na ugonjwa wa kiharusi, lakini hakuna hitimisho kuhusu uwezo wake wa akili kama inavyotakiwa na sheria.
“Kwa hiyo maombi mbele ya Mahakama ya chini hayakuwa na msingi wa kutosha kuthibitisha madai hayo. Ninaona kwamba, ombi hili lina mashiko. Mwenendo wote, uamuzi na amri katika maombi namba 28375 ya mwaka 2025 vinafutwa kwa kuwa ni batili,” amesema na kuongeza.
“Hivyo, mwombaji Johnson Ishengoma anarudishwa katika hali yake ya awali na anaruhusiwa kusimamia mali na mambo yake ya kifedha, ikiwa ni pamoja na akaunti ya CRDB namba 01J2052669300 bila usumbufu.”
Jaji Mkwizu amesema kwa kuzingatia uhusiano wa pande hizo, kila upande utajilipa gharama zake.
