Dodoma. Viongozi na wanasiasa nchini, wameaswa kutohubiri amani pekee bila kutaja neno haki, kwani moja kati ya maneno hayo likisimama peke yake huwafanya watu kuwa watulivu kwa muda, huku Watanzania wakielezwa kuwa malezi ya vijana yamo mikononi mwao.
Mchungaji Felix Msumari wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), ametoa kauli hiyo wakati wa kuhitimisha kongamano la kitaifa la viongozi wa dini na wazee lililofanyika jana Desemba 2, 2025.
Kongamano hilo lilihusisha Taasisi ya Mwalimu Nyerere na kuongozwa na Joseph Butiku, likiwa na lengo la kuzungumzia amani ya nchi na hatima ya Tanzania ya kesho.
Mchungaji Msumari amesema amani imekuwa ikihubiriwa kila kona lakini bila ya kutaja haki, jambo linalosababisha watu wengi kuishi na kinyongo katika mioyo yao.
Amesema ukimya wao usichukuliwe kwamba wanakubaliana na kinachoendelea bali wanajengewa usugu.
“Watu wanahubiriwa amani, hawahubiriwi kuhusu haki na kwa kufanya hivyo lazima tutambue amani isiyokuwa na haki ni sawa na utulivu wa muda ila kuna mahali watu watakuja kudai haki yao, maana amani inatumika kama kinga ya kukwepa wajibu,” amesema.
Mchungaji Msumari amesema haki ikiwepo hakutakuwa na utekaji na watu wakiishi kwenye haki hata ukosoaji utakuwa wenye maana bila hofu ambayo watu wamejengewa ili wasiitaje haki.
Amesema kwa sasa baadhi ya viongozi hawataki kuambiwa makosa yao, akatoa ushauri ili kuepuka mambo hayo, Serikali iruhusu uhuru wa vyombo vya habari, wanasiasa na wanaharakati walindwe ili kujiepusha na mambo maovu, ikiwemo vifo.
Akisoma maazimio ya kongamano hilo, Dk Musuto Chirangi, ametaja mambo manne waliyokubaliana kwenye kusanyiko hilo, ikiwemo kuitaka Tume ya Uchunguzi kutoa taarifa kamili ya vifo na mali zilizoharibiwa kwenye machafuko ya Oktoba 29, 2025.
Mengine ni kuomba uanzishwe haraka mchakato wa Katiba mpya ukihusisha vyama vyote na makundi mbalimbali, viongozi wawajibike kwa matendo yao na Serikali iendelee kusimamia haki na usawa wa raia.
Wameomba kila mtu kujiepusha na kukemea matamko na vitendo vya kibaguzi na vinavyohamasisha ubaguzi wa kidini, kisiasa na ukabila.
Mwenyekiti wa kikao hicho, Joseph Butiku amesema maandamano ni haki ya kila raia isipokuwa yanapotokea yawe ya amani, pasipokuwa na mauaji wala matumizi ya nguvu na waandamanaji wasianzishe vurugu za uvunjifu wa amani.
Butiku amesema Taifa lolote linajengwa kwa amani, umoja na maendeleo kwa watu wote bila kujali itikadi zao.
Amewaomba Watanzania kutambua kuwa jukumu la utulivu wa nchi na malezi ya vijana lipo mikononi mwao.