Meya Uzairu aahidi Temeke ya viwango

Dar es Salaam. Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Temeke leo Jumatano, Desemba 3, 2025 limekutana kwa mara ya kwanza na kuunda rasmi safu yake ya uongozi kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Kikao hicho pia kumeshuhudiwa uchaguzi wa viongozi wakuu wa baraza hilo ambapo Uzairu Athumani amechaguliwa kuwa Meya na Nuru Cassian kuwa Naibu Meya, muda mfupi baada ya madiwani hao kuapa kiapo cha uaminifu.

Akitoa mwelekeo wa baraza hilo, Meya Uzairu ameahidi kuiongoza Temeke kuwa halmashauri ya viwango, akisema amejipanga kusimamia utendaji uliotukuka na maendeleo ya manispaa hiyo.

Ametaja kuwa katika kipindi chake atasimamia vipaumbele vinne muhimu vinavyoelekeza dira ya utendaji wa baraza hilo.

Madiwani kutoka kata mbalimbali za Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam wakiwa katika kakao chao cha kwanza cha Baraza la halmashauri ya wilaya hiyo leo Jumatano Disemba 3, 2025.

Amesema kipaumbele cha kwanza ni kuhakikisha utekelezaji wa ahadi za siku 100 za Rais Samia unafanyika ndani ya Temeke, zikiwemo huduma ya bima za afya kwa wazee na watoto, utoaji wa Sh200 bilioni kwa mikopo, ajira katika sekta ya afya na elimu pamoja na marufuku ya kuzuiliwa kwa miili ya marehemu hospitalini.

Amesisitiza kuwa haki za msingi za wananchi, ikiwemo upatikanaji wa huduma za maji, ni mambo ambayo baraza lake litayapa kipaumbele ili kuzifanya taasisi za utoaji haki kutekeleza wajibu wao ipasavyo.

Katika kipaumbele cha pili, Uzairu amesema baraza litasimamia matumizi ya rasilimali fedha na rasilimali watu kwa masilahi ya wananchi.

Kipaumbele cha tatu alichokitaja ni utekelezaji wa miradi ya halmashauri, akisisitiza umuhimu wa kupanga kazi kwa umakini na kuharakisha mchakato wa mipango na manunuzi, ili kuepuka changamoto zinazowakwamisha madiwani kutekeleza ahadi zao.

Katika kipaumbele cha nne, Uzairu ameweka msisitizo kwa vijana, akisema wingi wao ndani ya manispaa hiyo unahitaji uongozi wa kasi katika utoaji wa fursa za ajira, uwezeshaji na mikopo, sambamba na utekelezaji wa mipango ya wizara mpya ya vijana.

Kwa upande wake, Naibu Meya Nuru Cassian amesema atashirikiana na makundi ya wanawake na vijana kuhakikisha huduma na fursa zinazowahusu zinawafikia kwa wakati.

Naibu Meya mpya wa halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, Nuru Cassian, akiomba kura za kuchaguliwa katika nafasi hiyo, leo Jumatano, Disemba 3, 2025.

Kikao hicho kimepokea pia taarifa ya Mkurugenzi wa Manispaa, Jomaary Satura, ambaye amewataka madiwani kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia maelekezo ya Rais Samia kuhusu kuwapa wananchi furaha kupitia huduma bora.

Pia baraza hilo   limeunda kamati mbalimbali za kudumu na zisizo za kudumu kwa mujibu wa sheria na kanuni.

Kamati hizo ni pamoja na Kamati ya Uchumi, Afya na Elimu ambayo imemchagua Mariamu Mtemvu kuwa Mwenyekiti, huku Juma Mkenga akichaguliwa kuongoza Kamati ya Mipango Miji.

Aidha, Kamati ya Kudhibiti Ukimwi imeongozwa na Naibu Meya kama inavyoelekezwa na kanuni huku Bodi ya Vileo ikiongozwa na Meya Uzairu.

Vilevile Bodi ya Ajira imewekwa chini ya Mwanaidi Abdullah, ambaye amechaguliwa kuwa mwenyekiti wake.

Akisoma kanuni za uendeshaji wa Kamati hizo, Meya Uzairu amesema Kamati ya Fedha na Uongozi huongozwa na Meya, na wajumbe wake ni Naibu Meya pamoja na wabunge wa majimbo ya Mbagala, Chamazi na Temeke, hivyo ametangaza kuwa itabaki katika mfumo huo.

Katika salamu za wageni, Hamis Choma, aliyewawakilisha wageni waalikwa amewataka viongozi hao  kupambana na changamoto zinazowakabili wananchi.

Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Temeke, Ally Tamtande, ameonya dhidi ya kujivunia vyeo na badala yake kuwataka viongozi hao kusimamia nafasi zao vyema.

“Nimeona jina Mheshimiwa limeanza kutumika humu leo, niwatahadharishe tu epukeni kutembea na uheshimiwa badala yake tembeeni na shida za watu,” amesema.

Msemaji huyo wa chama ambacho madiwani wote katika halmashauri hiyo wanaotokana nacho, amewataka kuacha siasa za kutazama mwaka 2030.

Katibu Tawala Msaidizi Ukaguzi na Ufuatiliaji kutoka Mkoa wa Dar es Salaam, Saudi Mpili, amewaeleza madiwani kuwa Temeke ni injini ya pili ya uchumi wa Mkoa wa Dar es Salaam na hivyo uongozi wa mkoa unategemea utendaji wao.

“Nawaomba sana madiwani, msaidieni Mkurugenzi kukusanya mapato, kusimamia watumishi na kuepuka migogoro inayotokana na kutofuata sheria na taratibu kwani mkoa unawategemea sana,” amesema.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ye Temeke, Ofisa Tarafa wa Mbagala, Bertha Minga, amewakaribisha madiwani hao katika uongozi wa wilaya akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kwa ajili ya maendeleo ya manispaa hiyo.